Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Anatropia Lwehikila Theonest

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ANATROPIA L. THEONEST aliuliza:- Je, nini haki za Abiria wa vyombo vya moto nchini na kwa kiwango gani wanatambua haki zao?

Supplementary Question 1

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Serikali imekiri dhahiri kwamba abiria hawafahamu haki zao na kwa sababu abiria hawafahamu haki zao, wamekuwa wakiumizwa katika vyombo mbalimbali vya moto ikiwa ni pamoja na kutofika kwa wakati, kutorudishiwa nauli zao pale ambapo vyombo vinapata ajali na kunyanyaswa na wamiliki wa hivyo vifaa vya moto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu la kwanza; ni kwa kiwango gani wananchi wameweza kujua kilo wanazopaswa kubeba kwa maana ya ujazo wa kila daraja wanalolipanda. Kwa mfano, nikipanda basi, ninapaswa kubeba mzigo wa kilogram kadhaa ambayo inaendana sambamba na nauli niliyoiweka tofauti na ilivyo leo, abiria analipa nauli na analipia mzigo ambao upo kwenye ujazo alioulipia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; ukipanda treni ya SGR, moja kati ya kero ya watumiaji wakubwa imekuwa ni suala la wrapping. Imekuwa biashara ya ku-wrap unalazimisha ku-wrap hata mzigo ambao haupaswi ku-wrap bila hata ku-negotiate bei. Ninataka kujua mkakati wa Serikali kuweka mbia wa kushindana katika gharama za wrapping ili kuondoa kero ambazo zimekuwa sugu kwa watumiaji wa hii treni? (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Anatropia kwa maswali yake ya msingi sana kwa maslahi ya watumiaji. Pili, nimhakikishie Serikali itaendelea kutoa elimu hatua kwa hatua kwa watumiaji ili waendelee kufahamu haki zao pamoja na wajibu wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, Bunge hili limepitia Sheria mwaka 1973, Sheria za leseni za usafiri kwa umma na mwaka juzi mwaka 2020 tumepitisha kanuni yaani Kanuni za Leseni za Usafiri wa Umma 2020. Ukisoma katika kanuni hizi, kifungu cha 37(1) na (2), imeainishwa kwa kina juu ya uzito ambao abiria anaruhusiwa mzigo wake uwepo ambapo imeainishwa kwamba ni kilo 20. Pia, ukienda kwenye Tanzania Railway Corporation Passenger Terms and Condition, pia imeainishwa kwa upande wa treni kwamba, kwenye upande wa economy abiria anaruhusiwa kubeba mzigo wa kilo 20 na upande wa business au biashara kilo 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia amezungumzia habari ya wrapping. Tunafanya wrapping pale tunapoona mizigo hiyo haijafugwa vizuri na ambayo inaweza kuwa hatarishi kwa usalama wa abiria wengine. Pamoja na hiyo, tunapokea ushauri wake. Kwanza tutaendelea kutoa elimu, lakini pia kuhusu mbia, tumepokea ushauri kutazama namna gani mbia anaweza akatusaidia kufanya kazi hiyo ya wrapping.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitoe maelekezo kwa Shirika la Reli pamoja na LATRA na taasisi zetu kwamba, tuhakikishe abiria wanatendewa inavyostahili na kuendelea kutoa elimu ili waendelee kunufaika na mifumo yetu ya usalama katika nchi yetu.