Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Primary Question

MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: - Je, Serikali inatoa elimu bure au inatoa elimu bila ada?

Supplementary Question 1

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Kwanza ninafurahi kwamba Serikali imesema ni elimu bila ada, sio elimu bure. Ninaomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa sasa wanafunzi wa O-level na A-level wanapewa yaani fedha ya uendeshaji shule inaenda pale shilingi 1,500 kwa mwezi, lakini fedha hiyo ni kwa ajili ya mitihani, ulinzi, upishi, stationery, umeme, ukarabati, vifaa vya maabara, michezo, posho na extra duty. Je, hii fedha kwa maisha ya sasa, Serikali inadhani kwamba inaweza kusaidia kuendesha shule zetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili; ada ya shule, O-level ilikuwa ni shilingi 20,000 na advance level ilikuwa ni shilingi 40,000, lakini ninayo hapa joining instruction ambayo inaendeleza michango ya uendeshaji, sijui ma-counter book, mafagio, majembe, magodoro; ukihesabu hii michango inaenda shilingi 400,000 hadi 600,000.

Sasa swali langu ni kwamba Serikali haioni kwamba ni wakati sasa iache wazazi na walezi walipe ada kwa sababu ni nafuu kwao halafu yenyewe ibebe mizigo ya hii michango ambayo ni mikubwa sana? Ahsante.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Tarime Vijijini kwa kuwa mdau mzuri sana wa sekta ya elimu, lakini kwanza nakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua chanzo na msingi wa kuwa na Waraka Namba 03 wa Elimu na Mafunzo wa mwaka 2016.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na wimbi la wazazi au walezi kutokuwapeleka kabisa watoto shule kwa hofu ya kutoweza kulipa ada, kwa hiyo, enrolment rate ya wanafunzi ilikuwa chini. Wanaostahili kuingia darasa la kwanza na kidato cha kwanza walikuwa hawapelekwi na sababu kubwa ya wazazi ikiwa ni kwamba hawana ada ya kulipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua umuhimu wa elimu, ikaona iondoe kikwazo cha ada kwa kuanza kulipa yenyewe Serikali na wazazi wawapeleke watoto bila ada na hiyo ilileta matunda makubwa sana. Kuanzia Januari, 2016, wanafunzi wengi sana wa kidato cha kwanza, darasa la kwanza na hata shule za awali, waliweza kwenda shule. Kwa hiyo, dhumuni la Serikali lilitimia kwa eneo hilo kuhakikisha kwamba wanafunzi wote wanakwenda shule kwa umri unaotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Serikali imeendelea kutoa fedha. Kwa mfano, wanafunzi wote wa shule za msingi wanalipiwa, kila mwanafunzi shilingi 10,000 na wanafunzi wote wa sekondari wanalipiwa shilingi 25,000 kwa ajili ya shughuli za uendeshaji na uchapishaji, lakini pia wanalipiwa shilingi 20,000 nyingine, kwa ajili ya ada, kwa maana ya wanafunzi wa kutwa. Wanafunzi wale wa bweni wanalipiwa shilingi 70,000 nyingine kama sehemu ya ada na kila mwanafunzi analipiwa shilingi 1,500 kila siku, kwa ajili ya huduma ya chakula. Kwa hiyo, unaweza ukaona kiasi ni gani Serikali imeweza kutenga fedha nyingi kuhakikisha kwamba wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri na kuepusha changamoto za michango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuhusu hoja yake kwamba labda Serikali iache kulipa ada ili iweze kulipia michango mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaona umuhimu wa kuendelea kulipa ada kwa niaba ya wazazi na walezi ili kuwezesha wanafunzi kuendelea kusoma bila vikwazo. Ukiangalia waraka huu, umetoa maelekezo katika section 3.3 majukumu ya mkoa, section 3.4 na section 3.7 majukumu ya mkoa na wilaya kwa utaratibu huo na wanaelekezwa kufuata taratibu ikiwa kuna uhitaji wa michango muhimu kuwezesha wanafunzi kusoma wanashirikisha wazazi kwenye mikutano ya pamoja kati ya Kamati na Bodi za Shule na Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa wanathibitisha na wanachukua hatua pale ambapo inajitokeza michango isiyo sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nahitimisha kujibu swali la Mheshimiwa Waitara kwa kutoa wito kwamba Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya kote nchini na Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa wasimamie kwa karibu utekelezaji wa Waraka wa Elimu Namba 03 wa mwaka 2016 kwa kuzuia michango holela ambayo haijafuata utaratibu. Natumia nafasi hii pia kuwahamasisha wananchi wa Tanzania, wazazi na walezi kuona umuhimu wa kushiriki kuchangia elimu za watoto wao katika yale maeneo madogo madogo yanayohitaji ustawi wa watoto, ili watoto wetu wasome katika mazingira mazuri na tujenge Taifa lenye elimu bora kwa manufaa ya kizazi hiki na kinachokuja. Ahsante.

Name

Husna Juma Sekiboko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: - Je, Serikali inatoa elimu bure au inatoa elimu bila ada?

Supplementary Question 2

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana kuondoa kikwazo cha ada kwenye elimu ya msingi na sekondari, jambo ambalo limesababisha ongezeko kubwa la wanafunzi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa kikwazo hicho cha ada kwa elimu ya kati na hasa elimu ya ufundi ili wanafunzi wote hawa waweze kupata ujuzi unaostahili?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nampongeza sana Mheshimiwa Sekiboko, Mwenyekiti wa sekta hii ya elimu amekuwa Mwenyekiti bora sana na mwakilishi mzuri sana wa wanawake katika Mkoa wa Tanga na Watanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali hii ya Awamu ya Sita ni sikivu ambayo tunaendelea kufanya maboresho mara kwa mara kwa sekta ya elimu kadri ambavyo tutaona inafaa. Tuchukue mawazo hayo, kwa ajili ya kuendelea kuyafanyia kazi, ili tuendelee kuboresha sekta ya elimu katika elimu ya kati, vyuo na maeneo mengine. Ahsante.

Name

Asha Salum Motto

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: - Je, Serikali inatoa elimu bure au inatoa elimu bila ada?

Supplementary Question 3

MHE. ASHA S. MOTTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, Serikali inahakikishaje shule zote za Serikali zinatekeleza kikamilifu Sera ya Elimu Bila Ada?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Asha Motto kwa uwajibikaji na ufuatiliaji wa karibu wa sekta ya elimu. Namhakikishia tu kwamba Waraka ule Namba 03 wa 2016 umeelezea kila mdau na majukumu yake; ngazi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, Mikoa, Wilaya, Mkurugenzi, Kamati na Bodi za Shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imeelezea kwamba wajibu wa Serikali katika kila eneo ni kuhakikisha waraka unazingatiwa na kuepusha michango holela, kwa hiyo, nakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kupitia Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Wakuu wa Mikoa, inapitia mara kwa mara michango inayotolewa shuleni na wazazi na kujiridhisha kuwa ina sababu za msingi. Ikiwa haina sababu za msingi, Serikali inazuia na kuchukua hatua za kinidhamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kipengele namba 3.5 inaelezea kwenye ngazi ya mkoa na wilaya kwamba Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya watakuwa na wajibu wa kuchukua hatua pale ambapo kunakuwa na michango ambayo haijafuata utaratibu. Nakuhakikishia, Serikali itaendelea kusimamia utaratibu huo.