Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JULIANA D. SHONZA aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kufuatilia maendeleo ya Wanafunzi wanaofanya vizuri kitaifa ili kuhakikisha wanakuwa rasilimali muhimu kwa maendeleo ya Taifa?

Supplementary Question 1

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua jitihada kubwa ambazo zimefanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, hasa kupitia Samia Scholarship. Swali langu, nataka kujua kuhusu wale ma-TO, kwa maana ya wale wanafunzi ambao wanaibuka kuwa vinara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni baada ya mimi kuguswa sana na taarifa ya TO wa Mwaka 2006, Elias Kihombo, ambaye kwa bahati mbaya kwa sasa hivi ni Marehemu. Elias Kihombo alifanya kazi kubwa sana ya kuzunguka kwenye shule nyingi kufundisha na vilevile kufundisha tuition nyingi, lakini inaonekana alivyofika chuo, hakufanya vizuri, hali iliyosababisha ku-disco.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, unaweza kuona kwamba, mtu ambaye ni TO, lakini akifika chuo ana-disco. Kwa hiyo, nataka nijue tu kwamba, ukiachana na hii Samia Scholarship toka mwaka 2000 mpaka sasa hivi, je, Serikali wana kanzidata ya TO’s wangapi? Vilevile, je, wanajua kwamba, wako wapi na wanafanya nini? Ahsante sana. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tunao wanafunzi wa kidato cha sita na vyuo vikuu ambao wanafanya vizuri zaidi kila mwaka. Serikali hii kwa kutambua umuhimu wao na kuwatumia katika ujenzi wa Taifa letu, imekuwa ikiwatambua, kwanza kwa kutoa zawadi mbalimbali na certificates.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwa kuhakikisha kwamba wanatambuliwa na kupewa ufadhili maalum katika vyuo vikuu kote nchini, na pia katika vyuo vikuu bora kabisa duniani, ili wapate utaalam mbalimbali ambao unakuja kusaidia ujenzi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika kipindi cha mwaka 2017 mpaka mwaka huu wa fedha 2025/2026 jumla ya wanafunzi waliofanya vizuri sana Kitaifa 1,113 wamepelekwa kwenye vyuo bora nje ya nchi na wanaendelea na masomo mbalimbali kwa lengo la kupata utaalam adhimu na kuja kutumia utaalam huo katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwanza Serikali inatambua na inawafuatilia wanafunzi wote wanaofanya vizuri ili kuhakikisha wanapata fursa nzuri ya kujiendeleza na kujenga uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, Mheshimiwa Mbunge anahitaji kuona kanzidata ya mwaka 2020 mpaka sasa, ninaomba hili nilichukue na nitafute, kwa sababu, ni suala la takwimu. Nitampa Mheshimiwa Mbunge, ili kuweza kutambua ni wangapi? Wako wapi? Wanafanya shughuli gani? Ahsante. (Makofi)

Name

Najma Murtaza Giga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JULIANA D. SHONZA aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kufuatilia maendeleo ya Wanafunzi wanaofanya vizuri kitaifa ili kuhakikisha wanakuwa rasilimali muhimu kwa maendeleo ya Taifa?

Supplementary Question 2

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu ya juu ni suala la Muungano. Je, Serikali ina mpango gani kwa wanafunzi ambao wanafanya vizuri sana kwa upande wa Zanzibar? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, suala la elimu ni la Muungano na ndiyo maana fursa hizi za wanafunzi wanaofanya vizuri zaidi, wanaopelekwa kwenye vyuo vikuu bora kabisa duniani, wanatoka pande zote mbili za Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kupitia Samia Scholarship, ambayo imeleta ukombozi mkubwa sana kwa wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo yao, imeendelea kuchukua wanafunzi kutoka pande zote za Muungano. Tutaendelea kuhakikisha kwamba, tunatoa fursa hizo ili wanafunzi wa pande zote waweze kunufaika na kujenga Taifa letu kwa ufanisi mkubwa zaidi.