Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
											Name
Stella Simon Fiyao
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza kujenga mifumo ya uvunaji maji ya mvua katika shule zote nchini?
Supplementary Question 1
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza niseme wazi, natambua jitihada kubwa ambazo zinafanywa na Serikali kuhakikisha kwamba katika kila shule kunakuwa na maji, lakini bado kuna changamoto kwa baadhi ya shule, mfano ni shule ya sekondari Ileje. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule hii ina wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha sita, imekuwa ikikumbwa na uhaba mkubwa wa maji, changamoto hii inapelekea wanafunzi kwenda kutafuta maji kwenye mito ili kuweza kukidhi mahitaji kwenye shule hii jambo ambalo linahatarisha usalama wa wanafunzi hususani wanafunzi wa kike. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba shule hii inapata maji ya uhakika ili wanafunzi waweze kuepukana na changamoto hii. 
Swali langu namba mbili, ninataka kujua mpango wa Serikali ni upi kuhakikisha mnapeleka fedha katika Shule ya Msingi Ilanga iliyoko Kata ya Mlale, Wilaya ya Ileje, shule ambayo iliezuliwa na mvua na kupelekea majengo matatu tu, kuna madarasa matatu ambayo yanatumiwa na wanafunzi kuanzia darasa la awali mpaka darasa la saba. 
Je, ni lini Serikali mtapeleka fedha ili wanafunzi waendelee kusoma kama walivyokuwa wanasoma hapo awali? (Makofi)
 
											Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
								NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama alivyosema, moja ya mikakati ya Serikali ni kuhakikisha kwamba shule zetu zote zinakuwa na maji safi na salama ili kuwawezesha wanafunzi kuwa na afya njema, lakini pia kusoma katika mazingira tulivu. 
Kwa hiyo, naomba nitumie nafasi hii kumuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, lakini pia Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya wapite katika shule hiyo, wafanye tathmini ya uwezekano wa kupata maji, waangalie uwezekano wa vyanzo vya maji ambavyo vinaweza vikapatikana kwa haraka, pia wawasiliane na Mamlaka za Maji RUWASA katika eneo hilo ili kufanya utaratibu wa haraka wa kupeleka maji katika shule ya sekondari ya Ileje ili watoto wasome katika mazingira bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusiana na madarasa ambayo yameezuliwa, ni wajibu wa halmashauri kwanza kutumia mapato ya ndani kufanya marekebisho madogo madogo kwenye madarasa ili watoto waendelee na masomo, lakini kama fedha hiyo haipo ndani ya uwezo wa halmashauri, namuelekeza Mkurugenzi alete taarifa Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili tuweze kuona namna nzuri ya kupata fedha mapema na kwenda kurekebisha madarasa hayo. (Makofi)
							
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved