Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
											Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Primary Question
MHE. STEPHEN L. BYABATO aliuliza:- Je, Serikali imefikia hatua gani katika jitihada zake za kuwekeza mtaji katika Kiwanda cha Kahawa cha TANICA - Bukoba Mjini?
Supplementary Question 1
MHE. STEPHEN L. BYABATO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa, ni kweli Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ilifanya tathmini na iliahidi kwamba itakipatia kiwanda, mtaji wa shilingi bilioni tano. Sasa ningependa kufahamu taratibu hizo za kuiwezesha TANICA kupata hiyo shilingi bilioni tano zimefikia wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Tumeona viwanda vingi vikikaa upande wa Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam na pembeni sana viwanda vingi vinakuwa haviji. Sasa ningependa kufahamu mkakati wa Serikali wa makusudi wa kuwezesha viwanda vinayojengwa pembezoni mwa Tanzania kuweza kufanya kazi ikiwemo Mkoa wa Kagera kwenye viwanda vya kahawa, viwanda vya maziwa na viwanda vya mazao mengine ambavyo ni vya wazawa? (Makofi)
 
											Name
Exaud Silaoneka Kigahe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Answer
								NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwanza ninachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Stephen Byabato kwa ufuatiliaji kwenye sekta ya viwanda na biashara na hasa katika Jimbo lake la Bukoba Mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, kiwanda hiki cha TANICA kina wanahisa wengi mmojawapo ni Serikali kupitia Msajili wa Hazina ambaye ana hisa 7.6% nilizozitaja, lakini kama unavyojua, Serikali hatufanyi biashara, lakini tumepata hisa kwenye viwanda hivi muhimu au kampuni ambazo zina tija kwa Serikali. 
Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanda hiki kiliomba fedha kutoka Serikalini shilingi bilioni 8.6, lakini katika majadiliano ilifikia hiyo shilingi bilioni tano ambapo ushauri ukaenda kwamba wakope kupitia Benki ya Kilimo. Sasa namwomba Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwanza tumesikia hoja yake, lakini Serikali inaendelea kufanyia kazi zaidi kwa kuwaelekeza waende kwenye Benki ya Kilimo ambako wataweza kupata hizi fedha.
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tunaomba utulivu ndani ya Bunge.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninawaomba Menejimenti na Bodi ya TANICA waendelee na ushauri tuliowapa Serikali kuomba mkopo TADB kwamba wapate hizo fedha bilioni tano, lakini zaidi tunatafuta wakekezaji ambao wanaweza kuingiza mtaji kwenye kiwanda hiki. Kwa hiyo, ninamshauri Mheshimiwa Mbunge kwamba aendelee kushikiriana na wenye kiwanda ambao ni wakazi wa Jimbo lake ili kuhakikisha wanaendeleza kiwanda hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, swali lake la viwanda ambavyo viko mbali na Bandari ya Dar es Salaam, maana yake ndiko amesema (Mtwara na Tanga). Serikali inafanya kazi kubwa hasa Serikali ya Awamu ya Sita kuweka miundombinu wezeshi kuanzia miundombinu ya barabara, reli na usafiri wa anga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba moja ya mikakati ya Serikali ni kuboresha miundombinu hii ambayo itawezesha hata wawekezaji waende kuwekeza katika mikoa mingine ya pambezoni ikiwemo kule Bukoba.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili; ni kweli kuna mkakati maalum ambao tunaangalia wa kuwapa vivutio mahususi ili wawekezaji wanaoenda mbali zaidi na Bandari ya Dar es Salaam kuwe na miundombinu wezeshi ili angalau kuhakikisha mtawanyiko; maeneo ambayo kuna rasilimali au malighafi waweze kuwekeza viwanda huko kuleta uchumi katika mikoa iliyopo pembezoni mwa nchi.
							
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved