Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
| Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
|---|---|---|---|---|---|---|
| 2025-2030 | Session 3 | Sitting 39 | Energy and Minerals | Wizara ya Madini | 463 | 2026-05-29 |
Name
Zuberi Yahya Mfaume
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Morogoro Kusini
Primary Question
MHE. ZUBERI Y. MFAUME aliuliza: -
Je, lini uchimbaji wa madini katika maeneo ya Sesenga na Duthumi utaanza baada ya leseni za uchimbaji kutolewa?
Name
Anthony Peter Mavunde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Dodoma mjini
Answer
WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na kwa niaba ya Waziri wa Madini, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Yahya Mfaume, Mbunge wa Morogoro Kusini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kusimamia kwa karibu maendeleo ya miradi ya madini nchini ili kuhakikisha leseni zinazotolewa zinatafsiriwa kwa uwekezaji halisi na ajira kwa wananchi, mapato kwa Serikali na maendeleo ya maeneo husika. Katika muktadha huo, maeneo ya Sesenga na Duthumi nayo yanaendelea kufuatiliwa kwa karibu ili yaanze kunufaisha wananchi wa Morogoro na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Sesenga lina leseni moja ya utafiti wa madini adimu (Rare Earth Elements) Namba. PL 13451/2025, iliyotolewa tarehe 22 Julai, 2025 kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO). Hadi sasa shughuli za utafiti bado hazijaanza rasmi kwa kuwa STAMICO ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha majadiliano na mwekezaji kuhusu makubaliano ya pamoja ya kuendeleza mradi huo. Mara baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, shughuli za utafiti zitaanza. Serikali imeelekeza hatua hizi zikamilike mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Duthumi lina leseni ya uchimbaji wa kati ya madini ya Kinywe (Graphite) Namba. ML 644/2021, iliyotolewa tarehe 8 Februari, 2021 kwa Kampuni ya Yudi Mining (Tanzania) Graphite Development Company Limited. Kwa sasa kampuni ipo katika hatua za ujenzi wa mgodi na maandalizi ya uzalishaji ambapo usimikaji wa mitambo ya uchenjuaji umefikia takribani 50%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni hiyo imefanikiwa kukamilisha taratibu za mkopo wa nje baada ya idhini kutolewa na Serikali, na fedha hizo zinatarajiwa kupatikana mapema mwezi Juni, 2026. Fedha hizo zitakapopatikana, kazi ya ukamilishaji wa ujenzi wa mgodi na mitambo itaendelea mara moja na uzalishaji unatarajiwa kuanza baada ya hatua hizo kukamilika.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved