Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
											Name
Hawa Mchafu Chakoma
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:- Je, lini Uwanja wa Ndege Mafia utaboreshwa ili ndege kubwa ziweze kutua?
Supplementary Question 1
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, David Kihenzile nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kufuatia changamoto za usafirishaji na ukuaji wa uchumi katika maeneo ya ukanda wa bahari ikiwemo Mafia, Bagamoyo, Kibiti na Mkuranga, ni upi sasa mkakati wa Serikali kuhakikisha inaboresha bandari za maeneo hayo na kujenga meli zake? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; nipende sana kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea na mkakati wa kujenga miradi mikubwa ya kimkakati. Swali langu ninataka kujua, ni upi mpango wa Serikali kuhakikisha vijana wanaopata ajira zile ambazo zisizo na ujuzi (unskilled labour) kutoka katika maeneo hayo ya miradi kwamba wanazingatiwa vijana kutoka katika maeneo hayo yenye miradi husika? Ahsante.
 
											Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
								NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitumie nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma kwa jinsi ambavyo amekuwa mfuatiliaji wa miradi mikubwa na hata ya kawaida katika Mkoa wa Pwani ikiwemo ya sekta yetu ya uchukuzi hususan pale Mafia, bandari na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, nimhakikishie Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma kwamba Serikali imeamua kuifanya sekta ya uchukuzi kama mishipa kwa kuitambua kwamba ni mishipa ya damu katika Taifa letu. Hivyo basi, inafanya maboresho ya bandari mbalimbali nchi nzima pamoja na kujenga meli katika maziwa makuu yote na sasa ninapozungumza kwa upande wa swali lake la msingi Bandari za Mafia, Mkuranga pamoja na Bagamoyo ya zamani, tayari tumeshapewa idhini na Serikali kupitia Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hivyo, tunaweka kwenye mpango wa mwaka wa fedha 2025/2026 tuanze maandalizi ya kuzijenga bandari hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inakwenda sambamba na kuanza kujenga meli. Tarehe 8 Machi TASHICO (Kampuni yetu ya Meli Tanzania) ilisaini mkataba wa kuanza usanifu wa kina kwa ajili ya kutazama fursa zilizopo katika mwambao wa Bahari ya Hindi. Lengo ni nini? Ni kutazama biashara iliyopo. Tunao mpango kama Serikali kuona kwamba tunaimarisha usafiri wa nchi jirani kama vile Visiwa Comoro, Madagascar, Shelisheli pamoja na maeneo kama vile Mtwara, Tanga, Lindi na kadhalika. Hivyo, tutakapokamilisha usanifu huo tutakwenda hatua ya pili ya kuanza kujenga meli hizo kulingana na mahitaji na kujua fursa ambazo ziko pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameuliza kuhusiana na vijana waliopo katika maeneo hayo wapewe kipaumbele. Kwanza, swali hili limekuwa likiulizwa sana hapa Bungeni. Ninapenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba nchi hii ni yetu sote. Ni haki ya kila Mtanzania kuajiriwa mahali popote bila kujali kuna mradi au hakuna mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazingatia pia kwamba, kodi zinazojenga miradi hiyo ni kwa Watanzania wote. Aliyekuwepo Iringa analipa kodi katika mradi uliokuwepo mkoa mwingine. Hivyo basi, ninapenda kuwataarifu Waheshimiwa Wabunge kwamba tuendelee kutoa fursa kwa vijana wetu nchi nzima wafanye kazi popote. Aidha, tukubaliane pia yako maeneo ambayo vijana hawapendelei sana kufanya kazi zile ambazo ni unskilled. Hivyo, hata mjenzi angependa kwenda kutafuta sehemu ambapo vijana wako tayari kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijahitimisha nitoe rai pia kwa kutambua umuhimu kwamba mradi unapotekelezwa kwenye eneo fulani ni vyema vijana wa eneo wakapewa kipaumbele zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaagiza wakandarasi waliopo kwenye sekta yetu ya uchukuzi watazame pamoja na kuchukua maeneo nchi nzima ya nchi hii lakini pia watazame katika eneo mradi uliopo ili wapewe kipaumbele vijana wa eneo hilo.
							
 
											Name
Maimuna Ahmad Pathan
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:- Je, lini Uwanja wa Ndege Mafia utaboreshwa ili ndege kubwa ziweze kutua?
Supplementary Question 2
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali itaboresha Uwanja wa Ndege wa Kilwa na Nachingwea, ukizingatia kwamba Uwanja wa Ndege wa Nachingwea umetumika sana katika ukombozi wa Bara la Afrika? Ahsante. (Makofi)
 
											Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Pathan kwa swali lake la nyongeza. Serikali inao mpango wa kuboresha viwanja vyote katika nchi hii na katika viwanja alivyovitaja kwa sasa hivi tupo kwenye hatua za awali kwa ajili ya kulipa fidia. Tukimaliza fidia pamoja na kutwaa maeneo tutakwenda kwenye hatua ya pili kwa ajili ya kuviendeleza.
 
