Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
											Name
Aziza Sleyum Ally
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. AZIZA S. ALLY K.n.y. MHE. SEIF K. S. GULAMALI aliuliza:- Je, lini Serikali itatoa fedha za ujenzi wa Viwanja vya Michezo Sekondari ya Ziba, Manonga?
Supplementary Question 1
MHE. AZIZA S. ALLY: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; je, Serikali inatambua Shule ya Ziba ni shule mojawapo ya wasichana ambao wanacheza mpira wa miguu na ndiyo inayotoa vipaji mbalimbali katika shule Kitaifa na kuwakilisha uchezaji wa mpira wa miguu Kimataifa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Serikali haioni umuhimu wa kujali viwanja katika shule mbalimbali nchini; viwanja pamoja na michezo kwa kuwa, michezo ni biashara kubwa sana katika nchi yetu, ili iweze kutoa vipaji mbalimbali vya vijana watakaoenda kucheza Kimataifa?  Ninashukuru. (Makofi)
 
											Name
Hamis Mohamed Mwinjuma
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muheza
Answer
								WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA, NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, moja, Serikali inaipongeza sana Shule ya Sekondari ya Ziba, ambayo imefanya vizuri sana katika kulea vipaji vya watoto wa kike, wasichana, katika michezo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mchezo wa mpira. Kwa kuzingatia hilo Wizara itatuma wataalam kwenda katika Shule hiyo ya Ziba ili kuona ni jinsi gani watashirikiana, lakini pia, pamoja na Mbunge wa Manonga, ili kuendeleza vipaji hivyo ambavyo ni muhimu kwa Taifa letu na kuona uwezekano wa tutakapokuwa na academy ya michezo, ambayo inajengwa Malya katika Mkoa wa Mwanza, ishirikiane vipi na Shule ya Sekondari ya Ziba na shule nyingine ambazo zina wasichana wenye vipaji kama hao.
Mheshimiwa Spika, kuhusu ujenzi wa viwanja vya michezo katika shule. Wizara na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, inachambua kuona umuhimu wa kuwa na mpango maalum wa kuweza kuboresha viwanja vya michezo katika shule zote za msingi na sekondari. Hivyo, halmashauri zetu za wilaya, za manispaa na majiji zinatakiwa, katika bajeti zao, ziweke umuhimu katika ujenzi wa viwanja katika shule za msingi na shule za sekondari.
							
 
											Name
Philipo Augustino Mulugo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Songwe
Primary Question
MHE. AZIZA S. ALLY K.n.y. MHE. SEIF K. S. GULAMALI aliuliza:- Je, lini Serikali itatoa fedha za ujenzi wa Viwanja vya Michezo Sekondari ya Ziba, Manonga?
Supplementary Question 2
MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Songwe ni mkoa mpya, ambao hauna uwanja wa michezo, kama vile ulivyo Uwanja wa Sokoine Mbeya. Je, ni lini Serikali itajenga uwanja wa michezo katika mkoa huo na Makao Makuu ya Mkoa pale Vwawa? Ahsante.
 
											Name
Hamis Mohamed Mwinjuma
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muheza
Answer
								WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA, NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ninatambua hali ya Uwanja wa Sokoine na mahitaji ya viwanja katika sehemu mbalimbali za Tanzania; Serikali imewekeza fedha nyingi katika miundombinu ya michezo. Kama mnavyofahamu tunajenga uwanja mpya wa mpira wenye uwezo wa kuchukua watu 32,000 kule Arusha, tunajenga mwingine hapa Dodoma wenye uwezo huohuo.  Tayari katika bajeti ambayo imekwishapitishwa tunaanza uchambuzi yakinifu wa kujenga viwanja vingine katika sehemu mbalimbali za Tanzania vipatavyo 26. Ninaamini kabisa katika hilo, Songwe inaweza kuwa mojawapo ya mikoa, kama itakidhi viwango vitakavyokuwa vimewekwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Uwanja wa Sokoine, nao umo katika mpango wa kuangaliwa tutakapokuwa tumeanzisha Wakala wa Miundombinu ya Michezo, ili kuhakikisha sasa viwanja vyote Tanzania vinasimamiwa na Wakala huyo badala ya Wizara.
SPIKA: Mheshimiwa Waziri, Wakala anaanzishwa lini, ili ndiyo tujue na sisi tutatazamwa miaka miwili, mitatu, minne inayokuja?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA, NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, tuombeane heri. Inshallah baada ya Oktoba. (Kicheko/Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Waziri, hapo sasa inabidi ujibu tu swali letu la Wanambeya kwa kweli. Naona kuna Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Profesa Kabudi kwa majibu mazuri kwa niaba ya Serikali, lakini ninapenda kuongeza kwamba, katika Maandalizi ya AFCON, 2027 Serikali imetenga viwanja vitano, ili vifanyiwe ukarabati. Viwanja hivyo ni Jamhuri, Morogoro; Mkwakwani, Tanga; Sokoine, Mbeya; CCM Kirumba, Mwanza; pamoja na Majimaji, Songea. Hivyo, Kiwanja cha Sokoine cha Mbeya kitaingia kwenye programu ya ukarabati wa viwanja, kwa ajili ya Mazoezi ya AFCON, 2027. (Makofi)
							
