Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Azza Hilal Hamad

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AZZA H. HAMAD K.n.y. MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza:- Je, lini Serikali itatoa fedha, kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi, Ushetu?

Supplementary Question 1

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali. Sasa ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, wananchi wa Jimbo la Ushetu na Halmashauri ya Ushetu wameonesha haja kubwa ya kuwa na Kituo cha Polisi katika Kijiji cha Nyamilangano. Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kutenga fedha, angalau kidogo kidogo, ili kuanzisha ujenzi wa kituo hicho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa, wananchi wa Mji Mdogo wa Tinde wameonesha haja kubwa ya kuwa na Kituo cha Polisi, wametenga eneo na tayari wameandaa matofali 3,000 pale. Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuweka fedha kidogo kidogo, ili Kituo cha Polisi cha Tinde nacho kiweze kujengwa? (Makofi)

Name

Mohammed Mahmoud Ayoub

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chaani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Azza kwa niaba ya Mheshimiwa Cherehani kwa maswali yake mawili madogo ya nyongeza. Ukweli ni msingi na ni muhimu kwa wananchi wa Ushetu kuweza kupata kituo katika eneo hili ambalo amelitaja la Nyamilangano kama ambavyo imeombwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari imeshatoa taarifa ya msingi kwamba imeshapanga utaratibu wa ujenzi wa kituo hicho katika kipindi cha mwaka 2027/2028. Hilo lipo kwa mujibu wa mpango wa Serikali wa miaka mitano wa ujenzi wa vituo 75 vya Wilaya vya Polisi kikiwepo hiki ambacho nimekitaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuhusu umuhimu wa kuanza kutenga fedha kidogo kidogo, ninataka nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwa niaba ya Serikali kuwa tutawaunga mkono wananchi wa Ushetu na sisi hata kama kupitia vyanzo vingine ikiwemo fedha za tuzo na tozo ama kwa fedha za matumizi ya kawaida na sisi tuweze kuweka mkono wetu kuunga mkono jitihada hizo za wananchi. Ninaomba kuwasilisha.

Name

William Kafiti Kafiti

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Primary Question

MHE. AZZA H. HAMAD K.n.y. MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza:- Je, lini Serikali itatoa fedha, kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi, Ushetu?

Supplementary Question 2

MHE. KAFITI W. KAFITI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Ilemela ninapenda kuiuliza Serikali, ni lini itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi chenye hadhi ya wilaya katika Wilaya hiyo?

Name

Mohammed Mahmoud Ayoub

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chaani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Kafiti Kafiti Mbunge wa Ilemela ambaye naye kama ambavyo walivyo Waheshimiwa Wabunge wengine, ameona umuhimu pia wa kuwa na Kituo cha Wilaya katika Jimbo la Ilemela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, kama nilivyotoa majibu ya msingi kwamba tayari tunao mpango ndani ya kipindi cha miaka mitano unaoanza 2026 - 2030 wa kuhakikisha kwamba vituo vyote vya Polisi vya ngazi ya Wilaya ambavyo ni 75 viwe vimejengwa. Hivyo, niwaahidi pia wananchi wa Ilemela kwamba kituo chao cha Polisi nacho kitakuwa katika mpango huo na tutaweza kutenga fedha kwa mujibu wa hali ya bajeti kuhakikisha kuwa tunajenga kituo hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, kwa sasa waridhie na waendelee kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita ya kujenga Kituo cha Polisi ambacho kipo katika eneo la Tunza Road ambacho ni kituo cha Daraja C ili kituo hicho kianze kutoa huduma na baadaye tuweze kujenga kituo cha ngazi ya Wilaya.