Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
											Name
Condester Michael Sichalwe
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Momba
Primary Question
MHE. CONDESTER M. SICHALWE Aliuliza: - Je, lini Serikali itavitambua vivutio vilivyopo Jimbo la Momba kama vile Nyayo za Mtu wa Kale, Nkanyama, Maporomoko ya Mfuso na Yala (Mpona)?
Supplementary Question 1
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru tena kwa nafasi. Naomba nipongeze majibu mazuri ya Serikali. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio makubwa ambayo yapo kwenye sekta hii ya utalii, lakini miongoni mwa changamoto kubwa ambayo inaikumba sekta yetu ya utalii hapa nchini ni watalii wanapokuja, wakitazama vile vivutio hawawezi kurudi tena kwenye nchi yetu, kwa ajili ya kutazama vivutio vingine maana vivutio vilivyopo ni vilevile. 
Swali langu, Serikali inaonaje kuongeza wigo mpana na kuweka vivutio vingi ili mtalii huyu anapokuja hapa nchini, akitembelea mbuga za wanyama, akienda sijui kwenye vitu gani, akutane na utalii wa chakula, simulizi za watu wa kale na mambo mbalimbali ili apate orodha ya vitu vingi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; inaonekana kwamba utalii unafanya vizuri Kaskazini tu, Arusha labda na Kilimanjaro na kwa mikoa michache kama Morogoro pale Mikumi na Iringa kwa sababu ya Ruaha, lakini mikoa mingine imeachwa nyuma. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatolea mfano, kule Zambia kuna maporomoko ya Victoria Falls; mtalii huyu inabidi anapotoka Arusha anaenda Morogoro, afike Iringa atembee na gari, afike labda Uyole pale akutane na mila za Wasafwa, aende Songwe akutane na mila za Wandali na Wanyamwanga, aende na gari mpaka kufika Zambia, lakini arudi kwenda Dar es Salaam kupanda ndege na kuondoka, hivi tunapoteza mapato hapa katikati. 
Je, ni mkakati upi wa Serikali kuongeza vivutio vingi, lakini kutokuweka matabaka kwenye mikoa kadhaa kwa sababu tuna vivutio vingi nchini kote? Ahsante. 
 
											Name
Dunstan Luka Kitandula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Answer
								NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: - 
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, zipo hisia kwamba utalii wetu umejikita zaidi kwenye utalii wa wanyamapori, 80% ya utalii wetu umejifunga hapo. Kwa hiyo, kama Wizara tumeweka mkakati sasa wa kuibua aina nyingine za utalii na kuwa na vivutio mchanganyiko ili kuhakikisha kwamba utalii usijikite tu kwenye wanyamapori, lakini uende kwenye maeneo mengine. Kama ambavyo wengi wenu mnafahamu, mwezi uliopita tu Mei, Tanzania ilipata heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa wa pili wa utalii wa vyakula katika Ukanda wa Afrika, hizi ni miongoni mwa jitihada tunazofanya kuhakikisha tunakuwa na utalii wa aina tofauti tofauti. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kule kwenye Ukanda wa Bahari tuna utalii mwingine wa kutumia meli zinazoleta watalii kwenda kwenye maeneo ya fukwe kuangalia maeneo yetu ya magofu na vitu kama hivyo. Kwa hiyo, jitihada zimeanza za kuhakikisha kwamba tunafungua uwanja mpana wa kuwa na vivutio mchanganyiko ili watalii waweze kukaa kwa muda mrefu na vilevile wavutike kurudi kutembelea nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili eneo ambalo tunasema mikoa mingine ni kama imefungwa hivi, haipati watalii wa kutosha, ni kweli Serikali imeliona hilo na ndiyo maana tumekuja na mkakati mkubwa sana wa kufungua mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambako uwekezaji mkubwa umefanyika na Serikali kuhakikisha tunafungua ukanda ule.
 Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile jitihada hizi zinazofanywa na Wizara ya kwenda kwenye mikoa yetu na kutambua vivutio vilivyopo kwenye maeneo hayo ili na vyenyewe viweze kuendelezwa na kufungua fursa za utalii mpana kwa nchi yetu. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeona changamoto hizi na zinafanyiwa kazi. 
							
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved