Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Lutengano George Mwalwiba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Primary Question

MHE. LUTENGANO G. MWALWIBA aliuliza: - Je, lini Serikali itafanya mapitio ya miradi ya maji Busokelo ili kubaini changamoto kwa baadhi ya miradi kutofanya kazi ipasavyo?

Supplementary Question 1

MHE. LUTENGANO G. MWALWIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Ninaipongeza Serikali kwa majibu yake mazuri, lakini pamoja na majibu hayo, hali ya maji katika Miji ya Lwangwa, Isange na Kandete bado siyo nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi ipatayo kama mitatu; mradi wa Ntaba ambao unahudumia vijiji vinne vya Kambasegela, Mbambo, Kapulampunguti. Miradi hiyo mkandarasi amesimama, haendelei kufanya kazi kwa sababu ya kukosa fedha pamoja na mradi wa Kabembe. Je, ni lini Serikali sasa itapeleka fedha ili kuweza kutimiza azma njema ya Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwapatia wananchi wa Busokelo majisafi na salama?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba wanafanya ukarabati wa miradi mingine ambayo ufanisi wake unaonekana siyo mzuri kutokana na kwamba ni miradi ya muda mrefu zaidi ya miaka 20. Ni lini sasa kazi hiyo itakamilika ikiwepo kubadilisha chanzo cha Kalinga katika Kata ya Isangi? Ahsante.

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri sana anayoifanya kwa ajili ya wananchi wake wa Busokelo. Ninamhakikishia, tutaendelea kushirikiana naye kutatua changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na kwa maelekezo na falsafa ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtua Mama ndoo kichwani, Busokelo mpaka sasa tunao upatikaji wa huduma ya majisafi na salama kwa 90%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua bado tunayo miradi ambayo inaendelea, bado ina changamoto, lakini kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi, Serikali inaendelea kutenga fedha ili kuhakikisha kwamba tunakarabati miundombinu ambayo imechakaa na skimu zote ambazo zilikuwa na changamoto ili kuhakikisha kwamba zinaweza kutoa huduma iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Ntaba ambao Mheshimiwa Mbunge ameutaja, mpaka sasa umefikia 50% ya utekelezaji wake. Mradi huu unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.987. Nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, mradi huu tunaenda kupeleka fedha ili mkandarasi aweze kuukamilisha na wananchi wa Busokelo wapate huduma ya majisafi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na mradi wa Kabembe, mradi huu ambapo kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 tumetenga kiasi cha milioni 184 kwa ajili ya kwenda kuutekeleza. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, Serikali iko makini kuhakikisha kwamba inawatumikia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la chanzo cha Kalinga ndicho chanzo ambacho kinatumika katika Kata ya Isange. Changamoto yake ni kwamba kuna kipindi kinajaa tope na wananchi pale wanashindwa kupata huduma iliyokusudiwa. Kwa muktadha huo, tunatumia fursa hii kuwaelekeza wataalamu wetu waende wakafanya tathmini na kujiridhisha aina ya hatua inayotakiwa kuchukuliwa katika chanzo hiki, ama kama ni kubadilisha chanzo, ama kukikarabati ili kisiwe na changamoto ya kujaa tope. Lengo ni kuhakikisha kwamba chanzo hiki kitoe huduma ambayo imekusudiwa kwa Watanzania. Ninakushukuru sana.