Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
											Name
Angelina Adam Malembeka
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuhifadhi mbegu na mimea ya asili kwa ajili ya vizazi vijavyo?
Supplementary Question 1
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwanza, nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo yametoa uelewa mkubwa na kujua kwamba kuna mbegu za asili zinahifadhiwa. Ninashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.  Ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa matunda mengi ya kisasa hayana mbegu na hata yakiwa na mbegu ukipanda hazioti na wakati huohuo Serikali ina sampuli 38,000 imehifadhi hazirudishwi tena kwa wakulima ili kuendeleza mzunguko wa mbegu za asili. Je, Serikali haioni kwamba huo ni mpango maalum wa kuzididimiza na kuzipoteza mbegu zetu za asili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; kwa kuwa baadhi ya matunda, mfano, embe wakati zinatoa maua ni lazima uweke dawa usipoweka dawa unavuna funza badala ya embe. Je, Serikali imejipangaje kukabiliana na athari za dawa hizo kwa ardhi na afya za binadamu? (Makofi)
 
											Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
								NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Malembeka kwa maswali mazuri ya msingi ambayo ameyauliza. Moja, nimthibitishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli kuna matunda ya kisasa ambayo hayana mbegu ambayo ukishapanda ukavuna huwezi kuyapanda tena, lakini haina maana ya kwamba tunaondoa mbegu za asili katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa ambacho kinafanyika, kuna mbegu ambazo zimeboreshwa ambazo zinaitwa improved seeds hicho ni kitu tofauti kabisa na mbegu za GMO. Sasa lengo kubwa la mbegu hizi ambapo zinatumika sasa hivi ni kutokana na mabadiliko ya tabianchi na kukabiliana na magonjwa lakini sisi tutaendelea kusisitiza matumizi ya mbegu za asili ambazo tunazijengea benki yake ambayo tutazihifadhi kwa ajili ya matumizi ya vizazi vijavyo lakini na kwa wakati uliopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kuhusu athari za dawa ambazo zinatokana na kupulizia kwa mfano hayo maembe ya kisasa kwa maana ya matunda ni kwamba tuna kitengo chetu cha TPHPA ambapo ni Mamlaka ya Udhibiti wa Afya za Mimea yenyewe imekuwa ikifanya mapitio na kuangalia kiwango ambacho kinastahili. Kwa sababu duniani tumewekewa viwango ambazo hatutakiwi kuzidi katika matumizi ya kemikali katika matunda ambayo yanatumika. Kwa hiyo, tunazingatia vile viwango vya Kimataifa ili tusiweze kuathiri afya za wanadamu pamoja na ardhi. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa majibu. Mheshimiwa Waziri.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninataka tu niongeze kwenye swali la Mheshimiwa Malembeka kuwa baada ya kuzi - characterize mbegu zetu za asili ambapo tumeshaanza. Bunge hili lilipitisha sheria ambayo msingi wake ninadhani ulikuwa ni development partner Sheria yetu ya Mbegu ambayo ilisukuma ajenda ya industrialization. Tumeanza mchakato wa kubadilisha kanuni, kwa sababu mfumo wetu wa mbegu ulikuwa hautambui mfumo wa kurasimisha mbegu zetu za asili. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumeanza mchakato vilevile wa kikanuni wa kubadilisha kanuni ili mfumo wetu wa kutambua mbegu zetu za asili ili ziingie kwenye maduka, uanze kutekelezwa katika nchi yetu. Kwa hiyo, hatua ya kwanza tumekusanya sampuli zote. Hatua ya pili, TARI wanafanya characterization, kwa sababu jamii zetu zimekuwa zikibadilisha mbegu. Kwa hiyo, tumeanza characterization. Katika process ya characterization tayari mbegu aina 33 zimeshakamilika za mpunga na mahindi ambazo sasa tunaanza mchakato wa kuzitambua rasmi kwenye kanuni zetu na sheria ili ziingie madukani kama mbegu nyingine. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, taasisi zetu zitaanza multiplication ili baada ya mwaka mmoja mkulima aweze kwenda dukani akute traditional seeds, OPV na hybrid ili achague kile ambacho anakitaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viuatilifu, TPHPA tayari imeshatambua aina 45 za Viuatilifu ambavyo tutaziondoa katika list ya viuatilifu vya nchi yetu ambavyo tunaamini kwamba havisaidii na tumeanza kutambua viuatilifu vya asili kuviingiza katika process. (Makofi)
							
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved