Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
											Name
Ally Juma Makoa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kondoa Mjini
Primary Question
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza:- Je, lini fedha za ujenzi wa Majengo ya X-ray, OPD, Wodi za Wagonjwa, Mortuary, Kuchomea Taka, kufulia na Walk ways zitapelekwa Vituo vya Afya vya Kondoa?
Supplementary Question 1
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru na ninashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nina maswali ya nyongeza.  Swali la kwanza; sasa, kwa kuwa miundombinu hii ni muhimu sana na wagonjwa wanapokosa miundombinu hii wanalazimika kuletwa Hospitali ya Wilaya kwa tabu sana. Pia, kwa sababu vituo vyote hivi vya afya havina ambulance, Serikali inasemaje kuhusu kutupatia ambulance kwa ajili ya kuhudumia vituo hivi wakati tukisubiria fedha za kukamilisha miundombinu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; niliomba Kituo cha afya kile cha Jimbo cha Kimkakati kujengwa Kondoa Mjini. Je, ni lini Serikali Serikali itatuletea fedha hizi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo hicho cha afya?
 
											Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
								NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba, vituo hivi vya afya ambavyo ameviwasilisha yeye mwenyewe Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ambavyo vina upungufu wa miundombinu hii tayari tumeanza kuviweka kwenye mpango kwa ajili ya kukamilisha miundombinu hiyo kwa awamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii pia kumwelekeza na kumsisitiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kondoa, kuna baadhi ya miundombinu kwa mfano walkways ziko ndani ya uwezo wa mapato ya ndani ya halmashauri. Kwa hiyo, wahakikishe kwenye bajeti zao za ndani wanatenga fedha kwa ajili ya kujenga walkways za kutembelea wagonjwa wakati Serikali Kuu ikiandaa fedha kwa ajili ya kwenda kujenga miundombinu hii ambayo inahitaji gharama kubwa zaidi. 
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusiana na magari ya wagonjwa. Ni kweli Halmashauri ya Mji wa Kondoa imepata pia magari ya wagonjwa, lakini tunafahamu kwamba bado ina uhitaji mkubwa. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kupeleka magari hayo kwa ajili ya vituo hivyo ambavyo havina magari.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho kuhusiana na Kituo cha Afya cha Kimkakati. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote kwamba, tayari Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeshaainisha kata zote za kimkakati ambazo Waheshimiwa Wabunge waliwasilisha na tayari tuko kwenye hatua ya Wizara ya Fedha kwa ajili ya kuwasilisha fedha hizo kwenye kata hizo kwa ajili ya ujenzi wa vituo hivyo vya afya.  Ahsante.
							
 
											Name
Rashid Abdallah Shangazi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Primary Question
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza:- Je, lini fedha za ujenzi wa Majengo ya X-ray, OPD, Wodi za Wagonjwa, Mortuary, Kuchomea Taka, kufulia na Walk ways zitapelekwa Vituo vya Afya vya Kondoa?
Supplementary Question 2
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri ya Lushoto, Kituo cha Afya Lunguza kimejengwa kwa awamu ya kwanza na bado awamu ya pili ambayo yanahitajika majengo ya mortuary, chumba cha upasuaji na jengo la X- Ray. Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kukamilisha kituo hiki?
 
											Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
								NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali ilishapeleka fedha katika Halmashauri ya Lushoto, Jimbo la Mlalo, kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya katika Kata hiyo ya Lungunza ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nimhakikishie kuwa Serikali inatambua kwamba majengo yaliyojengwa ni ya awamu ya kwanza na tunahitaji fedha kwa ajili ya kujenga majengo ya awamu ya pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tunafahamu umuhimu wa jengo la upasuaji, wodi pamoja na majengo mengine na tayari tutaweka kwenye mpango wa bajeti kwa ajili ya kwenda kumalizia majengo hayo.  Ahsante.
							
 
											Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Primary Question
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza:- Je, lini fedha za ujenzi wa Majengo ya X-ray, OPD, Wodi za Wagonjwa, Mortuary, Kuchomea Taka, kufulia na Walk ways zitapelekwa Vituo vya Afya vya Kondoa?
Supplementary Question 3
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, tunaishukuru Serikali kwa watu wa Sirari na Nyamwaga kupata X-Ray machine.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Nyamongo kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022 ina zaidi ya watu 60,000. Vilevile, Vituo vya Afya Sungusungu, Nyamongo na Kerende hawana X-Ray Machine. Ni lini Serikali itapeleka X-Ray machine ili kusaidia watu wa Nyamongo wasiumie sana hasa kwenye machimbo ya mgodi? Ahsante. (Makofi)
 
											Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika vigezo vya kipaumbele katika kupeleka vifaatiba ni pamoja na idadi ya wananchi. Pia, kwa kuwa Kata hiyo ya Nyamongo ina wananchi takribani 60,000 ina kila sababu ya kupata mashine ya X-Ray. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutaiweka kwenye mpango kwa ajili ya kupeleka X-Ray katika Kituo hicho cha afya. Ahsante sana.
 
											Name
Eng. Ezra John Chiwelesa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Biharamulo Magharibi
Primary Question
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza:- Je, lini fedha za ujenzi wa Majengo ya X-ray, OPD, Wodi za Wagonjwa, Mortuary, Kuchomea Taka, kufulia na Walk ways zitapelekwa Vituo vya Afya vya Kondoa?
Supplementary Question 4
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Biharamulo umekamilika na unaendelea vizuri na wananchi wanapata huduma. Hata hivyo, yako maombi yetu ya jengo la theatre, wodi ya wanaume, walkways pamoja na kichomea taka. Je, ni lini ile pesa shilingi milioni 750 itafikishwa pale ili kila kitu kiweze kukamilika na wananchi wapate huduma kikiwa kimekamilika? Ahsante sana.
 
											Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Chiwelesa kwamba ujenzi wa Hospitali zetu za Halmashauri na vituo vya afya huenda kwa awamu na tumejenga majengo kadhaa katika Hospitali ya Wilaya ya Biharamulo na ninafahamu kwamba kuna upungufu wa majengo hayo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo la Biharamulo, kwamba Serikali inatambua na itakwenda kukamilisha majengo yaliyobaki ili tuweze kutoa huduma zote muhimu kwa ngazi ya hospitali katika Halmashauri ya Biharamulo.