											Name
Suma Ikenda Fyandomo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:- Je, lini Uwanja wa Ndege Mafia utaboreshwa ili ndege kubwa ziweze kutua?
Supplementary Question 3
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Je, ni lini safari za ndege za kutoka Dodoma kwenda Mbeya zitaanza, ukizingatia Mbeya kuna abiria wengi sana? Unapokwenda Mbeya mpaka uende Dar es Salaam ndiyo uende Mbeya.
 
											Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
								NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza dada yangu Mheshimiwa Suma Fyandomo kwa swali lake aliloliuliza la kufuatilia safari za ndege Mkoani Mbeya. Ni kweli Mkoani Mbeya kuna abiria wengi na ndege hazitoshi, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Suma kwamba siyo Mbeya tu, kutokana na kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameifanya ya kujenga viwanja vingi mahitaji ya ndege yameongezeka zaidi. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tungesema kila Mbunge asimame karibu Wabunge zaidi ya 20 wangeweza kusimama ili tuongeze ndege kwenye maneo yao. Hata hivyo, kutokana na umuhimu huo mkubwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali imepanga kununua ndege nyingine mpya za masafa marefu na mafupi pamoja na ndege ya mizigo. Tunategemea kwamba kadiri muda utakavyozidi kuongezeka ndivyo tutaendelea kuboresha na kupeleka ndege kwenye maeneo mbalimbali ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine kabla sijamaliza kujibu swali lake ninapenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba viko viwanja hivi ninavyoongea zaidi ya vitano ambavyo vinafanyiwa maboresho vikikamilika navyo vitahitaji ndege. Kwa hiyo, Mheshimiwa Suma na Wabunge wote waendelee kutuvumilia wakati Serikali inaendelea kutafuta suluhu ya kudumu ya jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mwisho niziombe sekta binafsi kwa maana private operators wa hizi ndege watazame fursa zilizopo Mkoani Mbeya na maeneo mengine kwa sababu siyo lazima kupeleka ndege za Serikali. Tunazo kampuni nyingi, hebu zichangamkie fursa hiyo.
							
 
											Name
Esther Nicholus Matiko
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:- Je, lini Uwanja wa Ndege Mafia utaboreshwa ili ndege kubwa ziweze kutua?
Supplementary Question 4
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbuga ya Serengeti ni kati ya mbuga kubwa na maarufu kwa Afrika ambapo watalii mbalimbali kutoka duniani hupenda kutembelea lakini kwa sasa hivi the only entry point its either watue Kilimanjaro au Arusha ndio waweze kuja Serengeti au watue Kenya waweze kupitia Tarime na kwenda Serengeti kitu ambacho kinakuwa kinawa-discourage at a time. Nikataka kujua ni lini Uwanja wa Serengeti utaanza kujengwa ili sasa watalii hawa waweze kuja moja kwa moja na kuongeza uchumi wa nchi yetu? Ahsante sana. (Makofi)
 
											Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Matiko kwa hoja yake ya Serengeti. Hata wiki iliyopita nilikuwa ninazungumza na viongozi wa CCM wa Mkoa wa Mara, kilio chao kikubwa ni hichohicho. Ninapenda kumhakikishia Mheshimiwa Matiko kwamba Serikali inao mpango wa dhati na imeshaweka kwenye Bajeti ya 2025/2026 kuanza mchakato wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege Serengeti.
 
											Name
Shally Josepha Raymond
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:- Je, lini Uwanja wa Ndege Mafia utaboreshwa ili ndege kubwa ziweze kutua?
Supplementary Question 5
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Uwanja wa Moshi utakamilika? Ahsante sana.
 
											Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Uwanja wa Moshi tunaufahamu ni uwanja wa kihistoria katika Taifa letu. Serikali kwa kutambua umuhimu huo mkubwa ilishaanza ujenzi na hivi ninavyozungumza iko zaidi ya 50%. Nimwombe Mheshimiwa Shally Raymond atupe muda kidogo wakati tunaendelea kufuatilia taratibu za malipo zikamilike ili mkandarasi aendelee kulipwa na hatimaye aweze kukabidhi uwanja.
 
											Name
Subira Khamis Mgalu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:- Je, lini Uwanja wa Ndege Mafia utaboreshwa ili ndege kubwa ziweze kutua?
Supplementary Question 6
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Serikali imerejea mpango wake wa ujenzi wa Bandari Bagamoyo na kwa kuwa wapo wananchi ambao waliahidiwa ardhi katika Kata ya Zinga; na kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri aliwahi kujibu na kukubali ombi langu la kutembelea Kata ya Zinga ili awasikilize wananchi wa maeneo yale hususan wa Mlingotini. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kutekeleza ahadi yake ili awasikilize wale wananchi ambao waliahidiwa kupata ardhi mbadala kwa ajili ya eneo ambalo limetengwa kujengwa Bandari ya Bagamoyo?
 
											Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niko tayari na Mheshimiwa Mbunge dada yangu Mheshimiwa Subira Mgalu, baada ya kutoka hapa tupange ziara twende Lindi tukazungumze na wananchi hao ili kuwaelewesha umuhimu na mawanda mapana ya Bandari yetu ya Bagamoyo Mbegani. Kwa sababu Taifa tayari sasa limeshaona fursa hiyo na tuko tayari kwa ajili ya kuanza uendelezaji wake.