Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Janeth Elias Mahawanga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza: - Je, kuna mpango gani wa kuanzisha au kuimarisha mifuko maalum ya uwezeshaji kwa wanawake?

Supplementary Question 1

MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mkakati gani katika kufuatilia na kutathmini mikopo wanayopewa wanawake ili kuhakikisha kwamba mikopo hii inaleta tija na matokeo chanya kiuchumi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni namna gani Serikali imejipanga kushirikiana na taasisi binafsi na benki ili kuleta tija zaidi na kuongeza wigo mpana kwa wanawake kupata mikopo na kurejesha kwa wakati?

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Janeth Mahawanga. Ni Mheshimiwa ambaye ana-deal sana na makundi ya wanawake, hususan kuhamasisha kukusanya vikoba, na vikundi mbalimbali. Hii inapelekea kuuliza maswali yenye tija sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mkakati katika kufuatilia na kutathmini kama wanawake hawa wanaokopa wanapata matokeo chanya kiuchumi. Tayari sisi kama Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum tunafanya hivyo. Hili linafanywa zaidi na maafisa wetu maendeleo ya jamii ambao wako mpaka ngazi ya kata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kule chini wanaendelea kuwafikia wanawake, kutoa ushauri, na vilevile wanahakikisha kwamba mikopo ile inaelekezwa kwenye malengo. Vilevile kuhakikisha kwamba wanawatia moyo kwamba wanaweza. Kuanzia ngazi ya vijiji kule, kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii ambao wapo kwenye kata, wanafanya kazi hii. Hivyo, mikopo hii hatuitarajii iwe mikopo chechefu au mikopo ile ya kuumiza kama mikopo ambayo mingine inaumiza mitaani, bali inakuwa yenye matokeo chanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili juu ya kushirikiana na taasisi binafsi, pamoja na benki, sisi kama Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, tayari tunahusiana na benki takribani zote nchini. Ukifika pale kwenye Benki ya Azania utakutana na Mwanamke Hodari Program. Hii program, mwanamke anakopeshwa kwa riba rafiki, hivyo anaweza kukopa hata shilingi milioni 200 au shilingi milioni 300, shilingi milioni moja kulingana na collateral aliyonayo, andiko la mradi au maelezo ya mkopaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, CRDB pia wana IMBEJU Program, pia wanasisitiza wanawake kukopa kwa malengo na kulipa kwa wakati. NMB Bank, NBC, Benki ya Kilimo, vilevile tunapenda kuona kwamba wanawake wanashiriki kwenye shughuli za kilimo za kisasa, hivyo kule pia wanapewa mikopo. Wachimbaji wadogo wadogo wanawake, pia wameweza kujiunganisha, wanakopeshwa kwenye benki na wanaweza wakafanya vizuri sana.