Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
											Name
Latifa Khamis Juwakali
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza:- Je, kuna mkakati gani wa kuwalinda Wanafunzi Shuleni?
Supplementary Question 1
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, kwanza ninaipongeza Serikali kwa jitihada mbalimbali ambazo wanazichukua. Hata hivyo, nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kumekuwa na changamoto hasa kwa wanafunzi wetu wa msingi ambao wanapanda kwenye school bus. Unaweza ukakuta mwanafunzi anaweza kufika mwaka mzima hajawahi kukaa kwenye seat.  Je, Serikali hawaoni kuwa sasa kuna haja ya kuandaa au kutoa kauli maalum kwa skuli zetu ambazo zinatumia school bus ili kuona sasa kuwa wanaweza kuwasaidia kwa kuweka matron na patron katika school bus?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; pamoja na jitihada hizo zinazochukuliwa bado mmomonyoko wa maadili umeendelea kuwa changamoto katika skuli zetu.  Je, Serikali haioni sasa kuweka nguvu maalum kwa kuwaandaa walimu maalum wa maadili katika skuli zetu nchi nzima?
 
											Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
								NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kwanza kwa kumpongeza Mbunge wa Vijana Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali kwa swali lake ambalo linalenga kuendelea kutengeneza mazingira salama zaidi kwa ajili ya wananfunzi wetu na hasa kipindi wanapokuwa wanaelekea shuleni, vilevile hata wanapokuwa nyumbani, kwa kuwa usalama wa wanafunzi ni kuanzia nyumbani, njiani hadi shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kwanza, tayari Serikali imekwishaweka utaratibu mzuri na maelekezo yalikwishatoka, kwamba kuwe kuna patron na matron kwenye mabasi yanayowapeleka watoto shuleni. Yote hiyo ni njia mojawapo ya kuhakikisha watoto wetu wanakuwa katika mazingira ya usalama kuanzia nyumbani, wanapokuwa njiani na pia wanapokuwa shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili linalohusu walimu maalum kabisa wa maadili; kama nilivyotangulia kujibu kwenye jibu la msingi, Serikali inaendelea kuongeza mafunzo kwa wadau muhimu ikiwemo walimu. Katika mwaka wa fedha 2024/2025 yameendeshwa mafunzo kwa walimu 7,451 kwa ajili ya ushauri na unasihi; Wakuu wa Shule za Msingi 17,817; Maafisa Maendeleo ya Jamii ngazi ya kata 900; Wenyeviti wa Kamati za Shule 1,980; na Wenyeviti wa Bodi za Shule 580.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, si tu walimu wanaoandaliwa kwa ajili ya kusimamia maadili na usalama wa wanafunzi wanapokuwepo mashuleni bali pia kuna wadau wengine ambao nao wanajengewa uwezo ili kuhakikisha kwamba wanafunzi wetu wanakuwa salama. 
							
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved