Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
											Name
Ally Juma Makoa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kondoa Mjini
Primary Question
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza kazi ya kurejesha Mto Kondoa katika njia yake ya asili?
Supplementary Question 1
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Spika, pamoja na maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.   Swali la kwanza; kwa kuwa, tayari athari zimetokea, sasa ni nini mpango wa Serikali sasa kuhakikisha mto huo unarejeshwa kwenye mkondo wake wa asili? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa, NEMC walifika kule, ninataka kujua sasa, walikuja na suluhisho gani kurejesha ule mto katika mkondo wake wa asili, ili kuepusha madhara ya uharibifu ambayo yanaendelea kutokea kwenye mali za wananchi pamoja na miundombinu ya Serikali? Ninashukuru. (Makofi)
 
											Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
								NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Makoa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, upo mpango ambao, kama Serikali, tumeshaanza kuuandaa, kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, tunaokoa huu Mto Kondoa. Moja ni kwamba, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais (NEMC) kwa kushirikiana na halmashauri, tayari kupitia bajeti ambayo tumeisoma tutahakikisha tunatenga fedha kwa lengo na madhumuni ya kuweza kufanya baadhi ya mambo katika mto huu, ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu. Kubwa zaidi ni kuhakikisha kwamba, tunaufufua mto huu kwa kutoa mchanga na vitu vingine, ili mto huu urudi kwenye asili yake.
Mheshimiwa Spika, ninamwomba Mheshimiwa Mbunge, pamoja na wananchi wa Jimbo hilo la Kondoa waendelee kuwa na subira. Fedha hizi zitakapokuwa tayari basi tutahakikisha kwamba, tunazipeleka, kwa ajili ya kuokoa hiyo hali.
Mheshimiwa Spika, lipo suluhisho ambalo tumeshalifikia; la kwanza ni kutafuta fedha, kama hatujapata fedha hatuwezi kufanya hili jambo. Kwa hiyo, tutakapopata fedha tutahakikisha kwamba, tunakwenda kutoa elimu na tutahakikisha kwamba, tunakwenda kufanya baadhi ya mambo ikiwemo kurejesha mto huu katika hali kwa sababu, changamoto kubwa ya mto huu ni pamoja na kutuama kwa mchanga na kupanuka kwa mto siku hadi siku.  Ninakushukuru. (Makofi)
							
 
											Name
Abdul Yussuf Maalim
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Amani
Primary Question
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza kazi ya kurejesha Mto Kondoa katika njia yake ya asili?
Supplementary Question 2
MHE. ABDUL YUSSUF MAALIM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mabadiliko ya tabia-nchi ni janga la Kitaifa ambalo linaathiri sehemu tofauti, ikiwemo Zanzibar na huku Tanzania Bara. Je, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Serikali ya Zanzibar zitapeleka fedha lini, ili kusaidia kuondoa matatizo hayo ya tabianchi? (Makofi)
 
											Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
								NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, zipo juhudi nyingi sana ambazo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, tumekuwa tunashirikiana kwenye hatua mbalimbali za kutafuta fedha, kwa ajili ya kukabiliana na athari kubwa ya mabadiliko ya tabianchi. Fedha hizo, baadhi zimeshapatikana na ndiyo maana kuna miradi mingi tumeianzisha kupitia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, miradi hiyo imeanzishwa Zanzibar, Unguja na Pemba, ikiwemo mikubwa ya kukabiliana na athari kubwa ya mabadiliko ya tabianchi, hasa miradi ya kurejesha ardhi, ambayo imekata tamaa, miradi ya mifugo, miradi ya maji, miradi ya ujenzi wa kuta na miradi mingine mbalimbali. Ninamwambia tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutaendelea kushirikiana kutafuta fedha na hata tunapokwenda kwenye vikao vikubwa vya Kimataifa, vya kwenda kutafuta fedha za mabadiliko ya tabianchi huwa tunawashirikisha wenzetu wa Zanzibar kwa lengo na madhumuni ya tunapopata tuhakikishe na kule tunapeleka, kwa ajili ya kutengeneza miradi hiyo.  Ninakushukuru.
							
