Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Fadhili Fabian Ngajilo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iringa Mjini
Primary Question
MHE. FADHILI F. NGAJILO aliuliza: - Je, lini huduma za kibingwa za magonjwa kama moyo, kansa, mapafu, figo na ini zitatolewa katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini?
Supplementary Question 1
MHE. FADHILI F. NGAJILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichukue nafasi hii pia kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwekeza sana kwenye huduma za kibingwa katika nchi yetu. Sisi Kanda ya Nyanda za Juu Kusini tunanufaika sana na huduma hizi. Sisi Nyanda za Juu Kusini tunategemea sana hospitali ya kanda ile iliyopo pale Mbeya.
MWENYEKITI: Uliza maswali.
MHE. FADHILI F. NGAJILO: Mheshimiwa Mweyekiti, huduma zetu za moyo na kansa bado zina changamoto. Upande wa kansa, tunaomba ule mtambo wa saratani wa kuchoma mionzi uweze kuletwa kwa haraka kwa sababu sasa hivi tunapata huduma tu za chemo kwa maana ya matibabu ya dawa.
Mheshimiwa Mweyekiti, swali la pili. Imekuwa ni gharama sana kwenye huduma hizi za kibingwa. Nini kauli ya Serikali kuhusu utaratibu wa "Medical Exemption", yaani utaratibu wa kupunguza gharama za huduma hizi za kibingwa kwa wananchi wetu hasa wananchi wangu wa Jimbo la Iringa Mjini? (Makofi)
Name
Dr. Florence George Samizi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Fadhili kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuwatetea Wananchi wa Jimbo la Iringa Mjini na wa Kanda ya Kaskazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza, ni kweli kabisa kwamba tunajenga sasa jengo la mionzi katika hospitali yetu ya Mbeya, na jengo hili linatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba mwaka 2025. Jengo hili litagharimu takribani shilingi bilioni 11. Hivyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, lakini na wananchi wote wa Mkoa wa Mbeya kwamba mtambo huo tutakwenda kuufunga kwenye jengo hilo pindi utakapokamilika mwaka huu ili huduma hizi ziweze kuanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu gharama za matibabu kwa kutumia msamaha, kwanza kabisa, hapa nimpongeze Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameendelea kulipa gharama za matibabu kwa wagonjwa ambao hawana uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bajeti ya mwaka 2025/2026 Serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni 34 kuwahudumia wagonjwa wa msamaha. Hivyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, wagonjwa ambao hawana uwezo, wataendelea kuhudumiwa na Serikali kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii waliopo katika hospitali zetu, na wagonjwa hawa watapata huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari ameshaanzisha huduma ya Bima ya Afya kwa Wote, ambapo 14% ya Mfuko huu utakwenda kuwahudumia wagonjwa ambao wana magonjwa sugu ikiwemo magonjwa haya ya moyo, figo pamoja na saratani. Hivyo, niwaombe Watanzania wote, wale wenye uwezo wajiunge kwenye Mfuko wa Bima Afya kwa Wote na wasiyokuwa na uwezo Serikali itawalipia ili kuweza kupata huduma hizi kwa karibu zaidi. (Makofi)
Name
Dr. Advocate Damas Daniel Ndumbaro
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Songea Mjini
Primary Question
MHE. FADHILI F. NGAJILO aliuliza: - Je, lini huduma za kibingwa za magonjwa kama moyo, kansa, mapafu, figo na ini zitatolewa katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini?
Supplementary Question 2
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kuna hospitali maalumu ya rufaa katika Manispaa ya Songea iliyoko katika Kata ya Mwengemshindo. Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa kama MRI na kutoa huduma za kibingwa katika hospitali hiyo?
Name
Dr. Florence George Samizi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza niendelee kumpongeza Mheshimiwa Mbunge Ndumbaro kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuwapigania wananchi wa Songea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali hii ya Rufaa ya Songea inatoa huduma nane za kibingwa, na sote ni mashahidi kwamba Mheshimiwa Rais alipohutubia Bunge, ametuelekeza tuongeze huduma za kibingwa. Hivyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mwongozo wetu wa 20 kwenda 30 hospitali zote za rufaa zitakwenda kutoa huduma za kibingwa 17.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo tunaendelea kujiandaa kwa kuendelea kununua vifaa, kuendelea kuwasomesha watumishi kupitia Samia Scholarship Program, lakini na kujenga miundombinu ili kuweza kutekeleza huduma hizi ambazo Mheshimiwa Mbunge anazihitaji katika jimbo lake. Ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
Name
Tinnar Andrew Chenge
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. FADHILI F. NGAJILO aliuliza: - Je, lini huduma za kibingwa za magonjwa kama moyo, kansa, mapafu, figo na ini zitatolewa katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini?
Supplementary Question 3
MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Kwa kuwa Hospitali ya Mkoa wa Simiyu ni hospitali ya rufaa, na kwa kuwa hospitali hii haina daktari bingwa wa mifupa, je, ni lini Serikali itapeleka daktari bingwa wa mifupa? (Makofi)
Name
Dr. Florence George Samizi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Mama yangu, Mheshimiwa Chenge kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuwapigania wananchi wa Mkoa wa Simiyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Simiyu ni moja ya hospitali inayotoa huduma za kibingwa, na hospitali hii inatoa huduma za kibingwa sita. Ninaomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa ajira za watumishi ili kukabiliana na changamoto za watumishi na hasa watumishi bingwa. Hivyo pindi watakapopatikana na kupata kibali cha ajira, basi hospitali hii ya Simiyu itapelekewa mtaalamu huyu wa mifupa ili wananchi waweze kupata huduma hizi za kibingwa za mifupa karibu na mkoa wao. Ninaomba kuwasilisha.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved