Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Michael Constantino Mwakamo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Primary Question

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:- Je, Serikali haioni ni muda muafaka kuchimba visima vya maji kwenye Taasisi za Umma kama shule, zahanati na hospitali zote nchini?

Supplementary Question 1

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru Serikali kwa majibu mazuri yanayoleta faraja ya upatikanaji wa maji kwenye hizi huduma, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza; sote tunafahamu kwamba utunzaji wa mazingira ya maeneo ya shule yanahitaji maji mengi na tunafahamu kwamba maji mengi ambayo yanatumika walimu wanashindwa kuwaruhusu watoto kuyatumia vizuri kutokana na gharama kubwa ya ulipaji wa maji hayo. Je, ni kwa nini sasa Serikali kutokana na uwepo wa mitambo ya uchimbaji wa visima isichimbe visima kwenye taasisi hizo ili kupunguza gharama za ulipaji wa bili kwenye taasisi zinazotoa maji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; utoaji wa elimu pia unatolewa na sekta zisizo za Kiserikali, kwa mfano kuna shule za binafsi na wao pia ni sehemu kubwa ya wanaosaidia upatikanaji wa elimu nchini na shule zao pia zina changamoto au zahanati zao zina changamoto ya huduma ya maji. Je, Serikali inaweza ikafanya mawasiliano na wawekezaji hao ili kuwasaidia kutumia mitambo ya Serikali kuweza kupata huduma ya maji kwa urahisi kwa sababu wanatoa huduma kwa wananchi? (Makofi)

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninamshukuru sana kaka yangu Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaendelea kuifanya kwa niaba ya wananchi wake wa Kibaha Vijijini. Kwenye swali la pili, Serikali iko tayari kufanya kazi na wadau wote ambao wana nia njema kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunaboresha utoaji wa huduma ya maji nchini ikiwemo katika taasisi ambazo Mheshimiwa Mbunge amezisema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa swali la kwanza, ni kweli kabisa gharama ya kuhudumia na hizi fedha ambazo wanazipata shuleni inawezekana hazitoshi kuhudumia gharama ya kulipa maji endapo wanafikishiwa zile bili. Sisi kama Serikali tumeshaliona hilo lakini pia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tunaendelea kuangalia njia bora zaidi ya kutatua changamoto hii kwa sababu kuna maerneo mengine ya shuleni hata kama tuna mitambo ya kuchimbia visima maeneo hayo katika maeneo husika hakuna maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba ni lazima tuchimbe maeneo mengine halafu yasukumwe yapelekwe pale. Yakishapelekwa katika eneo husika maana yake kuna gharama za umeme ambazo zitakuwa zimetumika ambapo kwa namna moja au nyingine uchangiaji tu lazima utakuwepo. Hata hivyo, kwa maeno ambayo hakuna changamoto ya upatikanaji wa maji Serikali imeendelea kutumia mitambo ya Mheshimiwa Rais ambapo alinunua mitambo 25 kuhakikisha kwamba tunaendelea kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika taasisi za umma, shule pamoja na vituo vya afya. Ahsante sana.

Name

Robert Chacha Maboto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda Mjini

Primary Question

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:- Je, Serikali haioni ni muda muafaka kuchimba visima vya maji kwenye Taasisi za Umma kama shule, zahanati na hospitali zote nchini?

Supplementary Question 2

MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Bunda Mjini, Kata ya Wariku Mradi wa Maji uko 40%. Je, ni lini Serikali itatoa fedha ili mradi huu uweze kukamilishwa uweze kutatua tatizo la changamoto za maji katika kata hiyo? Ninakushukuru.

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Maboto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshawasiliana na Mheshimiwa Mbunge na jana tuliongelea kuhusu hili suala na kuna MD wetu kutoka kule Bunda pia ameliongelea. Ni kweli kabisa kulikuwa na changamoto ya fedha zilikuwa hazijafika, lakini tayari tumeshawasilisha hati ya madai Wizara ya Fedha ili waweze kulipwa na tayari mchakato uko katika hatua nzuri kabisa na mradi huu ni mradi wa kimkakati katika eneo hilo la Bunda na katika kata ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja na amekuwa akiongelea sana kuhusu hili suala na sisi tumejizatiti kwenda kutatua ili mradi huu ukamilike na wapate huduma ya maji safi na salama. Ahsante.

Name

Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:- Je, Serikali haioni ni muda muafaka kuchimba visima vya maji kwenye Taasisi za Umma kama shule, zahanati na hospitali zote nchini?

Supplementary Question 3

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Katika Kata ya Mbulumbulu Serikali iliahidi kuchimba visima vinne vya maji, lakini mpaka sasa tunapoongea ni angalau kijiji kimoja tu wameanza kuchimba. Vijiji vingine vyote zoezi hilo haliendelei. Nini kauli ya Serikali?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana, pia ninamshukuru Dada yangu, Mheshimiwa Paresso kwa kuendelea kuwasemea wananchi wa Karatu na hakika kweli tunaelewa kwamba dhamira ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi na falsafa ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani ninamwona Mheshimiwa Mbunge pia anaendelea kuiishi kwa vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali, kwenye sekta ya maji tunatambua kabisa kwamba katika programu ya visima 900 kuna maeneo ambapo tulikumbana na changamoto ya kutokupatikana kwa maji, lakini tumekuwa tukitafuta njia mbadala badala ya kuchimba kisima tunaweza tukatafuta mradi ulioko karibu tunafanya usanifu, tunaangalia namna ya kuyafikisha maji katika vijiji husika ambavyo havijapata maji chini ya ardhi. Nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge vijiji hivyo tutavizingatia, lengo ni kwamba wapate huduma ya majisafi na salama. Ahsante sana.

Name

Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Primary Question

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:- Je, Serikali haioni ni muda muafaka kuchimba visima vya maji kwenye Taasisi za Umma kama shule, zahanati na hospitali zote nchini?

Supplementary Question 4

MHE. FESTO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninasimama kwa mara ya saba nikiuliza kuhusu Mradi wa Mfumbi kwa maana ya Usalimwani Mfumbi zaidi ya shule tano za msingi na sekondari ziko pale na hazina maji. Vijiji vitano havina maji na mradi huu walianza kujenga lakini umesimama hadi dakika hii. Ipi kauli ya Wizara kwenye hili suala ili iweze kutoa fedha mradi ukatekelezwe?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa kaka yangu Sanga, Mbunge mahiri kabisa kutoka Makete pale. Nimhakikishie kwa namna ambavyo amesimama kwa mara ya saba kwa msisitizo huo huo ninaomba nikitoka hapa niende nikalifanyie kazi kwa uzito stahiki kwa ajili ya wananchi wake wa Makete kwa sababu lengo la Serikali siyo kukwamisha miradi, lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba miradi yote inakamilika na iweze kutoa matokeo yaliyotarajiwa. Kama Mbunge alivyowasilisha sisi tunachukua kwa namna hiyo. Baada ya hapo nitampa mrejesho kwa niaba ya wananchi wake. Ahsante sana. (Makofi)

Name

Vita Rashid Kawawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Primary Question

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:- Je, Serikali haioni ni muda muafaka kuchimba visima vya maji kwenye Taasisi za Umma kama shule, zahanati na hospitali zote nchini?

Supplementary Question 5

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Namtumbo tuna Mradi wa Kumbara – Litola, mradi mkubwa ambao sasa umefanikiwa na maji yanatoka na umedhihirisha una maji mengi sana mradi huo, lakini tuna Kata jirani ya Namabengo ambayo ina shule ya kutoka kidato cha kwanza mpaka cha sita ambapo pia kuna shida sana ya maji. Iko kilometa sita kutoka mwisho wa mradi huo. Je, Serikali inaweza ikafanya usanifu na ikajenga tenki kubwa na kutandaza mabomba ikapeleka katika Kata hiyo ya Namabengo ili waweze kupata maji ambayo wana shida ya maji pia eneo hilo? (Makofi)

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni habari njema sana. Tunapokuwa na chanzo cha uhakika na tunakuwa na kiu ya kutosha ya maji, sisi kama Serikali ni kuhakikisha kwamba maeneo husika yanayozunguka hicho chanzo cha maji wanapata maji ya uhakika. Serikali iko tayari kufanya usanifu kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameshauri ili kata jirani waweze kupata huduma hiyo ambayo ni msingi wa uhai wa binadamu. Ahsante sana. (Makofi)