Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Masache Njelu Kasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Primary Question

MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: - Je, lini ujenzi wa barabara kutoka Makongolosi hadi Rungwa kwa kiwango cha lami utaanza?

Supplementary Question 1

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa majibu ya Serikali ambapo kila mwaka wakati swali hili linapoulizwa, majibu ni haya haya. Kipande cha barabara ambacho kinazungumzwa sasa hivi ambacho kimeshajengwa kuanzia Mbeya – Chunya – Makongolosi kilishakamilika takribani miaka 10 imeshapita, kwa sasa hivi barabara hiyo imeshaanza kuharibika hasa kipande cha Mbeya – Lwanjilo kina mashimo mengi na kimeanza kuwekewa viraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, swali la msingi, ni lini Serikali itaanza kujenga kipande cha barabara kuanzia Makongolosi – Rungwa, barabara hii inayounganisha Mkoa wa Mbeya, Singida pamoja na Tabora? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, barabara ya kuanzia Igawa inayopita Mbeya Mjini – Tunduma, imechakaa, imekwisha na ni barabara mbaya sana. Tutambue barabara hii ndiyo barabara moja Tanzania kwa maana T1 inayopitisha mizigo takribani asilimia 40 inayotoka Bandari ya Dar es Salaam. Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa barabara hii na kutoa fedha ili barabara hii iweze kujengwa kwa kiwango cha lami?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba barabara tunayoisema ya Mbeya – Makongolosi – Rungwa – Itigi na Rungwa – Ipole hadi Tabora ni moja ya barabara ndefu katika nchi yetu ambazo ni trunk. Kama nilivyosema katika jibu langu la msingi la Serikali, ni kwamba tumeanza kuijenga kwa awamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbeya tumeshajenga hizo kilometa 112, lakini barabara hiyo inakwenda Singida, ambapo tunavyoongea sasa hivi wako wakandarasi wameanza Singida kutoka Mkiwa Manyoni wakija Naronga ambapo mwelekeo ni kwenda Rungwa kuja Makongolosi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mbunge kwamba Serikali tunatafuta chanzo ambacho kitakuwa cha uhakika ili kuweza kuunganisha mikoa hiyo mitatu ya Tabora, Singida na Mbeya. Kwa sasa kabla hatujapata chanzo cha uhakika kujenga barabara yote, ndiyo maana tunakwenda kwa awamu, tukiwa na uhakika kwamba tunatafuta chanzo cha uhakika ambacho tutaijenga hiyo barabara yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, ni kweli kwamba barabara kubwa katika nchi yetu ni T1 TanZam, Dar es Salaam – Morogoro – Iringa – Mbeya – Tunduma. Barabara hii iko kwenye mipango hasa kipande cha Igawa – Mbeya – Tunduma ni barabara ambayo tumeamua kuijenga kwa ubia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyoongea sasa hivi, Serikali ipo kwenye majadiliano ya mwisho na watu ambao wameonesha utayari wa kusaidiana na Serikali kujenga hiyo barabara ya Igawa – Mbeya – Tunduma njia nne kwa utaratibu wa ubia. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mbunge, Serikali inalifanyia kazi na tuna hakika tutafika pazuri ili barabara hiyo iweze kujengwa, ahsante.

Name

Hawa Mchafu Chakoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: - Je, lini ujenzi wa barabara kutoka Makongolosi hadi Rungwa kwa kiwango cha lami utaanza?

Supplementary Question 2

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili kuweza kuuliza swali dogo la nyongeza. Barabara ya Bungu – Nyamisati ni barabara ya muda mrefu, ina historia na inaunganisha Majimbo matatu; Jimbo la Mafia, Jimbo la Kibiti na Jimbo la Mkuranga. Ni lini barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante.

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii tumeshakamilisha usanifu wa kina, Bungu – Nyamisati na ninakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na kuunganisha, lakini barabara hii ndiyo inayopeleka watu wa Kisiwa cha Mafia. Kwa hiyo, Serikali tumeshafanyia usanifu na tusubiri bajeti tuone tutakuwa tumeipangia nini kwa maana ya kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.