 
											Name
Abubakar Damian Asenga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Primary Question
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza kazi ya kurejesha Mto Kondoa katika njia yake ya asili?
Supplementary Question 3
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itafukua Mto Lumemo na kuboresha tuta la Mto Lumemo, upande wa Kata ya Lumemo, ili kupunguza athari za mafuriko kwa wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara?
 
											Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
								NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asenga Abubakari wa Kilombero, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika shilingi bilioni 81 ambazo Waheshimiwa Wabunge wametuidhinishia katika bajeti ambayo tumeisoma mwezi uliopita, tarehe 25, Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, miongoni mwa kazi ambazo tunakwenda kuzifanya ni kuhakikisha kwamba, kwanza tunakwenda kusafisha mito ambayo imekuwa ni changamoto, hasa kipindi hiki cha mvua na kile kipindi kingine ambacho mito huwa inajaa mchanga na mambo mengine. Kikubwa zaidi ni, fedha zile tunakwenda kuzitumia, kwa ajili ya kujenga kuta mbalimbali, ikiwemo maeneo ya huko Kilombero, Nungwi, Mtwara, Lindi na maeneo mengine yenye changamoto ambazo hizi kuta zinahitajika zijengwe. Tunakwenda kufanya hiyo kazi.  Ninakushukuru. (Makofi)
							
 
											Name
Abdallah Dadi Chikota
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyamba
Primary Question
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza kazi ya kurejesha Mto Kondoa katika njia yake ya asili?
Supplementary Question 4
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Changamoto iliyopo Mto Kondoa inafanana na ile iliyopo Mto Ruvuma. Sasahivi Mto Ruvuma unahama njia yake ya asili na hivyo kuleta madhara katika Vijiji vya Maembe Chini, Kitaya na Kilambo. Je, Serikali ina mkakati gani wa kukabiliana na tatizo hilo? (Makofi)
 
											Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
								NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge. Ni kwamba, kama nilivyoeleza katika majibu yaliyopita, changamoto kubwa ni tunatafuta fedha; fedha zitakapopatikana tunakwenda kutatua changamoto ya mito yote Tanzania, ama mito yote ambayo imeleta changamoto, hasa kile kipindi cha mvua kubwa. 
Mheshimiwa Spika, ninataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge, changomoto hizi za mito hii, ukiachia mbali mvua kubwa ambayo inanyesha, bado kuna baadhi ya wananchi wanasababisha. Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge tusaidiane hili; kwamba, tuendelee kuwaambia wananchi wetu wasifanye shughuli za kibinadamu katika vyanzo hivi vya maji.  Aidha, wazingatie Sheria yetu, ile ya Mazingira, sheria ya mita 60. Wafanye, lakini mbali kidogo kwa lengo na madhumuni ya mito hii ibakie kuwa salama, kwa ajili ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira.  Ninakushukuru. 
							
 
											Name
Joseph George Kakunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Primary Question
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza kazi ya kurejesha Mto Kondoa katika njia yake ya asili?
Supplementary Question 5
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, ninafurahia sana majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri.  La kwangu ni, sisi Sikonge 100% ni wana mazingira na tuna mambo mengi ya kujadiliana ana kwa ana na Mheshimiwa Naibu Waziri. Tangu Wizara hii ianzishwe hajawahi kutembelea Sikonge. Je, lini atatembelea Sikonge, ili tukae kwa pamoja tumwoneshe, kwa maneno mengine tujadili kwa pamoja?
SPIKA: Sasa Mheshimiwa Mbunge, wewe si ndiyo uko kwa niaba ya Wanasikonge? Si ukae tu na Mheshimiwa Naibu Waziri? Au kuna changamoto maalum inayohusu mito ili ndiyo nijue sasa, Mheshimiwa Naibu Waziri ajibu, ama? (Makofi)
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, mito yetu mingi perennial inakauka. Sasa kuna mambo mengi ya kujadili na yeye kuyaona ili tuweze kupata solution. (Makofi)
 
											Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
								SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, pokea ombi hilo la Mheshimiwa Kakunda. 
Ahsante sana kwa majibu yako kwa maswali ya Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)