Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2025-2030 Session 3 Sitting 47 Finance Wizara ya Fedha 560 2026-06-10

Name

Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Primary Question

MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza:-

Je, lini Serikali itaweka uzio wa fedha za Mfuko wa Maji ili zisitumike kwenye matumizi mengine ikizingatiwa adha ya maji bado ni kubwa nchini?

Name

Mshamu Ali Munde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. ENG. MSHAMU A. MUNDE)
alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kenneth Ernest Nollo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu msingi wa swali hili, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Nollo kwa namna anavyowapambania wananchi wake wa Jimbo la Bahi kwa sababu najua anahitaji wananchi hawa waweze kupata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Taifa wa Maji awali umeanzishwa kwa Sheria Namba 12 ya mwaka 2009 ya Huduma za Majisafi na Mazingira. Kwa sasa mfuko unatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria Namba 5 ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kwa mujibu wa Kanuni ya 4(1) mpaka (5) ya sheria hiyo, imeelekeza matumizi ya fedha zinazowekwa kwenye akaunti ya Mfuko wa Taifa wa Maji kutumika kwa ajili ya shughuli za maji tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme wazi kwamba pesa zinazoingia kwenye mfuko huo zinatumika kwa shughuli za maji kwa mujibu wa kanuni hii ambayo nimeitaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme kwa kifupi kwamba sheria hii na kanuni ambayo imetajwa, Mheshimiwa muuliza swali ana wasiwasi kwamba fedha hizi zikikusanywa hazipelekwi kwenye Mfuko wa Maji kama ipasavyo, lakini nimhakikishie kwamba kwa kushirikiana na Kamati ya Kudumu ya Bajeti, Waziri wa Fedha anakuja na mabadiliko ya sheria ambayo yataenda kuboresha ufanisi wa kanuni hii kwamba sasa pesa zote zinazokusanywa kutoka kwenye vyanzo vya kuleta kwenye mfuko juu zitapelekwa moja kwa moja kwenye mfuko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)