Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Taska Restituta Mbogo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza: - Je, kwa nini Mahindi yanayovunwa kutokana na Mbegu za kisasa hayawezi kupandwa kwa mara ya pili?
Supplementary Question 1
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, tangu mwaka 2021 Wizara ya Kilimo ilianzisha utaratibu wa kusafisha, lakini kutambua mbegu za asili na pia kufanya utafiti ili mbegu hizo za asili ziweze kutumika kibiashara.
Mheshimiwa Spika, je, ni lini mbegu hizo zitaanza kutumika kwa sababu mwaka 2025 aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Bashe alizindua aina za mbegu 17 zikiwemo mahindi, maharage, na mbegu mbalimbali za karanga, mpunga na kadhalika. Je, ni lini mbegu hizo zitaanza kutumika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Mbegu ndiyo msingi wa chakula nchini Tanzania, lakini mbegu ndiyo msingi wa kilimo. Zipo kampuni za Kitanzania zinatengeneza mbegu zinaipatia Wakala wa ASA (Agriculture Seed Agency), lakini agency ya Agriculture Seed Agency hailipi haya makampuni ya Kitanzania ilhali ikijua kwamba mbegu ndiyo msingi wa kilimo.
Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itazilipa kampuni za Kitanzania zinazotengeneza mbegu nchini kwetu?
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, moja, ni kweli Serikali tunafanya utafiti. Pili, jukumu ambalo Mheshimiwa Rais ametuelekeza ni kuhakikisha kwamba tunalinda mbegu za asili. Jukumu hilo linafanywa na taasisi yetu ya TARI. TARI wameendelea kufanya utafiti wa kuhakikisha tunazilinda.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kuhakikisha kwamba zinaongeza tija ya uzalishaji kwa wakulima. Kwa hiyo, jambo hili limeshakuwa likifanyika na tumeshatambua mbegu kama Mheshimiwa Mbunge alivyoainisha mbegu 17 na matumizi yake yamekuwa yakitangazwa kwa wananchi kuendelea kutumia lakini bado uzalishaji wa mbegu za asili hapa nchini ni mdogo.
Mheshimiwa Spika, tatu, kwenye hili suala la mbegu asili, moja ya jukumu kubwa ambalo tunalifanya, kwa mfano sasa hivi kule Arusha tunajenga benki ya mbegu (gene bank) pale Seriani Arusha ili kuhakikisha tunahifadhi mbegu zote za asili katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme tu kwa wananchi, matumizi yanaendelea, lakini uzalishaji ndiyo bado haujawa mkubwa, watarajie tu kwamba tutakavyoongeza uzalishaji maana yake na usambazaji wake kwa wananchi utafika kama ambavyo tumekusudia.
Mheshimiwa Spika, kuhusu wakala wa mbegu wa Taifa nchini kwa maana ya ASA kutokulipa wadai wake ni kwamba walikuwa na changamoto ya kifedha na sasa hivi Wizara ya Fedha ilishatuahidi kutupatia fedha ili kuweza kuwalipa mawakala hao. Kwa hiyo, wapo ambao tumeshawalipa kwa awamu ya kwanza, wapo ambao tutawalipa kwa awamu ya pili na kuhakikisha kwamba wanaendelea na shughuli hiyo. Kwa hiyo, jukumu hili lipo, na tunalifanyia kazi, ahsante sana.
Name
Neema Gerald Mwandabila
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza: - Je, kwa nini Mahindi yanayovunwa kutokana na Mbegu za kisasa hayawezi kupandwa kwa mara ya pili?
Supplementary Question 2
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante, ninapenda kufahamu Wizara imechukua hatua zipi kutokana na changamoto iliyojitokeza ya mbegu feki kwa wakulima waliolima msimu huu?
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, ninamshukuru Mheshimiwa Neema Mwandabila. Ni kwamba, moja ya hatua ambazo Serikali tumechukua kupitia taasisi yetu ya TOSCI, imewakamata wale mawakala waliosambaza mbegu feki kwa wananchi na kuhakikisha kwamba tumewafutia leseni ili katika msimu unaokuja hawatafanya biashara ya mbegu hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, pia, tumeipa TOSCI jukumu la kuhakikisha wanaendelea kuelimisha wananchi kwamba kwenye kila mbegu inayouzwa hapa nchini inakuwa imeandikwa vocha ambapo mwananchi anakwangua ile vocha na kutuma zile namba katika ile kodi iliyowekwa pale chini ambapo ataitambua mbegu ile kwamba ni mbegu halali ama ni mbegu feki kwa sababu zile namba ziko registered na zinajitegemea kwa namba moja moja.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hatua ambazo tutaendelea kuzichukua ni kuhakikisha wale wanaokiuka tunawachukulia hatua za sheria. Pia nitoe rai kwa wananchi kwamba wahakikishe wanaponunua zile mbegu ambazo zimethibitishwa na TOSCI wahakikishe wanaituma kwa sababu ile namba ni bure ili kujua kama mbegu aliyonunua ni halali?
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, inatusaidia sisi ku-trace kumjua yule aliyesambaza ni nani, na kuwahi kuchukua hatua kabla, kuliko wananchi wanakuwa wamezitumia zile mbegu halafu wanakuja kuleta matokeo baadaye. Kwa hiyo, hiyo ndiyo hatua ambayo tunaifanya.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved