Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Bakari Bakari Shingo
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Ukonga
Primary Question
MHE. BAKARI B. SHINGO aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani kukarabati kwa dharura barabara ya Nyerere katika maeneo ya Mombasa – Gongo la Mboto na maeneo ya makaburi ya Kiltex?
Supplementary Question 1
MHE. BAKARI B. SHINGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Swali langu msingi wake ulitokana na ujenzi huo wa barabara ambapo ujenzi huo umepelekea kuwa na mafuriko na Mheshimiwa Waziri analijua hili jambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya Mombasa kulikuwa na kalavati la asili pale lenye ukubwa wa sentimita 60, sasa hivi ujenzi huu wameenda kuweka kalavati lenye ukubwa kama sentimita 90 ama 120 ambayo imepelekea mafuriko, ndiyo ambayo swali langu la msingi lilivyokuwa linaelekea hivyo. Kumekuwa na mafuriko sasa Wizara iniambie inafanyaje kudhibiti yale mafuriko yasiende kuingia kwenye makazi ya watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa na tukio hilo pia lipo katika msikiti wa mashine ya maji kwamba pale tulikuwa na kalavati kubwa lenye ukubwa wa zaidi ya sentimita 120 sasa hivi ile njia imefungwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa hiyo kitendo cha kufunga na barabara imepanda juu kumesababisha pia mafuriko yanaingia kwenye misikiti na majengo ya wakazi eneo lile.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, hapo mwisho wa stendi ya mwendokasi palikuwa na kalavati, kalavati lile limeondelewa pakajengwa stendi kwa hiyo maji yamekuwa mafuriko na yanaelekea kwenye makaburi ya Kiltex ambavyo hivi ninavyozungumza inawezekana hata mabaki ya wanadamu yakawa yako juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ndiyo hoja yangu ipo hapo kwamba mpango gani wa dharura sasa wa hiyo shida ambayo imesababishwa na ujenzi wetu itakwenda kwisha?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tuna suala la stendi ya pale ubena, mmejenga barabara imepanda juu vizuri na stendi lakini hatukuweka service road, (sehemu ya kupita waenda kwa miguu) kwa hiyo imekuwa kama kisiwa, ndiyo msingi wa swali langu kwako.
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa naibu spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kwa pamoja ya Mheshimiwa Bakari Bakari Shingo, Mbunge wa Ukonga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hili analolisema tunakubali lipo, na bahati nzuri mimi hilo eneo kwa kweli nalifahamu vizuri. Nataka tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba TANROADS makao makuu, TANROADS mkoa waliokuwa wanasimamia ujenzi wa hiyo barabara ya DRT na wenzetu wa TARURA ambao sisi tuna ushoroba wetu ambao ni mdogo huko tunapokwenda kwenye makazi sisi hatutakiwi kwenda, lakini tunashirikiana na wenzetu wa TARURA kutengeneza hiyo mifereji na hasa baada ya kukamilisha huo mradi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nataka nitumie nafasi hii kumwelekeza Meneja wa Mkoa wa Dar es Salaam, TANROADS Makao Makuu waweze kumshirikisha Mheshimiwa Mbunge mipango ambayo ipo na wanachokifanya ili aweze kusaidia na kuwaelimisha na kuwaeleza wananchi Serikali inafanya nini ili kuondoa hiyo adha baada ya kukamilisha ujenzi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge watakushirikisha, watakupa mipango ya kufanya ili kuhakikisha kwamba baada ya ujenzi huu hatufanyi adha kwa wananchi ambao walikuwa na maisha ambayo hawakuwa na hayo mafuriko.
Name
Mwantumu Mzamili Zodo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. BAKARI B. SHINGO aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani kukarabati kwa dharura barabara ya Nyerere katika maeneo ya Mombasa – Gongo la Mboto na maeneo ya makaburi ya Kiltex?
Supplementary Question 2
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Barabara ya Handeni-Kang’ata-Negero-Mziha mpaka Turiani ni mbovu sana. Je, ni lini Serikali inakwenda kujenga barabara hii inayohudumia majimbo manne; Jimbo la Handeni Mjini, Handeni, Kilindi pamoja na Mvomero?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Barabara aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge tumeshaanza kuijenga kwa awamu na sasa hivi tumeshajenga mpaka pale Turiani na tunategemea katika bajeti hii tutaendelea kujenga kilometa 30, na malengo ni kukamilisha barabara hiyo kadiri fedha itakavyopatikana lakini tuna uhakika tumepanga kuendelea kilometa 30.
Name
Mashimba Mashauri Ndaki
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Magharibi
Primary Question
MHE. BAKARI B. SHINGO aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani kukarabati kwa dharura barabara ya Nyerere katika maeneo ya Mombasa – Gongo la Mboto na maeneo ya makaburi ya Kiltex?
Supplementary Question 3
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Barabara ya Njia Panda - Ikungu kwenda Malampaka kilometa 15, mkandarasi wake ametelekeza kazi na inasemekana ni kwa sababu ya malipo. Je, ni lini mkandarasi huyo atalipwa ili arudi kazini kuendelea na kazi yake? (Makofi)
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, iko miradi kadhaa ambayo tulikuwa tunatekeleza na wakandarasi wameshaleta certificate (hati za madai ya malipo) ambapo tuko tunaendelea kutafuta fedha na kuwalipa ikiwa ni pamoja na huyu mkandarasi ambaye Mheshimiwa Mashimba Ndaki amemsema. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sasa hivi kazi zote ni kuhakikisha kwamba kazi zote zilizokuwa zimesimama tunawalipa wakandarasi na wanarudi site ili kuendelea na kazi.
Name
Rashid Abdallah Shangazi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Primary Question
MHE. BAKARI B. SHINGO aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani kukarabati kwa dharura barabara ya Nyerere katika maeneo ya Mombasa – Gongo la Mboto na maeneo ya makaburi ya Kiltex?
Supplementary Question 4
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Lukozi kwenda Malindi mpaka Mlalo, takribani wiki moja sasa haipitiki baada ya mkandarasi kuweka kifusi ambacho hakina ubora. Je, ni mkakati gani wa dharura ambao utafanyika ili wananchi hawa wa Lukozi, Malindi mpaka Mlalo waweze kuwasiliana kwa haraka? (Makofi)
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, barabara aliyoitaja ni kati ya barabara ambazo kwenye ziara ya Mheshimiwa Waziri mkuu tulipita na akatolea maelekezo moja ilikuwa ni kwanza kuifanyia usanifu, na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tayari hiyo kazi imeshaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu matengenezo ya dharura, hiyo barabara ni barabara ambayo kuna mvua nyingi sana. Tuna wakandarasi ama tuna mkandarasi ambaye yupo standby. Nitumie nafasi hii kumwelekeza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga, mkandarasi huyo aende site akarekebishe yale maeneo ambayo hayapitiki. Lakini baada ya hapo tutasubiri mvua mpaka itakapokuwa imepungua ndio tutaitengeneza barabara yote, lakini kwa sasa ahakikishe anakwenda kurekebisha maeneo yote ambayo hayapitiki ili wananchi waweze kuwa na mawasiliano.