Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Primary Question

MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza: - Je, kwa nini Serikali isipeleke ajira kwenye ngazi ya halmashauri ili kuweka uwiano wa nafasi katika kila jimbo?

Supplementary Question 1

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa Mbulu Vijijini kuna zaidi ya nafasi 220 hazina kabisa watumishi na ufanyaji wa kazi umekuwa mgumu. Je, Serikali imejipangaje sasa kusaidia Jimbo la Mbulu na Mbulu Vijijini na Halmashauri ya Mbulu ili kuwa na utendaji mzuri wa kazi ndani ya jimbo hilo? (Makofi)

Swali la pili, natambua majibu yako ya Sera ya mwaka 2008, sasa hivi kuna tatizo kubwa la ajira katika maeneo yetu na hasa vijana wengi wamekuwa wakitafuta hizi ajira na zimeshakuwa kama bomu.

Je, ni mpango gani wa Serikali kutatua eneo hili ili kusaidia vijana wengi kupata ajira kama nilivyouliza? (Makofi)

Name

Deus Clement Sangu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, nimpongeze sana Mheshimiwa Flatei, amekuwa mstari wa mbele kufuatilia sana suala la ajira na watumishi kwa ujumla katika jimbo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikimjibu maswali yake yote mawili kwa ujumla, kwanza naomba Mheshimiwa Flatei, nikuhakikishie Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeonesha mfano dhahiri wa kutoa kipaumbele katika ajira kwa vijana. Kwa mfano, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alitoa kibali cha ajira 47,404. Haitoshi mwaka 2024/2025 alitoa kibali cha ajira 45,000 lakini pia mwaka wa fedha ujao na kwenye bajeti yetu ya Ofisi ya Rais, Utumishi mlitupitishia kibali cha ajira 41,500. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais ameonesha kwa nia ya dhati kwamba anawapenda vijana wa Kitanzania na kwa kadri fedha zinavyopatikana na bajeti amekuwa akitoa tu vibali vya ajira, kwa kweli tumpongeze Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Flatei kuwa katika ajira hizi nilizotaja zote, tayari kuna ikama imepangwa kwa ajili ya watumishi kwenda kwenye jimbo lake. Kwa hiyo kama pia Mkurugenzi alikuwa hajawasilisha maombi kwa mwaka ujao wa fedha aandae maombi na alete Ofisi ya Rais, Utumishi ili tuweze kumpa kipaumbele.