Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Abdulaziz Mohamed Abood

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Mjini

Primary Question

MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD aliuliza: - Je, lini tatizo la mafuriko Kata za Lukobe na Kihonda litamalizika ambapo wananchi wamekuwa wakiathirika na baadhi ya nyumba kubomoka?

Supplementary Question 1

MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu haya ya Serikali, leo ni mwaka wa nne Kata za Lukobe na Kihonda wanaathirika kila mvua zinaponyesha. Wanapoona wingu watu wapanda daladala kurudi mjini kukimbia mafuriko. Tunataka jibu ambalo Serikali itamaliza kero hii ya Kata ya Lukobe na Kihonda. Je, Serikali itamaliza lini kero hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika hii miaka minne ya mafuriko wananchi wameathirika, nyumba zao zimebomoka na hasa kwa wanawake ambao walikuwa wajasiriamali ndiyo wamejenga nyumba zao na wastaafu. Je, Serikali haioni kuwa kuna umuhimu wa kuweza kuwafidia?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Abdul-Aziz Mohamed Abood, Mbunge wa Morogoro Mjini kwa namna ambavyo anawawakilisha kwa umahiri mkubwa wananchi wa Jimbo la Morogoro Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba eneo hili la Kata ya Lukobe na Kihonda limekuwa likiathirika mara kwa mara na mafuriko hususani wakati wa mvua na ndiyo maana Serikali katika kipindi hiki imeamua kuzitumia taasisi mbalimbali kufanya tathmini. Liko Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), wapo Bodi ya Maji Bonde la Wami-Ruvu, TMA, SGR, TARURA, Kamishna wa Ardhi wa Mkoa wa Morogoro na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeamua kushirikisha taasisi mbalimbali ili kupata suluhisho la pamoja na la kudumu kujua chanzo cha tatizo na njia sahihi ya kutatua changamoto hiyo ya mafuriko katika Kata za Lukobe na Kihonda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Morogoro Mjini na wananchi wa kata hizi kwamba Serikali ipo hatua za mwisho za tathmini na usanifu ili kuja na njia, mwarobaini wa kuondoa changamoto ya mafuriko katika kata hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la fidia, Serikali imeweka utaratibu, yako majanga ambayo yanakidhi vigezo vya kuitwa majanga na yako madhara ambayo huwa yanajitokeza kutokana na mazingira tofauti tofauti. Ili tuweze kufikia hatua hiyo ni lazima tujiridhishe kwamba vigezo vya majanga vimefikiwa.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali ya Mkoa wa Morogoro na Wilaya ya Morogoro wanaendelea kufanya tathmini, ikiwa madhara yale yatakidhi vigezo vya kuwa majanga, watawasilisha Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Maafa kwa ajili ya hatua stahiki.