Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
											Name
Eric James Shigongo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buchosa
Primary Question
MHE. ERIC J. SHIGONGO aliuliza: - Je, Serikali inafahamu tatizo la uhaba wa walimu, hasa wa masomo ya sayansi nchini?
Supplementary Question 1
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Ni kweli kabisa kwamba walimu wamekuwa wakipatikana na wakiletwa Jimboni Buchosa, lakini Shule za Sekondari za Nyakarilo, Nyehunge, Katoma, Bupandwa na Maisome bado zina uhaba mkubwa sana wa walimu wa masomo ya sayansi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, nina maswali mawili ya nyongeza. Je, Serikali inaweza kufanya commitment kwamba itakapoajiri safari hii italeta walimu wa kutosha Jimboni Buchosa? 
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kutokana na uhaba huu, sisi Buchosa tumeamua kuanzisha mradi wa Buchosa Smart Classes ambapo tunatumia mtandao wa internet kufundisha watoto wetu. Mwalimu yupo Dar es Salaam, lakini anafundisha madarasa yaliyopo Buchosa. 
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Waziri yupo tayari kuja kutuzindulia mradi huu, na pia Serikali ipo tayari kutuunga mkono kwa kutupatia fedha tuweze kuunganisha shule nyingi zaidi? 
 
											Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
								NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA):  Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Eric Shigongo kwa kweli tunaona kazi kubwa anayoifanya ya uwakilishi katika jimbo lake. 
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la kwanza, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba Serikali inafanya jitihada kubwa sana ya kuhakikisha inaajiri walimu. 
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi hiki cha miaka minne, tayari walimu 45,742 wameajiriwa kwa ajili ya kufika katika shule zetu hizi kwenda kuwafundisha wanafunzi wetu. 
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea na jitihada hizi za kuhakikisha kwamba inaendelea kuajiri walimu pamoja na kutumia mikakati tofauti tofauti kwa ajili ya kuendelea kuboresha eneo hili la upatikanaji wa walimu. Kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge hata katika shule zake za sekondari Nyakarilo, Nyehunge na shule nyingine hizi zote alizozitaja ambazo zina uhitaji wa walimu wa sayansi, Serikali italeta walimu hao kwa ajili ya kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu iliyo bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili, ni kweli kabisa kwamba miongoni mwa mikakati ya Serikali ya kukabiliana na changaoto ya upungufu wa walimu ni pamoja na kutumia teknolojia ya TEHAMA katika kufundishia, yaani kwa maana ya kutumia madarasa janja (smart classes). Kwa hiyo, wanafunzi wanakuwa wanafundishwa kwa utaratibu wa ufundishaji mbashara. Mwalimu anakuwa yupo katika kituo kimoja kwa kutumia TEHAMA anaweza kufundisha wanafunzi katika shule zaidi ya moja, kwa wakati mmoja, kwa ufundishaji mbashara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza sana Jimbo hili la Buchosa katika halmashauri hii, kwa wenyewe pia kuona umuhimu sana wa kuendelea kuunga mkono jitihada hizi za Serikali za matumizi ya Smarty Classes katika mkakati wa kupunguza ukali wa upungufu wa walimu. 
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nitumie nafasi hii kumhakikishie Mheshimiwa Eric Shigongo kwamba nipo tayari kuungana naye kwenda katika Jimbo lake la Buchosa kwa ajili ya kwenda kuwazindulia hili darasa lao janja, ikiwa ni sehemu ya kuonesha na kuunga mkono jitihada hizi za matumizi ya TEHAMA kwa ajili ya kufundishia. (Makofi)
							
 
											Name
Grace Victor Tendega
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ERIC J. SHIGONGO aliuliza: - Je, Serikali inafahamu tatizo la uhaba wa walimu, hasa wa masomo ya sayansi nchini?
Supplementary Question 2
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Changamoto iliyopo katika Jimbo la Buchosa inafanana sana na changamoto ambayo ipo katika Jimbo la Kalenga. Kuna uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi hasa katika Shule ya Sekondari ya Muhwana ambayo ipo katika Kata ya Magulilwa ambako walimu wa masomo ya sayansi ni wachache, lakini pia hawana nyumba za walimu. Je, ni lini Serikali itawapatia walimu hawa nyumba kuwajengea?
 
											Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
								NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Tendega, kwa kweli amekuwa akifanya ufuatiliaji wa karibu sana wa masuala mbalimbali ya kimaendeleo katika Mkoa huu wa Iringa. Ninaomba nitumie nafasi hii kumweleza kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inafanya jitihada za makusudi kabisa kuhakikisha kwamba inaendelea kupata walimu wa kutosha kwa ajili ya kutoa elimu bora kwa wanafunzi wetu. 
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimhakikishie pia kwamba katika eneo hili shule hii aliyoitaja katika Kata ya Magulilwa nayo Serikali tutafanya mkakati mahususi kabisa kwa ajili ya kuleta walimu wa sayansi, ili waweze kuwafundisha wanafunzi wetu. 
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na uhitaji wa nyumba za walimu Serikali ya Awamu ya Sita inafanya uwekezaji mkubwa katika eneo hili. Katika uwekezaji wa miaka minne wa Serikali ya Awamu ya Sita katika sekta ya elimu msingi, zaidi ya shilingi trilioni 5.1 zimetumika kwa ajili ya kuboresha sekta hii msingi kabisa. 
Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa kazi kubwa katika hiyo shilingi trilioni 5.1 ni pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu ili walimu wetu wapate maeneo mazuri ya kufanyia kazi na maeneo mazuri ya kupata makazi, kwa maana tunaelewa kuna maeneo mengine ambayo wanaweza wakakosa nyumba za kupanga. Kwa hiyo, ili wapate utulivu Serikali inawajengea nyumba. 
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali itaendelea na jitihada hizi za kujenga nyumba za walimu ili walimu wetu wapate mazingira bora zaidi ya kufanya kazi.
							
 
											Name
Prof. Patrick Alois Ndakidemi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Vijijini
Primary Question
MHE. ERIC J. SHIGONGO aliuliza: - Je, Serikali inafahamu tatizo la uhaba wa walimu, hasa wa masomo ya sayansi nchini?
Supplementary Question 3
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi. Shule ya Sekondari ya Masoka iliyopo katika Jimbo la Moshi Vijijini ni ya mchepuo wa kilimo, lakini haina mwalimu wa kufundisha somo la kilimo. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutusaidia kupeleka mwalimu katika shule hii?
 
											Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
								NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Prof. Ndakidemi amekuwa akifanya ufuatiliaji wa hali ya juu wa masuala mbalimbali ya kimaendeleo katika jimbo lake. Ninaomba nitumie nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, haya ni maombi mahususi kabisa na tutayafanyia kazi ili tuweze kumleta huyu Mwalimu wa Kilimo katika Shule hii ya Masoka ili aweze kuwafundisha wanafunzi katika haya masomo ya kilimo. 
Mheshimiwa Naibu Spika, ninafahamu kwamba yeye ni mdau mkubwa sana wa kilimo nchini, kwa hiyo, tutatekeleza hili. Ninamwahidi kabisa Mheshimiwa Prof. Ndakidemi. (Makofi)