Name

Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: - Je, lini ujenzi wa barabara kutoka Makongolosi hadi Rungwa kwa kiwango cha lami utaanza?

Supplementary Question 3

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Barabara ya Tabora – Mambali – Shinyanga, barabara hii ujenzi wake umekuwa ukisuasua na hususan kwenye kipande cha kutoka Tabora Mjini kuelekea Bukene. Umuhimu wa barabara hii kwa wananchi wangu wa Kata ya Misha, Kalunde pamoja na Kata ya Kabila ni mkubwa sana. Ni lini Serikali italeta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii ili iweze kunufaisha wananchi wa maeneo wa hayo?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba hii barabara ya Tabora – Mambali – Bukene Nzega ni kweli tumeanza kufanya kwa kiwango kidogo japo tulianza upande wa Bukene, lakini ni barabara ambayo hata ukienda kwenye vitabu vyetu vya bajeti, tumeitambua na tukaipangia kuwa kwenye mpango wa kuijenga. Sasa kitakachojitokeza ni bajeti, ikiruhusu, basi tutaanza kwa sababu tayari ipo kwenye mipango yetu ya kuijenga kwa kiwango cha lami, ahsante.

Name

Amosy William Maganga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Primary Question

MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: - Je, lini ujenzi wa barabara kutoka Makongolosi hadi Rungwa kwa kiwango cha lami utaanza?

Supplementary Question 4

MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi hii. Barabara ya kutoka Ipole – Rungwa imekuwa kwenye ahadi ya Serikali ya kujengwa kwa kiwango cha lami kwa zaidi ya miaka 30 sasa. Hebu Serikali sasa iwaambie wananchi hao wa Kata za Ngoywa, Kitunda, Kiloli, Kirumbi pamoja na Kipili kwamba sasa kwa mwaka wa fedha ujao 2026/2027, Serikali sasa inaenda kutekeleza ahadi hiyo. (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge ni sehemu ya barabara ambayo ipo kwenye swali la msingi ambayo ni Mbeya – Makongolosi – Rungwa – Kitunda – Ipole na hiki kipande alichokitaja nadhani nimekielezea kwamba tunatafuta fedha kuunganisha Mkoa wa Tabora kuja Rungwa, Singida kuja Rungwa na kwenda Makongolosi kilometa hizo 172 Ipole – Rungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama nilivyosema wakati najibu swali la mwuliza swali la msingi, ni kwamba Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa kweli kuijenga hiyo barabara. Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba hata katika bajeti itakayokuja, tutakuja na mapendekezo ya kuomba ianze kujengwa kwa kiwango cha lami, kipande hicho cha Ipole – Rungwa na kwenda Makongolosi, ahsante.

Name

Regina Henry Mikenze

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: - Je, lini ujenzi wa barabara kutoka Makongolosi hadi Rungwa kwa kiwango cha lami utaanza?

Supplementary Question 5

MHE. REGINA H. MIKENZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami niulize swali la nyongeza. Wilaya ya Nyang’hwale ndiyo Wilaya pekee katika Mkoa wa Geita ambayo haina barabara yoyote ya kiwango cha lami inayounganisha Wilaya hiyo na Wilaya nyingine ikiwemo Makao Makuu ya Mkoa wa Geita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni lini Serikali itatujengea barabara kwa kiwango cha lami katika Wilaya hiyo? (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Mbunge na ninatambua kwamba hili swali tumelijibu mara kadhaa kuhusu barabara ya lami aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge. Barabara hii ipo kwenye utaratibu kwa sasa wa kuisanifu kuanzia Busisi – Ngoma - Nyang’hwale hadi Nyambura na pia kutoka Nyang’hwale kwenda Geita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilisha usanifu, gharama zitajulikana, na sasa ndiyo tutakuja na mpango wa kuijenga kwa kiwango cha lami, ahsante.