Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
											Name
Nusrat Shaaban Hanje
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza:- Je, lini Wananchi wa Kijiji cha Sambaru, Kata ya Mang'onyi, Singida Mashariki, watapata maji safi na salama?
Supplementary Question 1
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, pamoja na kwamba, Serikali inaendelea na zoezi la kuchimba visima, hususan katika Kijiji hiki cha Sambaru kwenye Kata ya Mang’onyi, bado kuna changamoto ya miundombinu ya usambazaji wa maji, kikiwemo kisima hiki kilichochimbwa juzi. 
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, kuna kata nyingine ambazo visima vimechimbwa, lakini bado hakuna miundombinu ya usambazaji wa maji, kikiwemo Kijiji cha Msule, Kijiji cha Sakaa pamoja na Kijiji chenyewe cha Misughaa, kwenye Kata ya Misughaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni kwa nini Serikali wakati inaweka mipango ya kuchimba visima isiunganishe na package ya usambazaji wa maji ili isiwe tu tunasema kwamba tumechimba visima kadhaa na tutaendelea kutafuta vyanzo, tuwe tunaweka kabisa, ili tuhakikishe maji yanawafikia wananchi kama ambavyo tumewaahidi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kuna mradi ambao unaendelea kuzinduliwa katika mikoa kadhaa nchini, mradi wa visima 900. Nilikuwa nauliza, katika jimbo letu la Singida Mashariki, ikiwemo Wilaya ya Ikungi, majimbo yote mawili, Mkoa wa Singida kwa ujumla, nataka nifahamu kama mkoa wetu pia umo katika huu mradi wa visima 900? Nakushukuru. (Makofi)
 
											Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
								NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali zuri kabisa kutoka kwa Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kazi kubwa ambayo Waheshimiwa Wabunge wanaifanya, akiwemo Mheshimiwa Nusrat, ya kupambania akina mama wanaohitaji kutuliwa ndoo kichwani. Ni programu ambayo ilizinduliwa na Mheshimiwa Rais, lakini visima 900 ni visima ambavyo vinachimbwa nchi nzima katika mikoa yote ya Tanzania Bara na vilevile kwa upande wa Singida imo katika programu ya visima hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na Mkoa wa Singida ulitengewa shilingi bilioni 18.6, kwa ajili ya miradi 43 inayotekelezwa katika Mkoa wa Singida. Vilevile visima hivi, zaidi ya 636, tayari vimeishapata maji na vingine tunaendelea kujenga zile point source ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali la kwanza ambalo Mheshimiwa Mbunge ameulizia, kwamba tunapochimba visima tuwe na package moja kwa moja ya usambazaji; tunachokifanya kwanza kabisa ni kuchimba ili kuona kama kuna maji. Pili, tunafanya test ya pampu kujua wingi wa maji, ili tuweze kujua ni pampu ya aina gani au miundombinu ipi tutakayoiweka pale, ifikie idadi ipi ya watu kulingana na maji ambayo tumeyapata?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi tunachokifanya ni kuhakikisha kwamba wananchi wote ambao wamezunguka maeneo hayo tunawafikishia maji kulingana na idadi, kulingana na kiu ya maji ambayo tumeipata na kulingana na kisima ambacho tumekichimba. 
Mheshimiwa Naibu Spika, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, Serikali imejipanga kwenye kuchimba, kujenga miundombinu, usambazaji wake na utoaji wa huduma yenyewe ya maji; yawe safi na salama na yenye kutosheleza, ahsante sana.
							
 
											Name
Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sengerema
Primary Question
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza:- Je, lini Wananchi wa Kijiji cha Sambaru, Kata ya Mang'onyi, Singida Mashariki, watapata maji safi na salama?
Supplementary Question 2
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Ni kwamba, Wizara ya Maji ilileta roli kwa ajili ya kuchimba visima 39 katika Wilaya ya Sengerema, hasa Jimbo la Sengerema na gari lilikuwepo pale kwa ajili ya kuchimba visima hivyo, lakini lile gari lilitoroshwa usiku. Ni lini hilo gari litarudishwa Sengerema, kwa ajili ya kuja kufanya kazi ya kuchimba visima? (Makofi)
 
											Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, sina uhakika kuhusu utoroshwaji wa gari, lakini natambua uhitaji wa gari hilo ili wananchi wa Sengerema wachimbiwe visima na wapate huduma ya maji safi na salama, ahsante sana.
 
											Name
Issa Jumanne Mtemvu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibamba
Primary Question
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza:- Je, lini Wananchi wa Kijiji cha Sambaru, Kata ya Mang'onyi, Singida Mashariki, watapata maji safi na salama?
Supplementary Question 3
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Rais kwa kukamilisha tenki la ujazo wa lita milioni tisa kule Bangulo na sasa wanaanza usambazaji wa maji katika maeneo mbalimbali. Je, ni ipi commitment ya Serikali kwenye kumaliza usambazaji wa maji katika Mtaa wa King’azi A na B, Mtaa wa Saranga na Mtaa wa Ukombozi ili wananchi hawa sasa wafurahie maji safi na salama? (Makofi)
 
											Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
								NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mtemvu kwa kazi nzuri anayoifanya kwa wananchi wa Kibamba. Ni kweli kabisa utekelezaji wa ujenzi wa tenki hili la lita milioni tisa, Mheshimiwa Mbunge tumekuwanaye wakati tunakagua mradi huu na sasa umeshakamilika katika ujenzi wake, lakini sasa zoezi linalofuatia ni kusambaza maji katika maeneo yote, ambapo katika study iliyofanyika ni kwamba, maeneo yote ambayo yanaguswa yatafikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaenda hatua kwa hatua kulingana na hali halisi ya upatikanaji wa fedha. Lengo ni kwamba, tunapofika Oktoba, 2025 basi wananchi wawe wamepata huduma ya maji safi na salama, ahsante sana. 
							
 
											Name
Ghati Zephania Chomete
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza:- Je, lini Wananchi wa Kijiji cha Sambaru, Kata ya Mang'onyi, Singida Mashariki, watapata maji safi na salama?
Supplementary Question 4
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi. Tunaishukuru sana Serikali kwa kuendelea kutekeleza miradi ya maji katika Mkoa wetu wa Mara, lakini ningependa kujua sasa ni lini Serikali itaanza kutekeleza mradi wa maji kutoka Musoma Mjini kuelekea Wilaya ya Butiama katika Kata ya Bisumwa – Nyankanga na Bukabwa ili wananchi wale waweze kupata maji hayo? Ahsante. (Makofi)
 
											Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
								NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ghati kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhamira ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuhakikisha kwamba wananchi wote wanapata huduma ya maji safi na salama. Maji yapatikane, maji yafikike na maji yaweze kunyweka yakiwa na ubora unaotakiwa. 
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Musoma, tayari Serikali imeshatekeleza miradi kadhaa chini ya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini mradi mmojawapo wa Mugango – Kiabakari ambao ulikuwa ni kizungumkuti, umeshakamilika na umeshaanza kutoa huduma ya maji safi na salama. 
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muktadha huo, tunaamini kwamba katika maeneo ambayo yamebaki, yakiwemo aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge, Serikali itaendelea kufikisha huduma ya maji safi na salama, ahsante sana.