Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
											Name
Priscus Jacob Tarimo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Mjini
Primary Question
MHE. PRISCUS J. TARIMO K.n.y. MHE. JOSEPH A. TADAYO aliuliza:- Je, lini Serikali itakamilisha Miradi ya Maji Kijiji cha Mangio, Mwaniko na Msangeni – Mwanga?
Supplementary Question 1
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa majibu hayo mazuri ya Serikali lakini ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; upatikanaji wa maji katika Mkoa mzima wa Kilimanjaro na maeneo ya Arusha ambayo inajenga ile Pangani River Basin inategemea sana utunzaji wa mazingira. Je, mamlaka zinazozunguka basin hiyo pamoja na Wizara wana mpango gani wa utunzaji wa mazingira? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Mamlaka ya Maji Moshi imewekeza fedha nyingi sana kwa ajili ya majitaka hasa kwenye Kiwanda kile cha Ngozi cha Karanga na kwa wakazi lakini inaonekana yale mabwawa yamefikia limit. Serikali inashirikiana vipi na sisi kuhakikisha kwamba yale mabwawa yanapata fedha kwa ajili ya upanuzi?
 
											Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
								NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na ninapenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa vivutio vya mazingira ni pamoja na uwepo wa vyanzo vya maji ikiwemo chemichemi, maziwa, mabwawa pamoja na mito na ni asilimia kubwa (zaidi ya 80%) ina mchango mkubwa sana kwa maisha ya binadamu, wanyama pamoja na mimea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Sheria yetu Na. 5 ya mwaka 2019 imeipatia majukumu Wizara ya Maji kupitia Bodi za Mabonde ya Mito kuhakikisha kwamba wanashirikiana na wadau kulinda, kutunza, kusimamia na kuhifadhi vyanzo vya maji na kuhakikisha kwamba mazingira yanaendelea kutunzwa. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, sanjari na hilo kupitia Mfuko wetu wa Maji wa Taifa katika kanuni ambazo Mheshimiwa Waziri alizisaini tumetenga 10% katika mapato ya Mfuko wa Maji ili ziende kwa mabonde kwa ajili ya kwenda kuhakikisha kwamba tunasimamia, kulinda na kuhakikisha kwamba mazingira katika maeneo hayo yanakaa vizuri kwa sababu vyanzo vya maji ndio msingi wa maji tunayoyapata. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipengele cha pili tunatambua kwamba Mji wa Moshi unaendelea kuwa msafi na kuendelea kwake kuwa msafi ni kwa sababu ya kazi nzuri sana ya Mheshimiwa Mbunge ambayo anaifanya kwa kushirikiana na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mabwawa pamoja na kile kiwanda ambacho Mheshimiwa Mbunge amesema ili kuendelea kuondosha maji na kuwa sustainable ni lazima tuwe na mabwawa ya uhakika ambayo yataweza kupokea yale maji na sasa yameelekea kufikia ukomo wake. Tayari Mamlaka ya Maji Moshi wameshaandika andiko kwenye Mfuko wa Taifa ili wapatiwe fedha kwa ajili ya kwenda kupanua yale mabwawa ili kuwa na uhakika wa ukusanyaji wa maji taka kutoka katika Mji wa Moshi. (Makofi) 
							
 
											Name
Issaay Zacharia Paulo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Mjini
Primary Question
MHE. PRISCUS J. TARIMO K.n.y. MHE. JOSEPH A. TADAYO aliuliza:- Je, lini Serikali itakamilisha Miradi ya Maji Kijiji cha Mangio, Mwaniko na Msangeni – Mwanga?
Supplementary Question 2
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na tunaishukuru sana Serikali tayari imechimba visima vitano katika Jimbo la Mbulu Mjini na hadi sasa baadhi ya visima vimeanza kutoa huduma kwa wananchi. 
Je, Serikali ina mpango gani sasa wa jumla kitaifa kuendeleza vile visima vitano kwa ajili ya programu ya visima 900 nchini? (Makofi)
 
											Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
								NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba zoezi la kwanza ilikuwa kuchimba na kuangalia wingi wa maji na baada ya hapo tunafanya usanifu ili kuhakikisha kwamba tunatengeneza mtandao wa wananchi kupata huduma ya maji. Pia tunapogundua kwamba maji yale hayatoshi kupelekwa kwa wananchi wengi sana tunatengeneza point source katika eneo lile la kisima ili wananchi angalau waanze kupata maji wakati Serikali ikiwa inatafuta fedha za kufanya usanifu wa kupanua mradi huo ama kutoka katika mradi mwingine ulioko karibu, lengo ni kwamba wananchi wafikiwe na huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe hofu, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga na kwa bajeti ya shilingi trilioni 1.06 hakika tutaenda kuhakikisha kwamba changamoto zote hizo tunazimaliza. (Makofi)
							
