Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
											Name
Rehema Juma Migilla
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ulyankulu
Primary Question
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga sekondari nyingine katika Kata ya Kanindo kwa kuwa Shule ya Sekondari Kanindo ina wanafunzi wengi?
Supplementary Question 1
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu ya Serikali. Majibu ya Serikali yanadhihirisha kwamba hitaji la kujengewa sekondari mpya katika Kata ya Kanindo liko palepale kutokana na sababu kwamba tayari kwenye majibu ya Serikali yanasema kuna wanafunzi wamehamishwa kutoka Shule ya Sekondari Kanindo na kupelekwa Shule ya Sekondari Ikonongo ambayo ipo kata nyingine ya Milambo, lakini bado wanafunzi wanaosoma hapo wanatembea umbali mrefu sana.
Mheshimiwa Spika, kutoka Kijiji cha Mbeta mpaka ilipo shule ya Sekondari Kanindo ni kilometa 15, lakini kuna vijiji vingine tena vinne ambavyo ni kilometa kuanzia 16 mpaka 20 kufikia shule.  Swali la kwanza; je, Serikali sasa haioni kuna haja ya kuwaunga mkono hao wananchi ambao tayari wameshatenga ekari 20 kwa ajili ya ujenzi wa sekondari hiyo?
SPIKA: Mheshimiwa Rehema umeshaanza swali la pili au bado ni la kwanza?
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, la kwanza.
SPIKA: Mheshimiwa, la kwanza umeshatoa maelezo mwanzo na swali umeshauliza, sasa nenda kwenye swali la pili.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa shule hiyo ina hosteli ambayo ilijengwa na shirika la UN, bweni lenyewe ni moja ambalo lina uwezo wa kuwa-accommodate wanafunzi 48 tu. Je, Serikali iko tayari sasa wakati tukiendelea kusubiri ujenzi wa shule mpya kutujengea hosteli zingine ili wanafunzi wanaotoka mbali waweze kusoma katika mazingira ambayo mi karibu na nyumbani kwao? Ahsante. (Makofi)
 
											Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
								NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, ninaomba nimfahamishe Mheshimiwa Rehema Migilla kwamba Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha inaendelea kuboresha sekta hii muhimu ya elimu msingi.  Katika kipindi cha miaka minne katika Jimbo la Ulyankulu imejenga shule za sekondari nne na mipango ya kuendeleza miundombinu kwa kujenga shule nyingine bado ipo. 
Mheshimiwa Spika, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Rehema Migilla kwamba Serikali itaendelea kuhakikisha inaleta fedha katika Jimbo hili la Ulyankulu kwa ajili ya kuendelea kujenga shule ambazo zitaweza kuwatosheleza wananchi wako ili vijana waweze kupata sehemu ya kuendelea kupata elimu.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake kuhusu ujenzi wa hosteli. Serikali ikishirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo itaendelea na jitihada za kuhakikisha kwamba kwa kushirikiana pia na wananchi (wazazi wa wanafunzi) kujenga hosteli ili ziweze kuwasaidia wanafunzi wetu na hasa wale ambao wanasafiri umbali mrefu, kwa maana Serikali msingi mzima wa kujenga shule hizi za kata ni kuhakikisha kwamba zinapunguza msongamano kwenye maeneo ambayo wanafunzi ni wengi, lakini pia inapunguza umbali mrefu wa wanafunzi kutembea kufika katika shule.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na jitihada hizi mbili ili kuhakikisha kwamba inaendelea kujenga hizi shule ambazo zitaweza kuwawezesha wanafunzi katika Jimbo lako la Ulyankulu waweze kupata sehemu nzuri ya kujifunzia.
							
 
											Name
Omari Mohamed Kigua
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilindi
Primary Question
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga sekondari nyingine katika Kata ya Kanindo kwa kuwa Shule ya Sekondari Kanindo ina wanafunzi wengi?
Supplementary Question 2
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwenye Wilaya ya Kilindi, Kata ya Msanja ndiyo kata yenye idadi kubwa ya wananchi, lakini ina shule ya sekondari moja. Je, nini mpango wa Serikali wa kujenga shule mpya? (Makofi)
 
											Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, shule 2,441 zimejengwa za sekondari. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Omari Kigua kwamba hata katika Kata hii ya Msanja ambapo kuna uhitaji wa shule mpya hii ya sekondari ya kata, nimhakikishie Serikali kupitia mpango wake wa kutenga fedha kila mwaka wa bajeti itafika ili kuhakikisha shule hiyo imejengwa ili kupunguza msongamano, lakini pia kupunguza umbali mrefu ambao wanafunzi wetu wanatembea kufika shuleni. (Makofi)
 
											Name
Dorothy George Kilave
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Temeke
Primary Question
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga sekondari nyingine katika Kata ya Kanindo kwa kuwa Shule ya Sekondari Kanindo ina wanafunzi wengi?
Supplementary Question 3
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, je, ni lini sasa Serikali itajenga shule ya sekondari katika Kata ya Makangarawe ndani ya Jimbo la Temeke? Ahsante. (Makofi)
 
											Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea na jitihada kubwa sana za kuendelea kuimarisha miundombinu katika Sekta ya Elimu na hasa kuhakikisha pia, inaongeza ujenzi wa shule za sekondari. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Dorothy Kilave kwamba, Serikali kupitia mapato ya ndani ya halamashauri na kupitia fedha kutoka Serikali Kuu itafika katika eneo alilolitaja la Makangarawe, kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, shule hii inajengwa, ili iweze kuwanufaisha wanafunzi wetu.
 
											Name
Charles Muguta Kajege
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwibara
Primary Question
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga sekondari nyingine katika Kata ya Kanindo kwa kuwa Shule ya Sekondari Kanindo ina wanafunzi wengi?
Supplementary Question 4
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, kuna wanafunzi wa sekondari zaidi ya 100 kutoka katika Visiwa vya Buguma, Sozia na Nafuba. Je, ni lini Serikali itawasaidia wananchi wa visiwa hivi kukamilisha ujenzi wa shule ya sekondari katika Kisiwa cha Nafuba?
 
											Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuendelea kuboresha Sekta ya Elimu Msingi kwa kuhakikisha, miongoni mwa mambo mengine, inajenga miundombinu ya shule. Katika eneo la visiwa ambalo Mheshimiwa Mbunge Charles Kajege amelitaja, ninaomba nimhakikishie kwamba, tutaendelea kuhakikisha fedha zinafika. Kila mwaka wa bajeti tutatenga fedha na zinafika, kwa ajili ya kuhakikisha shule katika maeneo hayo zinajengwa ili watoto wa wananchi katika visiwa hivi na wenyewe waweze kupata shule, kwa ajili ya kupata elimu. (Makofi)
 
											Name
Shabani Omari Shekilindi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lushoto
Primary Question
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga sekondari nyingine katika Kata ya Kanindo kwa kuwa Shule ya Sekondari Kanindo ina wanafunzi wengi?
Supplementary Question 5
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, Shule za Sekondari Shambalai, Mlongwema na Ubiri hazina uzio. Je, ni lini Serikali itajenga uzio katika shule hizo? (Makofi)
 
											Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali inajenga uzio katika shule zetu, kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa wanafunzi na usalama wa mali za shule. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Shabani Shekilindi kwamba, kupitia mapato ya ndani ya halmashauri tutajenga uzio katika shule alizozitaja, kwa ajili ya kuhakikisha usalama huo wa wanafunzi unapatikana na pia wa mali za shule.