Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dougras Didas Massaburi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kivule
Primary Question
MHE. DOUGRAS D. MASSABURI aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa madaraja na Barabara ya Kitunda – Nyangasa – Kibeberu hadi Magole kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 1
MHE. DOUGRAS D. MASSABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali ya kaka yangu Mheshimiwa Naibu Waziri. Pia nachukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wa Wizara hii ya TAMISEMI na Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam, kwa kaka yangu Mheshimiwa Chalamila na DC wetu wa Ilala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 8 Mei, niliuliza swali linalohusu Barabara ya Banana – Kitunda mpaka Msongola na hatua za haraka zikachukuliwa. Ninaipongeza Serikali yangu, zaidi ya shilingi bilioni nane zimelipwa na sasa mkandarasi yuko kazini kukamilisha barabara hiyo kwa kiwango cha lami, lakini pamoja na pongezi hizo sasa ninayo heshima kubwa kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kivule, niulize maswali ya nyongeza, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza; tunayo barabara inayotoka Kampala University kupita Majohe mpaka Chuo Rada, kilometa 6.35. Swali la pili, ni barabara inayotoka Njia Nne kupita Buyuni – PSSSF mpaka Taliani, inaunganisha Jimbo la Kivule na Jimbo la zamani la Ukonga; na kwa kuwa Serikali yetu sikivu ilitupatia jimbo hili jipya la Kivule, changamoto kubwa ni miundombinu ya barabara na nyakati hizi za mvua kumekuwa na changamoto kubwa ya kupitika kwa barabara hizo. Basi angalau siku ya leo tupate majibu ya Serikali kwenye maswali yangu mawili ya nyongeza katika Wizara yetu ya TAMISEMI. Ahsante. (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza, nampongeza sana Mheshimiwa Dougras Didas Massaburi, Mbunge wa Jimbo la Kivule kwa uchapakazi wake na kwa kweli anawawakilisha ipasavyo wananchi wa Jimbo la Kivule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, napokea pongezi zake kwa Serikali yetu na kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa anayoifanya. Kwa kweli, kwa hakika Serikali ya Awamu ya Sita inafanya kazi kubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya barabara na katika Jimbo la Kivule, Mheshimiwa Mbunge ameshuhudia hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Barabara ya kutoka Kampala University – Magohe – Rada, kilometa 6.35 na Barabara ya Njia Nne - Buyuni, ni barabara muhimu sana ambayo inaunganisha wananchi wa Taliani – Magohe. Ni barabara ambazo kwanza kwa kutambua umuhimu wake Serikali imeshaziweka kwenye Mpango wa DMDP II, inakwenda kujengwa kwa ile 70%. Hivi sasa wanaendelea na taratibu za manunuzi ili kuhakikisha kwamba barabara hizi zinajengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa barabara hizi, Serikali imefanya maamuzi na sasa zitajengwa kwa kiwango cha lami. Kwa mfano katika mwaka huu wa fedha wakati tunajiandaa na ujenzi wa lami, imekwishatengwa shilingi milioni 20 kwa ajili ya matengenezo madogo madogo. Mwaka wa fedha 2026/2027 imetengwa shilingi milioni 950 kwa ajili ya ujenzi kiwango cha lami kilometa 0.6. Pia imetengwa shilingi milioni 100 kwa ajili ya matengenezo madogo madogo (periodic maintenance), na imetengwa shilingi milioni 20 kwa ajili ya matengenezo ya maeneo korofi. Barabara hii yote jumla yake ni kilometa 5.26 na zote zitajengwa kiwango cha lami kwa awamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo la Kivule kwamba Serikali iko kazini, itahakikisha barabara hizi zinajengwa na zinapitika vizuri kwa manufaa ya wananchi.
Name
Exaud Silaoneka Kigahe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Primary Question
MHE. DOUGRAS D. MASSABURI aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa madaraja na Barabara ya Kitunda – Nyangasa – Kibeberu hadi Magole kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 2
MHE. EXAUD S. KIGAHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Barabara ya kutoka Ifwagi – Mdabulo; kwanza ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutujengea lami kilometa 14 kutoka pale Mtili – Ifwagi.
Je, ni lini barabara hii itakamilika sasa kuendeleza ujenzi chini ya Mradi wa RISE kutoka Ifwagi – Mdabulo – Ibwanzi ambako pia kuna madaraja katikati yake?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, Mheshimiwa Exaud Kigahe, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini amefuatilia mara kadhaa kuhusiana na ujenzi wa Barabara ya Ifwagi – Mdabulo kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo la Mufindi Kaskazini kwamba Serikali tayari imekwishaweka utaratibu wa kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami kupitia Mpango wa Kuboresha Uchumi na Huduma za Jamii (RISE). Tayari tunaendelea na hatua za ujenzi wa barabara hiyo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hiyo itajengwa kwa wakati. Serikali ya Tanzania inashirikiana na Benki ya Dunia na kazi hiyo itafanyika.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafanya shughuli hiyo kuhakikisha kwamba barabara inajengwa kwa kiwango cha lami.
Name
Sikudhani Yasini Chikambo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DOUGRAS D. MASSABURI aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa madaraja na Barabara ya Kitunda – Nyangasa – Kibeberu hadi Magole kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 3
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, tunafahamu wakati ule wa mvua barabara nyingi ziliharibika na madaraja yamekatika. Leo nilitamani kulisemea daraja moja ambalo liko katika Kata ya Mindu, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, maarufu linaitwa Daraja la Mto Lwangula, limekatika, mawasiliano na wananchi hakuna, pale wanapita kwa shida. Tathmini imefanyika, takribani shilingi milioni 400 zinatakiwa kwa ajili ya ujenzi wa daraja lile.
Je, Serikali ina kauli gani katika kuhakikisha tunapeleka fedha na daraja lile linajengwa ili wananchi waendelee kunufaika na faraja hii ya Serikali yao ya Chama Cha Mapinduzi?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ni kweli kwamba ziko barabara nyingi na madaraja ambayo yameathirika na kubomoka kutokana na mvua ambazo zimenyesha sana msimu huu, na ndiyo maana kwanza Serikali ilifanya tathmini ya gharama zinazohitajika kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja hayo likiwepo daraja hili la Wilaya ya Tunduru ambalo Mheshimiwa Mbunge amelisemea na barabara zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa baada ya mvua kuwa zimepungua kwa kiasi kikubwa kote nchini, Serikali imekwishatoa maelekezo kwa Mameneja wote wa TARURA wa Mikoa na Wilaya kuanza kutangaza zabuni za ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja yote yaliyoharibiwa wakati wa mvua na shughuli hii inaendelea. Tunategemea mwishoni mwa mwezi huu wa Juni tutakuwa tumemaliza kupata wazabuni au wakandarasi na tutaendelea na hatua nyingine.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutatoa kipaumbele kwenye daraja hilo muhimu ambalo limeharibika katika Wilaya ya Tunduru.
Name
Edefonce Joackim Canoni
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Primary Question
MHE. DOUGRAS D. MASSABURI aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa madaraja na Barabara ya Kitunda – Nyangasa – Kibeberu hadi Magole kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 4
MHE. EDIFONSI J. KANONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Kalambo linapakana na Jimbo la Kwela, katika Kata ya Mkali Kijiji cha Myunga na Kata ya Kaengesa katika Kijiji cha Rula ni kilometa 22. Tathmini imefanyika kwa ajili ya kuunganisha hizi kata mbili na majimbo haya mawili; je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba inajenga barabara kilometa 22 kwa kiwango cha changarawe?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya kipaumbele cha Serikali ni kuunganisha kata na kata, jimbo na jimbo, wilaya na wilaya. Ni kweli barabara hiyo ambayo ameisema Mheshimiwa Kanoni ni barabara inayounganisha Jimbo la Kalambo na Jimbo la Kwela kule kwa Mheshimiwa Deus Sangu, Waziri wa Masuala ya Mahusiano. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutahakikisha kwenye bajeti ambazo tunaendelea tunapeleka fedha kwa ajili ya matengenezo ili kuwezesha barabara hii iweze kupitika vizuri hizo kilometa 22.
Name
Edwin Enosy Swalle
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupembe
Primary Question
MHE. DOUGRAS D. MASSABURI aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa madaraja na Barabara ya Kitunda – Nyangasa – Kibeberu hadi Magole kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 5
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza nimpongeze sana Naibu Waziri Mheshimiwa Dkt. Festo John Dugange kwa kujibu vizuri maswali ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa pale Mtwango eneo la Welela, kuna daraja moja limekatika kwenda Mawande. Pia liko daraja ambalo linaunganisha Welela na jimbo lake la Wanging'ombe, linaitwa Daraja la Sakalenga, limekatika, tumejenga kwa miti.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nimshukuru na nimpongeze sana Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, Mbunge wa Lupembe, Mbunge mahiri na mchapakazi kweli kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeshatoa maelekezo. Nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI kumsisitiza Meneja wa TARURA Mkoa wa Njombe, Meneja wa TARURA Wilaya ya Njombe na Meneja wa TARURA Wilaya ya Wanging'ombe, washirikiane kufanya tathmini kwenye eneo la daraja hilo la Welela ambalo linaunganisha maeneo muhimu ya Jimbo la Lupembe na Jimbo la Wanging'ombe na maeneo mengine ili katika 60% inayotangazwa tuhakikishe kwamba barabara hizo zinapelekewa fedha na tuanze kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa madaraja hayo.
Name
Ramadhani Hamza Singano
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bumbuli
Primary Question
MHE. DOUGRAS D. MASSABURI aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa madaraja na Barabara ya Kitunda – Nyangasa – Kibeberu hadi Magole kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 6
MHE. RAMADHANI H. SINGANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, katika Jimbo la Bumbuli kuna Kata ya Baga na Kata ya Makanya kupitia kwa Bogo, Kata ya Milingano na Mkomole na Dule 'B', wakati wa mvua zinakuwa haziwasiliani kabisa.
Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kujenga madaraja au vivuko katika kata hizi ili ziweze kuwasiliana muda wote?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge wa Bumbuli. Nimhakikishie tu kwamba moja ya hatua ambazo Serikali imechukua kwanza ni kuboresha aina ya barabara tulizozijenga na madaraja ili yasiathirike sana wakati wa mvua na kurudia kujenga kila mwaka maeneo hayo, utaratibu huo unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba kutokana na mvua barabara zetu zinazounganisha kata kadhaa alizozitaja Mheshimiwa Mbunge ziko kwenye mpango wetu wa 60% ya bajeti zetu kwa ajili ya matengenezo ili kuziwezesha kuweza kupitika vizuri.