 
											Name
Shally Josepha Raymond
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. PRISCUS J. TARIMO K.n.y. MHE. JOSEPH A. TADAYO aliuliza:- Je, lini Serikali itakamilisha Miradi ya Maji Kijiji cha Mangio, Mwaniko na Msangeni – Mwanga?
Supplementary Question 3
MHE. SHALLY J. RAYMOND:  Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na niipongeze Serikali kwa jinsi ambavyo wanakubali na kuhakikisha wanamsikiliza Mheshimiwa Rais kumtua mwanamke ndoo kichwani. 
Kwa kuwa kuzalisha maji safi na salama ni gharama sana, lakini bado upotevu wa maji uko juu; je, ni lini ile programu ya kuelimisha wanawake kuhusu utunzaji wa maji safi na salama hayo itaanza hususan mkoani Kilimanjaro? (Makofi)
 
											Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
								NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ninapenda sana kupokea kwanza ushauri wa mama yangu Mheshimiwa Shally Raymond ambapo kwa kweli amekuwa akilipigia chapuo sana hili suala la kuwaelimisha kwa sababu suala la maji kwanza kuwa na elimu ili tuweze kutunza vyanzo na miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa sana Serikali inaendelea kupokea ushauri kutoka kwa wadau akiwepo Mheshimiwa Mbunge. Tutalifanyia kazi na pale fedha zitakapopatikana tutaanza programu hiyo mara moja ili wakina mama wapate elimu hiyo stahiki. (Makofi)
							
 
											Name
Nicodemas Henry Maganga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbogwe
Primary Question
MHE. PRISCUS J. TARIMO K.n.y. MHE. JOSEPH A. TADAYO aliuliza:- Je, lini Serikali itakamilisha Miradi ya Maji Kijiji cha Mangio, Mwaniko na Msangeni – Mwanga?
Supplementary Question 4
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninakushukuru kwa kuniona, lakini ninakushukuru pia kwa maelekezo yako. Ninaenda moja kwa moja kwenye swali kwa ufupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mheshimiwa Waziri, visima vitano tumechimba mwaka 2024, lakini Mji wa Mbogwe yaani watu wa Mbongwe, hayo maji hayatoshi. Lini Mradi wa Maji mkubwa wa Ziwa Victoria utaanza kutekelezwa, kupelekwa Mbogwe pamoja na Bukombe? 
 
											Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
								NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napokea shukrani za Mheshimiwa Mbunge wa Mbogwe kwa kutambua mchango mkubwa wa Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumchimbia visima vitano na yeye amekiri kabisa kwamba vimekamilika. Suala la maji kutoka Ziwa Victoria ni ndoto ya Watanzania wengi, kutumia maji ya Ziwa Victoria, lakini ndoto hii inakamilishwa na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, zoezi la kufikisha maji Mbogwe linatanguliwa na usanifu wa mradi. Utakapokamilika basi zoezi la ujenzi wa mradi kuja Mbogwe utafanyika bila kuwa na taswishwi yoyote. Ahsante sana.
							
 
											Name
Oliver Daniel Semuguruka
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. PRISCUS J. TARIMO K.n.y. MHE. JOSEPH A. TADAYO aliuliza:- Je, lini Serikali itakamilisha Miradi ya Maji Kijiji cha Mangio, Mwaniko na Msangeni – Mwanga?
Supplementary Question 5
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Je, lini mradi wa maji kutoka Kanazi, Kemondo, utafika Vijiji vya Muhutwe na Mayonde, Jimbo la Muleba Kaskazini, kwa Mheshimiwa Mwijage?
 
											Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana dada yangu Mheshimiwa Oliver. Ninafahamu anavyoendelea kuwapigania wananchi wa Kagera kwa ujumla akiwa mwakilishi wa akinamama mashuhuri kabisa, lakini pia ninaomba nilipokee hili, ili nimpatie taarifa stahiki ambazo zinaendana na uhalisia uliopo kule. Ahsante sana.
 
											Name
Anatropia Lwehikila Theonest
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. PRISCUS J. TARIMO K.n.y. MHE. JOSEPH A. TADAYO aliuliza:- Je, lini Serikali itakamilisha Miradi ya Maji Kijiji cha Mangio, Mwaniko na Msangeni – Mwanga?
Supplementary Question 6
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukru sana. Takwimu zinaonesha kwa mwaka 2024 mikoa yote Tanzania Bara, kuondoa miwili ya Kilimanjaro na Iringa, wamepata kipindupindu na tunajua sababu za kipindupindu ni pamoja na kunywa maji machafu. Sasa pamoja na uchimbaji wa mabwawa, kwa maana ya kupata maji, je, ni mkakati gani wa Serikali kuhakikisha inaweka water purifiers, ili kuondoa changamoto ya kipindupindu ambayo imekuwa inajitokeza na kujirudia miaka yote?
 
											Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
								NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kipindupindu; kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuliongelea hili kwa sababu linalenga moja kwa moja kwenye afya za watoto, akinamama na wakazi wote wa nchi hii, lakini suala la kipindupindu ni jambo mtambuka ambalo linagusa sekta mbalimbali. Sisi kama Serikali, tutaendelea kushirikiana na wadau wote wanaoguswa na jambo hili, ili tuwe na mkakati wa pamoja. Lengo ni wananchi wetu tuhakikishe kwamba hawapatwi na magonjwa kama haya. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sisi Wizara ya Maji tunaendelea kusisitiza kuhakikisha kwamba maji yetu yanatibiwa ili yawafikie yakiwa ni salama na ni safi. Lengo ni kwamba mpaka sasa tumeshafikia 80% ya kufikisha huduma ya maji safi na salama kwa wananchi vijijini na 91% kwa upande wa mjini. Kwa hiyo, hiyo ni sehemu mojawapo ya mkakati wa Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha kwamba wananchi hawapati magonjwa ambayo yanatokana na kunywa maji machafu. Ahsante sana. 
							
 
											Name
Regina Ndege Qwaray
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. PRISCUS J. TARIMO K.n.y. MHE. JOSEPH A. TADAYO aliuliza:- Je, lini Serikali itakamilisha Miradi ya Maji Kijiji cha Mangio, Mwaniko na Msangeni – Mwanga?
Supplementary Question 7
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na niishukuru kwanza Serikali kwa kutukamilishia mradi wa visima katika Kijiji cha Riroda na Hewasi na tayari mabomba yameshaanza kusambazwa. 
Je, ni lini sasa mradi huu utakamilika, ili wananchi waweze kupata huduma ya maji?
 
											Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
								NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge, ameuliza hili swali mara kadhaa na leo hii ninafurahi na yeye amekiri kwamba tayari mabomba yamesambazwa. Ninaamini kabisa kwamba utaratibu wa ukamilishaji wa mradi huu upo ndani ya utaratibu wa mkataba ambao tumesaini na mkandarasi. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Mheshimiwa Mbunge awe mvumilivu, mradi huu utakamilika kwa wakati. Ahsante sana.
							
 
											Name
Boniphace Mwita Getere
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Primary Question
MHE. PRISCUS J. TARIMO K.n.y. MHE. JOSEPH A. TADAYO aliuliza:- Je, lini Serikali itakamilisha Miradi ya Maji Kijiji cha Mangio, Mwaniko na Msangeni – Mwanga?
Supplementary Question 8
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushuru sana na ninaishukuru Wizara ya Maji walipeleka shilingi milioni 830 katika Kijiji cha Unyali, lakini wiki mbili zilizopita niliuliza swali hili wakaniambia kwamba hela shilingi milioni 180 itaenda kumalizia huu mradi. Sasa ni lini hiyo hela itafika kwa sababu sasa wiki mbili zimepita?
 
											Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Getere na naomba nirejee, sikusema zitapelekwa, nilisema zimeshapelekwa na tayari zipo zinafanya kazi na ndivyo ambavyo nilijibu siku ile. Ahsante sana.
 
											Name
Hawa Subira Mwaifunga
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. PRISCUS J. TARIMO K.n.y. MHE. JOSEPH A. TADAYO aliuliza:- Je, lini Serikali itakamilisha Miradi ya Maji Kijiji cha Mangio, Mwaniko na Msangeni – Mwanga?
Supplementary Question 9
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nini mkakati wa Wizara kuhakikisha wanachimba visima kwenye vituo vya afya ambapo wamekuwa na madeni makubwa ya maji kutokana na kwamba hawana uwezo wa kulipa maji kwa wakati na badala yake wawe na visima?
 
											Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
								NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hawa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu analenga hospitali gani na vituo vya afya katika Mkoa wa Tabora. Hakika tunajua kabisa kwamba lengo lake ni kuhakikisha kwamba hatupati changamoto katika vituo vyetu vya afya kwa kukosa maji kwa sababu ya bili. Tunatambua kwamba sasa tumeshaweka mkakati, tunapofanya usanifu tunafikiria pia taasisi za Serikali, shule, vituo vya afya na zahanati, usanifu wetu uhakikishe kwamba unajumuisha taasisi hizi ili maji yanapohitajika yasiwe na changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tuna mkakati wa pamoja kuhakikisha kwamba vituo vya afya havikosi maji na hata shule ambapo watoto wetu wanasoma, hawakosi maji. Ninakushukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuendelea kukumbusha hili na Serikali tutaendelea. Ahsante sana.