Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph Zacharius Kamonga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Primary Question

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanzisha Kituo cha Meli katika Vijiji vya Nsele na Lifuma ili kuwaondolea adha ya usafiri wananchi wa maeneo hayo?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; tulikwenda pale Itungi na Mheshimiwa Naibu Waziri tukaiona ile Meli ya MV-Songea bado iko vizuri sana. Je, lini Serikali itatoa fedha ili meli ile ikarabatiwe na kuweza kusaidia usafiri wa wananchi wa Ziwa Nyasa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; wananchi wa Ziwa Nyasa, Ludewa ina kata nane wanatumia usafiri wa maboti ambayo mengine hayana usalama kwa sababu ratiba ya meli ni mara moja kwa mwezi. Je, nini maelekezo ya Serikali ili kusaidia wananchi wale waweze kusafiri kwa usalama mkubwa ndani ya Ziwa Nyasa?

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Kamonga kwa ufuatiliaji wake mkubwa wa usafiri katika Ziwa Nyasa. Ni kweli mimi na yeye tulikwenda pamoja na Wabunge wengine ambao wanapakana na Ziwa Nyasa tulifanya ziara katika Ziwa hilo tukatambua fursa zilizopo na changamoto ambazo zinawakumba wananchi hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa mambo ambayo Waheshimiwa Wabunge waliishauri Serikali ikiwa ni kutimiza jukumu lao la msingi la kuishauri na kuisimamia Serikali, ilikuwa ni kuomba Meli ya MV Songea irejeshwe kwa sababu ni mbovu na imesimama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusikia kilio chao Serikali makini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, ilifanya maamuzi katika mwaka wa fedha 2025/2026 wa kurejesha meli hiyo. Tumetenga bilioni 4.0 na katika mwaka wa fedha 2025/2026 tunakwenda kukarabati meli hiyo kwa sababu kwanza, ilivyotengenezwa inaendana na hali halisi ya Ziwa Nyasa kwa sababu inaweza kustahimili mawimbi pia inatumia mafuta kidogo na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, amezungumza kuhusu ratiba. Kwanza, nimpe pole kwa sababu kuna changamoto pale Kyela ya mafuriko na hivi navyozungumza tunapata changamoto kubwa ya kupata vitendea kazi kama mafuta na vitu vingine. Hivyo, usafiri ni kama vile umesitishwa. Lakini mara baada ya hali itakapotengemaa naielekeza Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) irejeshe ratiba zake angalau mara mbili badala ya kufanya mara moja kwa mwezi.