Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Yannick Ikayo Ndoinyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Primary Question

MHE. YANNICK I. NDOINYO aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga Barabara kutoka Kigongoni hadi Wasso – Ngorongoro kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 1

MHE. YANNICK I. NDOINYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa majibu ya Wizara. Nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa ile barabara inaenda kuifungua wilaya yetu kwa sehemu kubwa sana. Ni kwa nini Serikali inashindwa kuendeleza kile kipande cha kilometa 49 kinachoanzia Sale kuja Engaresero na imekaa kwa muda mrefu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la nyongeza, linahusiana na madaraja makubwa ya mito ambayo inatusumbua. Ni kwa nini, Serikali isitumie mpango wa dharura kujenga madaraja mawili ya Mto Moinik na Mto Athumani, ili yaache kusumbua na kuchukua maisha ya wananchi wetu? Ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Majibu, Mheshimiwa Naibu Waziri.

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemwelewa swali la pili kuhusu madaraja, lakini swali la kwanza sikumsikia vizuri Mheshimiwa Mbunge.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ndoinyo.

MHE. YANNICK I. NDOINYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nifafanue. Hii barabara ilikuwa inaitwa Loliondo – Kigongoni na ikaanza kwa kilometa 49 kutoka Waso hadi Sale na ikasimama kwa muda mrefu. Kwa nini, hicho kipande hakijaendelezwa badala yake inaanza mpya? (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri, umemwelewa?

Mheshimiwa Ndoinyo, ninaomba uzungumze kwa utaratibu. Lugha yako kidogo ni ngumu kwetu. (Makofi)

MHE. YANNICK I. NDOINYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Kiswahili hicho cha Kimaasai ni kigumu, ngoja niweke Kiswahili. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii barabara ilitengenezwa awali kilometa 49 ikasimama kwa muda mrefu, Waziri ametujulisha kwamba, wanaanza Kigongoni kwenda Selela na Selela kwenda Engaruka. Ninauliza, ni kwa nini kipande kipya kinaanza badala ya kuendeleza kile walichoanza mwanzoni? (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri, Umemwelewa sasa Mheshimiwa Ndoinyo? Ninafikiri sijui ni sauti kidogo au Mheshimiwa Naibu Waziri umemwelewa sasa? Majibu, Mheshimiwa Waziri.

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemwelewa kwamba, tulianza kule Waso – Sale. Sijamwelewa anataka kwamba, tungeanzia Sale kuja huku, ama! Yaani ndiyo kitu ambacho sijakielewa vizuri, ili tujibu vizuri.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ndoinyo, ongeza sauti kidogo.

MHE. YANNICK I. NDOINYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema Barabara hii ilikuwa inaitwa Loliondo – Mto wa Mbu, ikajengwa kweli kwa kuanzia Loliondo, maana ya Waso kuja Sale, ikasimama. Nilitegemea fedha zikipatikana ianzie Sale ije Engaresero na kwenda mpaka Kigongoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri ametuambia utaratibu uliopo ni kuanzia Kigongoni. Sasa kipande kingine tofauti kabisa kuelekea Selela na Engaruka, ndiyo swali langu. Kwa nini, waanze kipya badala ya kuendeleza kile walichoanza? (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza na swali la pili, ambalo nimelielewa vizuri, kuhusu madaraja yake mawili. Madaraja aliyoyasema, mawili, ni kweli yamekuwa ni moja ya madaraja ambayo yanasumbua sana unapotoka Mto wa Mbu kwenda Loliondo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Daraja alilolitaja la Moinik tumepanga kulijenga katika bajeti hii ya 2026/2027 na Daraja la Athumani ambalo lina urefu wa kama mita 80, tunavyoongea sasa, wapo wataalamu wanalifanyia usanifu, ili litangazwe kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha na lianze kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili. Ni kweli, tulijenga mwishoni, Waso – Sale kilometa 49 na tutajenga kutoka pale Sale kwenda Loliondo kilometa 10, ambapo ni Makao Makuu ya Wilaya. Katika hii barabara tumeanzia Mto wa Mbu kwenda Selela na Selela kwenda Engaruka kwa sababu, barabara ni hiyo hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli pia kwamba, pale Engaruka tunakwenda kujenga kiwanda kikubwa cha magadi. Kwa hiyo, ilikuwa ni muhimu sana katika hiyo barabara kwanza tujenge na ndio maana tumechukua mpango wa dharura kujenga hilo Daraja la Athumani, ambalo linakwenda kujenga kiwanda hicho cha Magadi (soda ash), ili kuweza kurahisisha usafari. Ni barabara hiyo hiyo ambayo Mheshimiwa Mbunge akitoka huku Makao Makuu ya Arusha atapita akiwa anaelekea Loliondo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango ni kujenga barabara yote baada ya Engaruka - Engaresero hadi Loliondo. Kwa hiyo, tumhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Mpango wa Serikali ni kuijenga yote, lakini tuliona kwanza hili eneo ni muhimu sana, la kimkakati na kiuchumi, tuweze kuimarisha usafiri, ili tuweze kuanza kuzalisha magadi. Ahsante.

Name

Fadhili Sandali Chilombe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kusini

Primary Question

MHE. YANNICK I. NDOINYO aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga Barabara kutoka Kigongoni hadi Wasso – Ngorongoro kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 2

MHE. ENG. FADHILI S. CHILOMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Barabara inayoanzia Tunduru Mjini – Mhesa – Nalasi mpaka Mchoteka imekuwa ikitolewa ahadi na Viongozi wetu wa Kitaifa kwa nyakati tofauti. Viongozi waliowahi kutoa ahadi pale ni pamoja na Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, aliyekuwa Rais wa nchi hii, Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli pamoja na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, juu ya barabara hiyo kujengwa kwa kiwango cha lami. Ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa barabara hiyo? (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kila ahadi za Viongozi wa Kitaifa ni kipaumbele cha Serikali kutekeleza hizo ahadi. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inaenda kutafuta fedha na pia, katika hiyo barabara hata kabla hatujaanza kuijenga kwa kiwango cha lami, tunachokwenda kukifanya ni pamoja na kuainisha maeneo korofi ili tuweze kuyaimarisha yawe yanapitika kipindi chote cha mwaka wakati tunatafuta fedha za kuijenga yote kwa kiwango cha lami. Ahsante.