 
											Name
Sophia Hebron Mwakagenda
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. AZIZA S. ALLY K.n.y. MHE. SEIF K. S. GULAMALI aliuliza:- Je, lini Serikali itatoa fedha za ujenzi wa Viwanja vya Michezo Sekondari ya Ziba, Manonga?
Supplementary Question 3
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Wilaya ya Rungwe tuna kiwanja kikubwa ambacho kinazungukwa na shule za sekondari mbili na chuo, kinaitwa Kiwanja cha Dkt. Tulia Ackson. Ni lini Serikali italeta fedha kukarabati kiwanja hicho? (Makofi/Kicheko)
 
											Name
Hamis Mohamed Mwinjuma
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muheza
Answer
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA, NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ninapenda kueleza kwamba, Wizara ina mkakati mkubwa sana wa kuboresha viwanja vyote nchini. Kutegemeana na upatikanaji wa rasilimali fedha tutahakikisha viwanja hivyo vinatengenezwa au vinakarabatiwa, ikiwa ni pamoja na kiwanja hicho kinachobeba jina la Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson Mwansasu. Uwezekano upo wa kuangalia kama kinakidhi viwango vya kuwa Kambi ya Kitaifa ya Mashindano ya UMITASHUMITA na UMISETA, kikikidhi viwango hivyo, basi ukarabati wa kiwanja hicho utafanywa haraka sana, ili kuenzi jina la huyo ambaye kiwanja hicho amepewa. (Makofi)
 
											Name
Issaay Zacharia Paulo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Mjini
Primary Question
MHE. AZIZA S. ALLY K.n.y. MHE. SEIF K. S. GULAMALI aliuliza:- Je, lini Serikali itatoa fedha za ujenzi wa Viwanja vya Michezo Sekondari ya Ziba, Manonga?
Supplementary Question 4
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Mbulu ni chimbuko la wanamichezo nchini. Je, Serikali ina mpango gani wa pamoja na Sekta Binafsi kwa kuwa, Uwanja wa Nyerere Stadium katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu unamilikiwa na taasisi binafsi? Ninakushukuru sana.
 
											Name
Hamis Mohamed Mwinjuma
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muheza
Answer
								WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA, NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza ninachukua nafasi hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Issaay kwa kufuatilia sana maendeleo ya michezo, hasa katika Mkoa wa Manyara, ambao unafahamika kuwa na sifa ya kutoa wanariadha wengi. Kwa kutambua hilo, Baraza la Michezo la Taifa limenunua ardhi kubwa Babati, ili kujenga kituo cha kufanya mazoezi, kwa ajili ya wanariadha; ambacho kitatumika, kwa ajili ya Mkoa wa Manyara na wanariadha wote Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la hicho kiwanja, kama nilivyosema, tunakuja na mkakati wa kuboresha viwanja vyote ikiwa ni pamoja sasa na kuwa na menejimenti kamili ya usimamizi wa viwanja. Kwa sababu tunaendelea katika hilo, ninaamini kabisa Manyara na Kiwanja hicho cha Mbulu, itapewa kipaumbele. (Makofi)