Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Zuberi Yahya Mfaume

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini

Primary Question

MHE. ZUBERI Y. MFAUME aliuliza: - Je, lini uchimbaji wa madini katika maeneo ya Sesenga na Duthumi utaanza baada ya leseni za uchimbaji kutolewa?

Supplementary Question 1

MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa upande wa Mgodi wa Duthumi, wananchi wamekuwa na wasiwasi mkubwa kutokana na shughuli zinazoendelea pale hasa kipindi cha usiku, shughuli za uchimbaji zinaonekana zikiendelea, lakini pia malori yakiingia na kutoka. Wasiwasi wao ni kwamba uchimbaji umeanza na madini yanatoroshwa na tabia yao ya kutotaka wananchi wanaozunguka mgodi ule kupata kazi hata zile ambazo hazihitaji ujuzi maalum.

Je, Serikali sasa ipo tayari kwenda kufanya utafiti na kubaini ni nini kinachoendelea katika mgodi ule? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna hali ya uchafuzi mkubwa wa mazingira katika eneo lile la uchimbaji wa madini (utiririshaji wa maji na utupaji hovyo wa taka). Je, Serikali ipo tayari sasa kwenda na kuangalia na namna gani uhifadhi wa mazingira unafanyika katika eneo la mgodi?

Name

Salome Wyckiffe Makamba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI K.n.y. WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Mfaume kwa kufuatilia kwa karibu na kuhakikisha kwamba madini yanayopatikana katika Jimbo lake la Morogoro Kusini yanawanufaisha Wana-Morogoro Kusini. Kuhusu swali la kwanza, taarifa ambazo Serikali inazo, kama nilivyojibu katika swali la msingi, ni kwamba wako katika hatua ya ujenzi wa miundombinu na baada ya hapo wataanza uzalishaji mwezi Juni, 2026.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge, ndiye anatoka mahali husika na anayelala na mgonjwa ndiyo anajua mapigo yake. Ninaomba nitumie fursa hii kuwaelekeza wataalamu wetu wa Wizara ya Madini, kwenda kufanya uchunguzi na kujua nini kinaendelea katika eneo hili, kwa sababu ni haki ya Wana-Morogoro Kusini kuhakikisha kwamba wananufaika na kupata ajira kwenye kazi ambazo Serikali imeelekeza zitafanywa na wazawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili kwenye eneo la Duthumi, kabla mgodi huu haujaanza, kulifanyika tathmini ya athari ya mazingira pale na andiko la usimamizi wa mazingira na jamii yaani Environmental and Social Management Plan liliandikwa na kuhakikisha kwamba hakutatokea athari za mazingira. Ninakuahidi Mheshimiwa Mbunge, Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kupitia NEMC, tutakuja kufanya tathmini na kuhakikisha wananchi wa Morogoro Kusini hawaathiriki na uchimbaji wa madini unaoendelea katika eneo lako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Primary Question

MHE. ZUBERI Y. MFAUME aliuliza: - Je, lini uchimbaji wa madini katika maeneo ya Sesenga na Duthumi utaanza baada ya leseni za uchimbaji kutolewa?

Supplementary Question 2

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, kumekuwa na mtindo wa leseni zinatolewa Dar es Salaam kwenye mtandao, halafu wanaenda kuchimba kule Tarime Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyozungumza hapa sasa hivi kuna mgogoro Kata ya Kiore na Kata ya Komaswa, kuna watu wawili wameshapoteza maisha. Kwa sababu kwenye leseni, wale wananchi wa kawaida hawajui, wameanza kuchimba akaibuka mtu mwenye leseni. Sasa kauli ya Serikali kwa sasa, kuhakikisha kwamba wanaenda, huyu mwenye leseni ambaye hajulikani kule, wakae na wananchi wazungumze na waoneshe watu watanufaikaje na machimbo yale ili amani irejee katika eneo hilo?

Name

Salome Wyckiffe Makamba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI K.n.y. WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Waitara, kwa kweli amekuwa ni mfuatiliaji mzuri wa sekta ya madini na tunafahamu kwamba katika maeneo ya Tarime kule Nyamongo, kuna uchimbaji mkubwa na kuna reserve kubwa sana ya madini hasa ya dhahabu. Mheshimiwa Waitara, unafahamu utaratibu wa upatikanaji wa leseni, ni lazima uwe jumuishi na ushirikishe wananchi pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, hata leseni inapokuwa imetoka ni kazi ya maafisa madini wa eneo husika kwenda kuonesha demarcation za maeneo ambayo mwekezaji amepewa leseni. Kwa sababu hiyo, kama kuna mgogoro, sisi kazi yetu Serikali ni kuhakikisha kwamba watu wanafanya kazi katika mazingira salama na yenye amani. Niwaelekeze Maafisa Madini wa Tarime, waende pale kuweza kuonesha demarcation ya maeneo kwa ajili ya mwekezaji na eneo kwa ajili ya wananchi ili kuweza kuondoa migogoro na kuleta tabasamu la utu kwa Watanzania kama ambavyo Mheshimiwa Rais anataka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. (Makofi)