Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Silvery Luboja Salvatory

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Misungwi

Primary Question

MHE. SILVERY L. SALVATORY aliuliza: Je, lini upanuzi wa barabara kuu kwa njia nne kutoka Kenyatta – Usagara Mwanza utaanza?

Supplementary Question 1

MHE. SILVERY L. SALVATORY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza na ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa kuna kila dalili ya kwamba mkandarasi amekwishapatikana na wakati wowote ataanza kazi. Je, Serikali iko tayari kuanza upanuzi wa barabara hii kutokea Usagara kuelekea Mjini ukizingatia ukweli kwamba eneo la Usagara halihitaji uhamishaji wa miundombinu kama vile mabomba na taa za barabarani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa upanuzi wa barabara hii unaenda kufungua shughuli za kiuchumi. Je, Serikali iko tayari kuanza mchakato wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami; Barabara ya Fulo – Nyambiti hadi Malya yenye urefu wa kilometa 73 kwani barabara hii inauhusiano mkubwa na dry port pamoja na SGR itakayokuwa kule Fela na itapita kwenye kata yangu ya Fela – Kolomije pamoja Kanyelele?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. (Makofi)

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Misungwi, Mheshimiwa Silvery Luboja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana na nimpongeze sana kwa umahiri wake kwenye kufuatilia hoja za wananchi wa pale Misungwi ambazo ukizitazama zinabeba vilevile eneo lote la Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Usagara kwenda Mwanza Mjini ama Mwanza Mjini kuja Usagara kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi la awali, ni kwamba ni barabara ya kimkakati na ni barabara muhimu sana na kwa kweli kwa sasa ni barabara ambayo ina msongamano mkubwa hasa mara baada ya ukamilifu wa Daraja la Kigongo – Busisi kama lilivyotamkwa maarufu Daraja la John Pombe Magufuli. Msongamano umeongezeka sana kwa sababu ni daraja limeleta msisimko mkubwa wa shughuli za kiuchumi katika Mkoa wa Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, tunatarajia pale Mwanza tutakuwa na kituo kikubwa cha SGR, kwa hiyo kitaongeza zaidi ule msongamano wa eneo lile, rai ya Mheshimiwa Mbunge ni kwamba tusianzie Mwanza Mjini, tuanzie Usagara kuelekea Mwanza Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niseme tu kwamba ushauri huu na rai hii ya Mheshimiwa Silvery Luboja, Mbunge wa Misungwi nimeipokea na nitaifikisha katika jopo la watalaamu, tutaitathmini na kuona kwamba ni namna gani tunaweza kutekeleza either kuanzia Usagara kwenda Mwanza Mjini au kuanzia Mwanza Mjini kurudi Usagara, lakini kwa hakika ushauri wake nimeupokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili; anasema kwamba kutokana na maendeleo haya mazuri yanayoendelea katika eneo hili yanapelekea umuhimu wa kuifungua Barabara ya kutoka Fulo mpaka Nyambiti mpaka Malya na ni kweli barabara hii ni muhimu ambayo itapeleka muunganiko mpaka Sengerema kwa Mheshimiwa Tabasam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie kwamba na yenyewe tunaikamilishia upembuzi yakinifu na mara baada ya kuwa tumekamilisha upembuzi yakinifu wake tutapata gharama halisi na katika lengo lile la kuondosha msongamano katika miji haswa Jiji la Mwanza, barabara hii na yenyewe ni muhimu kwa hivyo tutaipa umuhimu kwanza tukishapata hizo gharama, tukishajua hizo gharama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaingia katika mkakati wa kutafuta fedha na baadaye kutangazwa zabuni kumpata mkandarasi na hatimaye hatua kwa hatua kuanza kuitekeleza kwa kuijenga. Nikupongeze sana tena kwa mara nyingine Mheshimiwa Silvery Luboja kwa maswali haya mazuri ya wananchi wa pale Misungwi na Jiji la Mwanza kwa ujumla wake, ahsante. (Makofi)

Name

Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Primary Question

MHE. SILVERY L. SALVATORY aliuliza: Je, lini upanuzi wa barabara kuu kwa njia nne kutoka Kenyatta – Usagara Mwanza utaanza?

Supplementary Question 2

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishukuru Serikali kwa kutupatia pesa kwa ajili ya kufanya ukarabati mdogo katika barabara inayotoka Mchinga – Kilolambwani – Mvuleni hadi Kijiweni na kiasi hicho cha pesa walichotupatia ni takribani ya shilingi milioni 100, sasa hizi shilingi milioni 100 haziwezi kutosheleza na tuliomba pesa takribani kama shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuitengeneza hii barabara ambayo ilikuwa imeharibika sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kujua lini Serikali itatupatia hizo pesa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa hiyo barabara ambayo inahusisha kata tatu, ahsante sana? (Makofi)

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Mchinga, Mheshimiwa Mama Salma Kikwete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimepokea shukrani hizi alizozitoa za wananchi wa Mchinga kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Jemedari Dkt. Samia Suluhu Hassan; na mbili ombi lake la kupata hizi fedha lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nilipokee jambo hili na niwahimize watalaam wetu ya kwamba fedha yoyote itakayokuwa imepatikana kuelekea katika Mkoa wa Lindi, tutaipa kipaumbele barabara hii kwa maana kwamba kwenda kutimiza ombi hili la wananchi wa Mchinga. Nisisitize na huu ndiyo msimamo wetu kwamba fedha ndogo tunayoipata ama fedha kidogo tunayoipata watalaam wote wa barabara ikiwa ni pamoja na TANROADS na hata wale wa TARURA ni muhimu sana kuhakikisha kwamba fedha hiyo kidogo itumike kikamilifu katika maeneo yale korofi yanayoweza kuwa ni chanzo kikubwa cha wananchi kutoweza kupata access ya kwenda sokoni, hospitali na katika huduma zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, fedha ile kidogo inayopatikana itumike vizuri kuondoa vikwazo kwa maana bottleneck ili wananchi/wakulima wa ufuta, wakulima wa korosho na mbaazi na mazao mengine wakiwa ni pamoja na wananchi wa pale Mchinga wawe na uwezo wa kutumia barabara wakati wowote bila ya kusahau kuzingatia viwango vya ubora vya ujenzi wa barabara zetu kwa kuwa zinajengwa kwa fedha za walipa kodi wa Taifa hili, mnatakiwa kuhakikisha kwamba ni lazima ziwe ni barabara zenye viwango vya ubora, ahsante sana. (Makofi)

Name

Neema Gerald Mwandabila

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SILVERY L. SALVATORY aliuliza: Je, lini upanuzi wa barabara kuu kwa njia nne kutoka Kenyatta – Usagara Mwanza utaanza?

Supplementary Question 3

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, sisi tuna barabara inayoanzia Igawa mpaka Tunduma. Barabara hii ni barabara inayoenda kutuunganisha nchi ya Zambia, magari yana…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Neema Mwandabila tafadhali ongeza sauti na ikaribie microphone ili tuweze kukusikia.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahaa, okay.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii magari ni mengi kiasi kwamba yanatuelemea na haina barabara ya mchepuko…
MWENYEKITI: Mheshimiwa barabara ipi? Anza swali lako.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna barabara inaitwa Igawa – Tunduma; barabara hii ni barabara ya msingi ambayo inaenda kuunganisha na Zambia. Barabara hii haina barabara ya mchepuko njiani, magari ni mengi, ajali ni nyingi na changamoto ni nyingi. Serikali kweli imeweka dhamira ya kujenga barabara nne, lakini hatuoni ule u-serious wa Serikali kuanza ujenzi wa barabara hiyo hususan kutoka Mloo kuelekea Tunduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni upi mkakati wa Serikali kuanza ujenzi haraka katika Mji wa Tunduma ili kutunusuru na ile foleni? Ahsante. (Makofi)

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Mwandabila, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimwondoe hofu najua hii ni barabara ya kiuchumi ni barabara kuu inabeba uchumi wetu. Mafanikio ya Bandari ya Dar es Salaam huwezi kuyataja bila ya kuitaja Barabara ya Igawa – Tunduma kwa sababu zaidi ya nusu ya mzigo unaotoka Bandari ya Dar es Salaam unapita barabara hii kwa lengo la kupeleka mizigo upande wa Zambia na upande wa Kongo pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan iko very serious, naomba nimhakikishie Mbunge na Wabunge wote iko very seriously na ushahidi wa seriousness hiyo pale ambapo yeye atakuwa shahidi na Wabunge wa Mkoa wa Songwe watakuwa mashahidi pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alifanya ziara na alitoa maagizo ya kuhakikisha ya kwamba tunatanua barabara eneo lile la Tunduma kwa sababu ni eneo ambalo limekuwa likikabiliwa na msongamano mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe taarifa ya kwamba moja; Wizara ya Ujenzi tulipokea maelekezo yale ya Mheshimiwa Waziri Mkuu; mbili, tuliweka mkandarasi pale, mkandarasi wa hapa nyumbani Kampuni ya Narumo iko pale; tatu, mkandarasi alikwishakuanza kufanya kazi ya upanuzi wa barabara ile mwanzo ilikuwa ni meta 700 lakini mara baada ya kufanya usanifu tumefanya zaidi ya meta 700.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa ni zaidi ya kilometa moja ni barabara nne, mbili zinaingia na mbili zinatoka na hivi sasa katika lile eneo utaona kuwa kuna pametanuka sana; na nne, katika jambo hilo ni kwamba mradi umeishafika zaidi ya 40% mara baada ya kupata fedha taslimu za mradi ule zote shilingi bilioni sita na milioni mia nne zimepelekwa pale Tanduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwalike Mheshimiwa Neema Mwandabila na Wabunge wa Mkoa wa Songwe wafanye ziara ya kwenda kukagua waone kazi kubwa na nzuri ambayo inafanywa pale Tunduma itakayoondoa ule msongamano uliokuwa siyo wa lazima katika eneo lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango mkubwa tayari feasibility study ya mwanzo imeshawasilishwa na hivi sasa tumepokea feasibility study ya pili ya Kampuni ambayo tunakwenda kufanyanalo PPP, Kampuni la CCECC ambalo imeonesha interests ya kuijenga barabara ile katika mfumo wa PPP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo sasa mara baada ya kukamilisha kazi hiyo ya hatua hizi mbili za feasibility study (upembuzi yakinifu) tutakuwa tunatarajia kwenda katika hatua inayofuata ili kusudi tuweze kufanya mradi ule wa kielelezo wa uchumi wa Taifa letu katika Mfumo wa PPP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe hofu Mheshimiwa Mwandabila na Wabunge wote na niendelee kumkaribisha kwenda kuona kazi kubwa na nzuri inayofanywa pale Tunduma ya marekebisho ya lile eneo na kwa hiyo, malori yaliyokuwa yaki-park njiani kwa sababu ya foleni, sasa yatapata unafuu mkubwa sana wa kuweza kupita katika eneo lile, naomba kuwasilisha. (Makofi)

Name

Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SILVERY L. SALVATORY aliuliza: Je, lini upanuzi wa barabara kuu kwa njia nne kutoka Kenyatta – Usagara Mwanza utaanza?

Supplementary Question 4

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini ujenzi wa barabara ya mzunguko (ring road) katika Jimbo la Tabora Mjini utaanza?

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya mzunguko ya Tabora (Tabora Bypass) imetamkwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi. Nimpongeze Mheshimiwa Hawa Mwandabila kwa ufuatiliaji wake na tayari...

Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani ni Mheshimiwa Hawa Mwaifunga, Mbunge wa Jimbo la Tabora kwa ufuatiliaji wake wa karibu sana wa Bypass hii ya Tabora na siyo bypass ya Tabora peke yake. Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Ilani ya Uchaguzi imezingatia Miji yetu yote ukienda Babati utakuta kwamba barabara kuu inapita katikati ya mji, ukienda Morogoro pamoja na kwamba ile ilikuwa ni bypass lakini sasa inaonekana kuwa inapita katikati ya mji na miji mingine ikiwa ni Singida na kadhalika, yote malori yanakatisha katikati ya mji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ujenzi kufuatia maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi tumelizingatia jambo hili kwamba ni lazima tuondoshe misongamano katikati ya mji kwa kutengeneza bypass. Hivyo hii ni moja ya kazi tutakayoifanya kwa kufanya upembuzi yakinifu na wa kina tupate gharama za kufanya hivyo pale Tabora Manispaa na baadaye kutafuta fedha na hatimaye kuitengeneza ile bypass ya Tabora ili kusudi tuuache mji uwe ni mji wa kibiashara na huduma na malori yaweze kupita pembezoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Hawa Mwaifunga, Mbunge wa Tabora kwamba jambo hili tumelipokea, tunalifanyia kazi na tumpongeze sana kwa ufuatiliaji wake kwa maslahi mapana ya wananchi wa Tabora na nchi yetu kwa ujumla wake, ahsante sana. (Makofi)