Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Primary Question

MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza:- Je, lini Serikali itaweka uzio wa fedha za Mfuko wa Maji ili zisitumike kwenye matumizi mengine ikizingatiwa adha ya maji bado ni kubwa nchini?

Supplementary Question 1

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani umeona Mheshimiwa Naibu Waziri anavyoambaa ambaa, kuna tatizo kwenye jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliweka chanzo mahsusi kwa ajili ya Mfuko wa Maji, na ni shilingi 50 kwa lita ya mafuta ambayo tunanunua na fedha hizi kwanza zimewekewa ukomo…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kenneth Nollo, tafadhali ongeza sauti na ukikaribie kipaza sauti.

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Maji ulianzishwa na Bunge na kutafuta chanzo ambacho ni shilingi 50 kwa lita ambayo tunanunua. Bahati mbaya kwanza mfuko huu umewekewa ceiling (ukomo) wa matumizi, lakini pamoja na hivyo, fedha hizi zimekuwa zikidokolewa na Serikali badala ya kwenda kutatua tatizo la maji na sote tunajua tatizo la maji hapa nchini ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa msingi wa swali langu ni
kwamba, ni lini fedha hizi zitaacha kudokolewa, ziende zikafanye kazi kama ambavyo imetarajiwa na kwa lengo la kutatua tatizo kubwa la maji tulilonalo hapa nchini? (Makofi)

Swali langu la pili ni kwamba tumekuwa tunapata NGOs na wafadhili wanaosaidia miradi ya maji. Bahati mbaya Serikali inatoza fedha tena kwenye miradi hiyo ambayo tunasaidiwa. Sasa nataka niiulize Serikali, ni lini itaondoa sheria hii, kwa sababu anayekuja kututatulia tatizo unataka tena umtoze kodi? Nakushukuru. (Makofi)

Name

Mshamu Ali Munde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. ENG. MSHAMU A. MUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nollo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kama nilivyotangulia kujibu kwenye swali la msingi kwamba kwa kushirikiana na Kamati ya Bajeti, Waziri kesho anakuja na maboresho ya sheria kwenye ile mifuko ambayo itafanya fedha hizo ziende moja kwa moja kwenye mifuko, lakini pia suala la miradi inayotekelezwa na
wadau wa maendeleo kwamba inatozwa kodi, niseme wazi kwamba miradi hiyo inapokuwa inabuniwa au inaletwa kwenye halmashauri au kwenye taasisi za Serikali, taasisi hizo zina uwezo wa kuomba msamaha ya kodi kama wanahitaji na si automatic kwamba ukianzisha mradi wa maji kwa mfano kwamba utapata
msamaha moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi ni kwamba kama kuna mahitaji ya msamaha wa kodi, taasisi husika inabidi iombe kutoka kwenye Mamlaka ya Mapato Tanzania ili kupata msamaha husika, hasa hasa pengine kama kuna ongezeko la thamani (VAT)
na hii nitoe rai kwenye taasisi zote, Maafisa Masuuli wanapokuwa na miradi ambayo inaletwa na wahisani au wadau wa maendeleo, basi kabla mradi haujaanza kutekelezwa taasisi hizo kama wanahitaji, zijipange kuomba msamaha na bahati nzuri Mamlaka ya Mapato Tanzania ilishatoa mafunzo kwa viongozi wote wa mamlaka hizo, hasa hasa Serikali za Mitaa wanafahamu, lakini pia viongozi, Mameneja wa RUWASA ambao wanatekeleza miradi ya maji, walipata mafunzo kutoka Mamlaka ya Mapato
Tanzania ya namna ya kuomba msamaha wa kodi hasa Kodi ya Ongezeko la Thamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mamlaka nyingine zote na
taasisi za Serikali. Wanapokuwa na miradi, najua Miradi ya SEQUIP, Miradi ya BOOST ambayo inatekelezwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, kama wanahitaji kuomba msamaha wa kodi kwa ile miradi ambayo haina makubaliano ya Serikali ya awali ya kwamba miradi hiyo itakuwa ina msamaha, basi wana wajibu wa
kuomba msamaha na wanaomba kupitia mfumo ambao wengi wao wameshapata mafunzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.

Name

Ally Mhata Yahya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Primary Question

MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza:- Je, lini Serikali itaweka uzio wa fedha za Mfuko wa Maji ili zisitumike kwenye matumizi mengine ikizingatiwa adha ya maji bado ni kubwa nchini?

Supplementary Question 2

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo ya viongozi wetu
wakuu, kwa maana ya Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu ni maagizo. Waziri Mkuu, aliagiza ndani ya Bunge lako hili Tukufu mwezi wa tatu kwamba fedha zote za mifuko zipelekwe moja kwa moja kwenye mifuko. (Makofi)

Naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri, agizo hilo la Waziri Mkuu tangu mwezi wa tatu limetekelezwa kwa kiwango gani? (Makofi)

Name

Mshamu Ali Munde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. ENG. MSHAMU A. MUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mhata, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli lilitoka agizo kutoka kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu na Wizara ya Fedha iko kwenye utekelezaji wa agizo hilo. Kwa maeneo ambayo miradi inatekelezwa na mfuko huo au mifuko hiyo, watakubaliana na mimi kwamba yapo maeneo ambayo fedha zimeshapelekwa kwa mujibu wa maelekezo ya Waziri Mkuu ambayo yalitolewa hapa hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Mipango na Uwekezaji.

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongeze tu kwamba Serikali
imechukua kwa uzito maoni ya Waheshimiwa Wabunge juu ya mifuko na kesho Mheshimiwa Waziri wa Fedha ataeleza vizuri namna ambavyo Serikali itatekeleza jambo hilo kwa umakini mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge walielewe hilo kwamba suala la mifuko ya maji, sauti hizi Serikali imezisikia na kesho katika Bajeti ya Serikali Mheshimiwa Waziri wa Fedha ataliweka vizuri. Nashukuru sana. (Makofi)