Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Primary Question

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza: - Je, lini Zahanati za Molemlimani, Muungano, Urafiki, Isanjandugu, Iyombakuzova na Kapumpa zitakamilika?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, ninaipongeza Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wananchi wa Vijiji vya Isanjandugu, Iyombokuzova, Urafiki, Muungano, Kapumpa na Molemlimani wamejitahidi sana kujitolea nguvu zao kwa kushirikiana na mfuko wa jimbo wakajenga maboma hayo.

Je, kwa nini Serikali isiwaunge mkono kwa block grants za Serikali Kuu moja kwa moja badala ya kusubiri bajeti ya ndani ya halmashauri ambayo imekuwa haitoshi ni ndogo, hadi mwaka 2026/2027; kwa nini mwaka huu wasisaidiwe?

Je, ni kwa nini Serikali isichukue orodha ya maboma yote ambayo wananchi wamechangia kwa nguvu za wananchi nchi nzima halafu ikaipangia bajeti kukamilisha maboma yote kabla hatujaanzisha ule Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza natumia nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Joseph George Kakunda kwa namna ambavyo amekuwa akiwasemea wananchi wa Jimbo la Sikonge na kwa namna ambavyo amefuatilia kuona kwamba Serikali inapeleka fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati hizi.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunatambua kwamba wananchi wametoa nguvu zao na natumia nafasi hii kuwapongeza wananchi wa Jimbo la Sikonge na yeye Mheshimiwa Mbunge kwa kutoa fedha za Mfuko wa Jimbo kwa ajili ya ukamilishaji wa baadhi ya maboma.

Mheshimiwa Spika, tumeendelea kutenga fedha kwenye bajeti kila mwaka. Kwa kipindi hiki, katika mwaka huu wa fedha tayari Serikali imeitengea Halmashauri ya Sikonge shilingi 180,000,000 kwa ajili ya ukamilishaji wa Zahanati za Ibumba, Mwamaluga na Ipembe.

Mheshimiwa Spika, wakati huo katika mwaka wa fedha 2026/2027 tutakwenda kukamilisha zahanati hizi kwa shilingi 250,000,000. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba zoezi hili ni endelevu na tutaendelea kutenga fedha kwa awamu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunakamilisha majengo haya ili yaweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, kwa swali la pili, tunafahamu kwamba kuna maboma mengi wananchi wamejenga na Serikali tayari imekwishaainisha. Tuna jumla ya maboma ya zahanati 1,614 ambayo yako kote nchini, yanahitaji fedha za ukamilishaji. Hivi karibuni, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, mwezi mmoja uliopita imetoa zaidi ya shilingi 17,650,000,000 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma 346 kati ya hayo 1,614 ambayo yamekwishatambuliwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea kuyatambua maboma, tunaendelea kutenga fedha kwa awamu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba yanakamilishwa na kutoa huduma.