Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
											Name
Jonas Van Zeeland
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mvomero
Primary Question
MHE. JONAS V. ZEELAND aliuliza: - Je, kuna mpango gani wa kujenga shule ya sekondari Kata ya Kikeo – Mvomero?
Supplementary Question 1
MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tumekuwa tukishuhudia baadhi ya miradi fedha zinaingia halafu zinachukua muda mrefu kuanza kazi kwa sababu ya kukosa eneo. Je, Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka kutoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji ashirikiane na viongozi wa Kata ya Kikeo akiwemo Mheshimiwa Diwani na timu yake, waandae kabisa eneo ili fedha zitakapokuja ziweze kuanza kazi mara moja?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kata ya Mlali ina vijiji nane na sekondari moja ya kata na kuna msongamano mkubwa sana wa wanafunzi. Je, Serikali haioni kuwa kuna haja ya kuongeza Sekondari ya pili, ili kupunguza msongamano huo wa wanafunzi na watoto kutembea umbali mrefu? 
 
											Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
								NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Jonas Van Zeeland kwa swali lake zuri kabisa, na kwa hakika amekuwa akifanya ufuatiliaji mkubwa sana wa kuhakikisha maendeleo yanapatikana katika jimbo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la kwanza, ni kweli kabisa kwamba fedha za miradi zinapopatikana inahitajika kuwa na maeneo mazuri yenye vigezo vinavyotosheleza kujenga miundombinu ya mradi husika. Mathalani kwenye upande huu wa elimu, maeneo inabidi yawe yanatosha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa fedha zinavyopatikana hazitakiwi kuchukua muda mrefu mpaka ujenzi unapokuwa unaanza. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kumwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri wafanye mipango ya utambuzi wa maeneo kwa ajili ya miradi hii ya kuendeleza miundombinu katika sekta hii muhimu ya elimu msingi ili pindi pale fedha zinapopatikana, basi maeneo yenye vigezo yaweze kuwepo kwa ajili ya kuanza kutekeleza miradi hii muhimu sana kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge kwenye eneo hili la Mlali ambapo anasema kuna uhitaji mkubwa sana wa shule nyingine ya sekondari, ni mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha kwamba inaendelea kuboresha miundombinu katika sekta hii muhimu kabisa ya elimu msingi. Ndiyo maana utaona kwamba katika Serikali ya Awamu ya Sita kuna mradi mahsusi kabisa wa kuboresha miundombinu kwa ajili ya elimu za sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu unaoitwa SEQUIP ni mradi wenye jumla ya thamani ya shilingi trilioni 1.2. Mpaka wakati huu, shule za sekondari ambazo zimejengwa ni 864 na Serikali inaendelea kujenga shule hizi. 
Mheshimiwa Naibu Spika, shule hizi zinajengwa mahsusi kabisa kwa ajili ya kupunguza msongamano darasani na pia kupunguza umbali mrefu ambao wanafunzi wanatembea ili kufika katika shule. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, ameuliza maswali yake haya ya msingi kabisa kuhusiana na hili eneo la Kikeo na Mlali kwamba Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea na hizi jitihada na itafika katika jimbo lake kuendelea kuboresha miundominu hii ya sekta hii muhimu kabisa ya elimu msingi.
							
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved