Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
											Name
Ritta Enespher Kabati
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga Kituo cha Afya Kata ya Endagau Jimbo la Hanang?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri. Kwa kuwa sera ya Serikali ni kujenga kituo cha afya kila kata na zahanati kila Kijiji; na Kata hii ya Endagau katika Wilaya ya Hanang’ vijiji vitatu vyote havina zahanati wala kituo cha afya. Je, kuna mkakati gani wa kuhakikisha kuwa wananchi hawa wanatendewa haki? 
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Kata ya Idete – Kimara – Ukwega ni kata ambazo zipo pembezoni sana mwa Wilaya ya Kilolo, lakini hazina vituo vya afya na barabara zao hazipitiki. Sasa hivi wagonjwa wanabebwa na machela. Je, ni lini sasa Serikali itaondoa mateso wanayopata wananchi wa kata hizi ambazo zipo pembezoni na hazina vituo vya afya? 
 
											Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
								NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza maswali hayo mazuri. Kuhusiana na hili swali la kwanza ambalo linahusu Halmashauri ya Hanang’, Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha miaka minne imefanya uwekezaji wa zaidi ya shilingi trilioni 1.29 kwenye upande wa afya msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari imejenga hospitali za halmashauri 129 na kukarabati hospitali kongwe 50. 
	Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi tu cha miaka minne vituo vya afya 367 vimejengwa. Utaona kabisa bajeti ya vifaa na vifaatiba imeongezeka maradufu katika kipindi hiki ambapo kabla, shilingi bilioni 35 ilikuwa ndiyo bajeti ya mwaka, lakini muda huu tunazungumza tangu Serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani, bajeti katika upande huu wa vifaa na vifaatiba imeongezeka mpaka shilingi bilioni 181; bajeti ya dawa na vitendanishi imetoka shilingi bilioni 96 mpaka sasa shilingi bilioni 116 kila mwaka.
	Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, utaona dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha sekta hii muhimu kabisa ya afya msingi. Ninaomba nimpe commitment na nimhakikishie Mheshimiwa Asia Halamga kwamba Serikali itafika katika vijiji hivi alivyovitaja kwa kutumia mapato ya ndani ya halmashauri, lakini kwa kutumia fedha kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya kuja kujenga zahanati katika vijiji hivyo, na kujenga kituo cha afya katika kata hiyo.
	Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali la pili la Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati katika kata alizozitaja katika Jimbo la Kilolo, ninaomba nimhakikishie na yeye kwamba ataiona dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita kwamba inaendelea kujenga vituo hivi muhimu kabisa vya kutolea huduma ya afya msingi. 
Mheshimiwa Naibu Spika, utaona kwamba katika mwaka huu wa bajeti shilingi bilioni 53.5 zimetoka kwa ajili ya kujenga vituo vya afya vya kimkakati katika katika kata 214 katika majimbo yote 214. Kwa hiyo, hata katika Jimbo la Kilolo tayari shilingi milioni 250 katika mwaka huu wa bajeti itafika kwa ajili ya kuendelea kujenga hivi vtuo vya afya. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kuboresha katika upande huu.
	Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na barabara kufika katika kituo cha afya alichokitaja ninaomba nitumie nafasi hii kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, kumwagiza Meneja wa Wilaya ya TARURA pamoja na Meneja wa Mkoa wa TARURA kwa pamoja waweze kushirikiana kuhakikisha kwamba miundombinu ya barabara inayoelekea katika huduma za msingi, kwa mfano kwenye hospitali zetu, kwenye zahanati, kwenye shule, kwenye maeneo yote yanayotoa huduma za msingi kwa wananchi waweze kuweka katika mipango ili iweze kuwepo kwenye bajeti kwa ajili ya kuchonga na kuimarisha miundombinu ya barabara hizo ili wananchi waweze kufikia huduma za msingi kabisa hizi. (Makofi)
							
 
											Name
Simon Songe Lusengekile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busega
Primary Question
MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga Kituo cha Afya Kata ya Endagau Jimbo la Hanang?
Supplementary Question 2
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, Kata yetu ya Kabita Jimbo la Busega ina population ya watu 36,000, lakini haina kituo cha afya na ipo kwenye orodha ya kata za kimkakati. Je, Serikali italeta lini fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kabita Jimbo la Busega? Ahsante.
 
											Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
								NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Simon Songe kwa swali hili lenye manufaa makubwa kwa ajili ya wananchi wake katika Jimbo lake la Busega. Ninaomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mwaka huu wa fedha na katika Jimbo lake hili la Busega watapokea shilingi milioni 250 kwa ajili ya kuanza kujenga majengo ya awamu ya kwanza ya kituo cha afya cha kimkakati. 
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo hili Mheshimiwa Simon Songe alipaza sauti yake na Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imemsikia na fedha hizi zinakuja katika mwaka huu wa bajeti kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo katika upande huu wa kituo cha afya. (Makofi)
							
 
											Name
Noah Lemburis Saputi Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arumeru-Magharibi
Primary Question
MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga Kituo cha Afya Kata ya Endagau Jimbo la Hanang?
Supplementary Question 3
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kulikuwepo na Kituo cha Afya cha Kimkakati cha Sambasha ambacho nacho kilitakiwa kupata fedha ambayo tuliiomba hapa Bungeni, je, ni lini sasa Serikali itakamilisha ahadi hiyo ya kupeleka fedha katika Kituo hicho cha Sambasha ili wananchi wapate kituo cha afya kwa ajili ya huduma? Ninashukuru.
 
											Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
								NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Noah Lemburis amekuwa akifanya ufuatiliaji wa masuala mbalimbali ambayo yanalenga kuleta maendeleo kwa wananchi katika jimbo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na ujenzi wa Kituo cha Afya cha Msambasha, ninaomba nimpe taarifa kwamba katika mwaka huu wa bajeti watapata shilingi milioni 250 kwa ajili ya kuanza kujenga majengo ya awamu ya kwanza ya kituo hicho cha afya ili kianze kutoa huduma na kuwanufaisha wananchi wake.
							
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved