Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Yustina Arcadius Rahhi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. YUSTINA A. RAHHI aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Mradi wa Maji wa Tsoray utakaohudumia vijiji 21 katika Halmashuri ya Mji wa Mbulu?
Supplementary Question 1
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Ninachukua nafasi hii kuishukuru sana Serikali kuleta mradi mkubwa na wa kimkakati unaogharimu shilingi bilioni 70.1 katika Tarafa ya Nambis na katika Jimbo la Mbulu Mji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema mradi huu fedha ikipatikana utatekelezwa ndani ya miezi 24. Sasa kwa bahati nzuri chanzo cha maji katika mradi huu ni Mto Tsoray ambao unapitisha maji mwaka mzima. Sasa ni upi mkakati wa Serikali wa kuwasaidia wale ambao angalau wako kwenye chanzo cha maji kuendelea kupata maji safi na salama?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Mheshimiwa Naibu Waziri, je, uko tayari kuambatana na mimi kwenda kutembelea Tarafa ya Nambis kujionea changamoto kubwa ya maji iliyoko hapo na kuwatia moyo wale wananchi kwa kuwa wanausubiri mradi huu kwa hamu kubwa? Ahsante.
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu maswali mawili ya nyongeza, na kwa faida ya Hansard, hili swali uliliuliza kwa niaba ya Mheshimiwa Mbunge wa Mbulu Mjini na kwamba sambamba na hilo pia, ninapenda kujibu maswali ya Serikali kwa mtazamo ule ule ambao niliujibu siku ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kutafuta fedha shilingi bilioni 70 zipatikane kwa pamoja, ninafikiri itakuwa ni suala ambalo ambalo litachukua muda zaidi na tukakubaliana kwamba mradi huu tutaanza kuutekeleza kwa awamu ili angalau tunapoenda kupata zile fedha zingine basi tunakuja kutumia kama kumalizia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukasema kwamba kutokana na ule Mto wa Tsoray, lakini pia tuna uwezo wa kujenga kwanza tanki, treatment plant (mtambo wa kutibu maji) ili wananchi waanze kupitia existing infrastructure kupata huduma ya maji wakati Serikali ikiwa inatafuta fedha za kujenga miundobinu mipya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, ninamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge dada yangu Mheshimiwa Yustina katika ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuwa akiuongelea sana huu mradi, lakini pia na maeneo mengine ya Mkoa mzima wa Manyara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua kwamba anayo kiu kubwa ya kuona akina mama hawaachi shughuli za kiuchumi kwenda kutafuta maji. Ninamtoa hofu, mimi kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, niko tayari kuongozana naye katika maeneo ambayo ameyataja ili tukajionea hali halisi ya huduma ya maji na baada ya hapo, tufanye tathmini na kuchukua hatua kulingana na mahitaji ambayo yatakuwa yamebainika. Ahsante sana.
Name
Prof. Pius Zebhe Yanda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buhigwe
Primary Question
MHE. YUSTINA A. RAHHI aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Mradi wa Maji wa Tsoray utakaohudumia vijiji 21 katika Halmashuri ya Mji wa Mbulu?
Supplementary Question 2
MHE. PIUS Z. YANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kata ya Rusaba hawajawahi kufaidika na huduma ya maji safi na salama. Sasa ninaomba kufahamu ni lini wananchi hao watawezeshwa kupata maji safi na salama katika kata hiyo katika Wilaya ya Buhigwe?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Profesa Pius Yanda, Mbunge wa Jimbo la Buhigwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua kwanza kazi kubwa anayoifanya Mheshimiwa Pius Yanda kwa kuwatetea Wana-Buhigwe na vilevile kuitetea sekta ya maji, yeye akiwa kama mtafiti katika vyanzo vya maji, ameisaidia sana Serikali hii na sasa ndiyo Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maji na Mazingira, anatambua umuhimu mkubwa sana wa kuwa na maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamtoa hofu Mheshimiwa Mbunge, hili tunalichukua kwa uzito kwa kufuata falsafa ile ile ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba wananchi wa kata hiyo ni lazima tukawatue akina mama ndoo kichwani. Ahsante sana.
Name
Abubakar Alli Omari
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manonga
Primary Question
MHE. YUSTINA A. RAHHI aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Mradi wa Maji wa Tsoray utakaohudumia vijiji 21 katika Halmashuri ya Mji wa Mbulu?
Supplementary Question 3
MHE. ABUBAKAR A. OMARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wangu wa maeneo ya Jimbo la Manonga ambao wameshafikiwa na mradi wa maji ya Ziwa Victoria, lakini upatikanaji wake imekuwa ni matatizo makubwa sana. Inapita mpaka wiki mbili, tatu maji haijatoka. Kuna shule ya sekondari iko Ntigu maeneo ya Ntigu, Usongo, wanafunzi imebidi waondoke kwa kukosa maji.
Je, Serikali ina mipango gani wa kuhakikisha maji ambayo yamekuja kwa gharama kubwa sana ya Serikali na yanapatikana kwa wananchi? (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Abubakar Omari tafadhali rudia swali lako na isogelee microphone. Sogelea kipaza sauti Mheshimiwa.
MHE. ABUBAKAR A. OMARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi; wananchi wangu wa Jimbo la Manonga maeneo ambayo Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria yamefika, lakini maji hayatoki mpaka wiki mbili mpaka tatu kiasi kwamba watu sasa hivi ukiwatajia Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria maeneo yale, wanakuwa yaani hawakuelewi. Kwa mfano, sasa hivi kuna wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Seif Gulamali wameanza kuondoka shuleni kwa kukosa maji wiki ya pili mpaka tatu sasa hivi. Shida ni nini hasa?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abubakar; jambo ambalo ameliongea ni jambo ambalo ni zito kidogo na ni la msingi sana. Wananchi ama wanafunzi kutoka shuleni ama kuondoka shuleni kwa sababu ya kukosa huduma ya maji safi na salama, si utaratibu na wala siyo maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Baada ya kikao hiki cha Bunge Mheshimiwa Mbunge tuonane ili tuende kuhakikisha kwamba tunachukua hatua za haraka ili wananchi na wanafunzi wa shule hiyo wanapata huduma ambayo inatarajiwa. Ahsante sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved