Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Primary Question

MHE. FROLENT L. KYOMBO aliuliza: - Je, lini Serikali itatenga bajeti ya kutosha ili kukamilisha ujenzi wa Barabara ya Katoma – Bukwali badala ya kujenga mita 200 kila mwaka?

Supplementary Question 1

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi kwa ajili ya maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninapongeza juhudi za Serikali kwenye Barabara hii ya Katoma – Bukwali ambayo imeendelea kutengenezwa kwa kiwango ambacho inapitika hadi sasa, lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, ninaendelea kuipongeza Wizara ya Ujenzi chini ya Mheshimiwa Ulega ambaye amekuwa ni mhimili katika ujenzi wa barabara na Wilaya ya Missenyi inaendelea kufaidi usimamizi wako, lakini pia kuwepo kwa Meneja wetu wa Mkoa Engineer Joel, ameendelea kusimamia vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hiyo kwa sasa imejengwa kilometa 8.2 kwa miaka 10 ambapo imekuwa ikijengwa meta 200; 200. Sasa ni nini ji jibu lenye matumaini kwa Wananchi wa Missenyi kwamba barabara hiyo kilometa 31 lilizobaki zitakamilika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Mheshimiwa Ulega amekuwa ni mwanajamii wa Missenyi na anajua wazee wangu wa Missenyi akina Sheikh wa Mkoa Alhaj Haruna Abdallah Kichwabuta, Mlangira Justin Lambert Kaiza, Ruimbao, wote umekuwa nao na barabara umeenda mpaka Bugandika pale. Sasa wazee wangu pale Bugandika – Kitobo – Buyango mpaka Ruzinga barabara yao kilometa 18 tu wanasema kijana wetu tupeleke kwa Mheshimiwa Waziri wetu.

Je, ni lini na sasa barabara hiyo ya Mshenye – Bugandika – Kitobo – Uyango mpaka Ruzinga itajengwa kwa kiwango cha lami ili na wazee hao angalau wasipite kwenye barabara ambayo ina mashimo mengi? Ahsante sana.

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge wa Missenyi Comrade Kyombo na ninampongeza kwa umahiri wake na ufuatiliaji wa karibu sana wa hoja za wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi hili la kuchukua muda mrefu wa Barabara ya Katoma – Bukwali, ninakiri kwamba tunakwenda kukamilisha upembuzi yakinifu wa sehemu iliyobaki. Sehemu ambayo tunakwenda ukamilifu wake kufika mwezi Septemba mwaka huu, mkandarasi anayefanya kazi ya upembuzi yakinifu atakuwa amekamilisha, na baada ya kupata uhakika wa gharama, sasa tutakwenda kuitangaza barabara hii yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyofahamu mradi huu ni miongoni mwa miradi inayoendelea, na ni msisitizo wa Serikali katika commitment ya Serikali ni kwamba tutahakikisha miradi yote inayoendelea na miradi yote iliyosainiwa, ndiyo kipaumbele chetu. Sasa mradi huu wa Bukwali kutokea Katoma ni miongoni mwa miradi hiyo na kwa msingi huo, wewe na Wana-Missenyi wote waendelee kuwa na subira, tutafanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana hivi sasa tumeendelea kufanya ubunifu kwa vyanzo vya mapato ya kuhakikisha kwamba miradi yetu hii yote ambayo inaendelea na iliyosainiwa iwe na vyanzo vya uhakika ili wakandarasi waweze kurudi site na waendeleze kazi ya kujenga miundobinu ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na katika hizo, tunavyo vyanzo vya PPP, tunacho chanzo cha uhakika cha Mfuko wa Barabara ambacho kitakwenda kufanya vizuri na ninawahakikishia Wabunge wote kwa kuwa mmetoa maoni na nina hakika Serikali imeyapokea, na vyanzo vya kutoka katika Mfuko Mkuu wa Hazina na hiyo itapelekea kuijenga barabara ile. Miji ya Kanyigo na mingine, yote itapata siyo tu kujengewa lami, lakini na kuwekewa taa za barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lake la pili Mheshimiwa Kyombo ni Barabara za Missenyi na amewataja baadhi ya wazee wetu wa kule Kagera akiwemo Sheikh Kichwabuta na Kaka yangu Lambert ambao barabara zao na mimi ni kweli nimepita huko mara kadhaa nikienda katika shughuli za kijamii ikiwa ni pamoja na kushiriki misiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachukua hoja hii na kwenda kuifanyia kazi, ninamwagiza Meneja wa Mkoa wa Kagera ahakikishe ya kwamba anakwenda kuziweka katika kipaumbele barabara hizi ili tuweze kuzifanyia kazi na hatimaye tuweze kutoa huduma iliyo nzuri kwa wananchi wa maeneo haya. Hongera sana Mheshimiwa Kyombo kwa ufuatiliaji mzuri wa shughuli na maendeleo ya Wananchi wa Missenyi, lakini na Mkoa mzima wa Kagera. Ahsante.

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FROLENT L. KYOMBO aliuliza: - Je, lini Serikali itatenga bajeti ya kutosha ili kukamilisha ujenzi wa Barabara ya Katoma – Bukwali badala ya kujenga mita 200 kila mwaka?

Supplementary Question 2

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Barabara ya Makofia – Mlandizi – Mzenga ina hali mbaya kutokana na mvua hizi zilizonyesha.

Je, Serikali ina mpango gani wa matengenezo ya dharura ili kuwaondolea shida Wananchi wa Bagamoyo ambao kwa sasa usafiri kuanzia jioni haupatikani na hata pikipiki bei imepanda mpaka shilingi 10,000 wakati wanasubiria ahadi ya Serikali ya ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara hii? (Makofi)

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Bagamoyo, Dada yangu Subira Mgalu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Barabara ya Makofia inayopita katika Miji ya Yombo, Viswe mpaka unafika Mlandizi na baadaye kutoka Mlandizi kwenda Mzenga, ni barabara ya kimkakati na ni barabara muhimu sana kwenye kuhakikisha pia inakuwa ni mbadala wa Barabara Kuu ya Morogoro kwa maana ya Kibaha - Chalinze mpaka Morogoro, na kwa hiyo, barabara hii inapokuwa katika hali nzuri, inarahisisha watumiaji hata wanaokwenda katika mikoa mingine wanaotokea Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwagiza Meneja wetu wa Mkoa wa Pwani kuhakikisha kwamba tunakwenda kuifanyia ukarabati, mvua zimekwishakupungua na kuisha kabisa katika maeneo yetu. Kwa hiyo, sasa atoe nafasi kwa mkandarasi kwenda kuisafisha barabara hii ambayo ni ya kimkakati kwenye kupunguza msongamano wa barabara kubwa ya Chalinze mpaka Kibaha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Subira Mgalu kwa msisitizo wake na ufuatiliaji wake wa barabara hii hadi kufikia tumeiweka katika mpango wa bajeti ya mwaka 2026/2027 kama barabara ya upunguzaji wa msongamano wa barabara kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutahakikisha kwamba tutaitangaza barabara hii, kupata mkandarasi na hatimaye ili tutakapokuwa tunajenga barabara kuu ya expressway ya kutoka Kibaha – Chalinze – Morogoro ambayo ni mkakati wa Serikali kuifanya kwa njia ya PPP, na hivi ninavyozungumza tayari NSSF na Kampuni ya CRJE wapo kwenye mazungumzo ya mwisho ya kuingia katika kutekeleza mradi huu, basi barabara hii ya Makofia – Mlandizi itakwenda kuwa ni mbadala mzuri wa msongamano wa barabara kubwa ikiwa ni pamoja na barabara ya kutoka TAMCO – Mapinga na na kutokea kule Kerege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)

Name

Zacharia Paulo Issaay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Primary Question

MHE. FROLENT L. KYOMBO aliuliza: - Je, lini Serikali itatenga bajeti ya kutosha ili kukamilisha ujenzi wa Barabara ya Katoma – Bukwali badala ya kujenga mita 200 kila mwaka?

Supplementary Question 3

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Barabara ya Mbulu – Garbabi ni barabara aliyopewa mkandarasi wa Kichina kwa miaka minne sasa. Sehemu ya barabara hiyo kutoka Mbulu Mjini kwenda Tlawi ama kwenda pale Tlawi haijatengenezwa kwa miaka minne sasa, mkandarasi huyu wa Kichina anayejenga lami kwa muda mrefu ameshindwa kutengeneza hicho kipande. Mheshimiwa Waziri, nini kauli ya Serikali kumsimamia huyu mkandarasi ili atengeneze hiyo barabara kuondoa adha kubwa sana kwa wananchi wa eneo hilo?

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Issaay, Mbunge wa Mbulu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli katika hii barabara tuna mkandarasi huyu aliyekwisha kumtaja na tayari sehemu ya barabara hii wiki mbili zilizopita tumeilipa. Tumelipia fedha ya kuhakikisha kwamba mkandarasi anarudi site. Ninafahamu ya kwamba hajarudi site bado na moja ya sababu ilikuwa ni hali ya hewa, lakini ninamwagiza sasa mkandarasi na ninamwagiza Meneja wa TANROADS wa Mkoa na TANROADS Makao Makuu kuhakikisha kwamba wanamrudisha mkandarasi, anaanza ujenzi mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ile sehemu iliyobaki ya kilometa zile 25 ambazo zilikabidhiwa kwa mkandarasi, lakini hazijafanyiwa kazi kwa sababu ya kukosekana kwa fedha ya awali ya malipo kwa mkandarasi yule. Ninamwagiza pia Meneja wa TANROADS kwa kuwa barabara hiyo ina mkandarasi wake, lakini hajaanza kazi, bado wajibu huo ni wa kwetu wa kuhakikisha kwamba tunaiboresha ili iweze kupitika wananchi wapate unafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakati huu yule anapoanza na wao TANROADS mara moja waanze kwa kuisafisha barabara ile ili watu wa Mbulu waweze kupitisha mazao yao ikiwa ni pamoja na mazao ya kilimo kama vile vitunguu na kadhalika kwa urahisi vinavyokwenda sokoni katika Miji ya Arusha, Miji wa Babati na nchini kote kwa ujumla wake. (Makofi)