Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Shaffin Ahmedali Sumar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uyui

Primary Question

MHE. SHAFFIN A. SUMAR aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara kutoka Malumba- Mabama Centre- Mwigelezi kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 1

MHE. SHAFFIN A. SUMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti,
ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza na naishukuru sana Wizara kwa majibu mazuri lakini ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hii barabara ilitokana na
ahadi ya Mgombea Mwenza mwaka 2020 ambapo alipokuwa amepita kuomba kura ambaye sasa hivi ni Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuona mapokezi mazuri kutoka kwa wananchi, aliahidi kwa mapenzi yake kwamba ataijenga hii barabara. Hivi sasa tuna zaidi ya miaka mitano barabara haijawahi kufanyiwa kazi, lakini fedha pia zilizotengwa shilingi milioni 15 kwa ajili ya hii barabara ni chache sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna haja na hoja ya kumaliza hii
barabara haraka kwa sababu Mama Samia, anarekodi ya
kukamilisha ahadi zake kabla ya wakati. Niiombe sana Wizara, ituongezee bajeti barabara hii ikamilike ndani ya mwaka mmoja kwa sababu ni ahadi ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tuna barabara ya
kutoka Kijiji cha Mabama kuelekea Kijiji cha Ideka, Kijiji cha Tura mpaka Kijiji cha Katunda ambayo kwa miaka mingi
haijahudumiwa wala haijakarabatiwa na ina makorongo mengi sana. Nini kauli ya Serikali kuhusiana na utengenezaji wa hii barabara? Ahsante.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mbunge wa Jimbo la Uyui, Mheshimiwa Shaffin Ahmedali Sumar, na amekuwa mfuatiliaji wa mara kwa mara kuhusiana na uboreshaji wa barabara katika Jimbo la Uyui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie tu kwamba
kwanza ahadi za viongozi wetu wa kitaifa ni kipaumbele nambari moja kwenye bajeti zetu na ndio maana katika mwaka huu wa fedha tumetenga shilingi milioni 15 kwa ajili ya kufanya usanifu ili kuweza kutambua gharama halisi zinazohitajika kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kilometa 5.37 kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa taratibu za kitaalamu
tumejiridhisha kwamba shilingi milioni 15 inatosha kugharamia kazi ya usanifu, lakini baada ya usanifu sasa tutatenga bajeti kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii kiwango cha lami ili ahadi hiyo iweze kutekelezwa na wananchi wa Jimbo la Uyui waweze kufurahia matunda ya Serikali yao sikivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, nimhakikishie
Mheshimiwa Mbunge kwamba tunafahamu barabara za
Mabama na maeneo mengine ambazo Mheshimiwa Mbunge
amezitaja, ni barabara ambazo zimeathirika na mvua, lakini pia nyingine hazijafanyiwa matengenezo na ndio maana tupo
kwenye hatua za mwisho za kutangaza zabuni 60% ya bajeti ya TARURA Wilaya na Mikoa kote nchini ili kuhakikisha kwamba barabara hizi zinajengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutahakikisha pia barabara hizo
Mheshimiwa Mbunge, tunazipa kipaumbele.

Name

Amosy William Maganga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Primary Question

MHE. SHAFFIN A. SUMAR aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara kutoka Malumba- Mabama Centre- Mwigelezi kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 2

MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Misheni ni moja kati ya
kata zilizopo katika mji wa Sikonge na baadhi ya barabara zake zipo katika ahadi ya kujengwa kwa kiwango cha lami pamoja na kufungwa kwa taa za barabarani. Je, ni lini sasa Serikali itaanza utekelezaji wa mradi huo?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Engineer Maganga, Mbunge wa Jimbo la Sikonge, amefuatilia kuhusiana na ujenzi wa barabara hizi na tumekwishamhakikishia na nirejee kumuhakikishia kwamba tunatambua zipo barabara za ahadi, zipo barabara za kwenye mipango ya kila mwaka ya TARURA kuhakikisha kwamba zinajengwa kiwango cha changarawe na kiwango cha lami, lakini pia kuweka taa za barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nikuthibitishie kwamba
huo ndio mpango wa Serikali na ndio tamko la Serikali kwamba tutaendelea kutenga fedha kwa awamu kuhakikisha kwamba barabara hizo zinajengwa na wananchi wanapata huduma nzuri za barabara katika Jimbo la Sikonge.

Name

Simon Songe Lusengekile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Primary Question

MHE. SHAFFIN A. SUMAR aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara kutoka Malumba- Mabama Centre- Mwigelezi kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 3

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti,
ahsante sana na ninaishukuru sana Serikali kwa kutujengea
majengo mawili; Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Ofisi ya Mkurugenzi, lakini tunazo changamoto za barabara kutoka barabara kuu Mwagulanja kwenda kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi ambazo zimekuwa zikiharibika mara kwa mara na zinaendelea kuhudumiwa na TARURA.

Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba inazijenga
barabara hizi kwa kiwango cha lami ili kufikika kirahisi kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Songe Lusengekile, Mbunge wa Jimbo la Busega, lakini pia niwapongeze kwa kupata ofisi mpya ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi, lakini nimhakikishie
tu kwamba barabara zilizokwenda kwenye ofisi hizo kubwa katika wilaya ni kipaumbele cha Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na niitumie nafasi hii nimuelekeze
Meneja wa TARURA wa Mkoa wa Simiyu na Meneja wa TARURA wa Wilaya ya Busega, wafike katika barabara hizo wazifanyie tathmini na kujua kwanza kuziboresha kwa kiwango cha changarawe inagharimu kiasi gani, lakini pili kuboresha kwa kiwango cha lami inahitaji gharama kiasi gani ili Serikali tuweze kufanya maamuzi ya kuanza kuziboresha barabara hizo kwa awamu.

Name

Onesmo Merdson Mnkondya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbozi

Primary Question

MHE. SHAFFIN A. SUMAR aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara kutoka Malumba- Mabama Centre- Mwigelezi kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 4

MHE. ONESMO M. MNKONDYA: Mheshimiwa Mwenyekiti,
Jimbo la Mbozi Barabara ya Mlowo – Pito - Isansa ni kilometa 13.6 inaenda kwenye Kituo cha Afya Isansa muhimu kabisa, kwanza haipitiki na ipo kwenye ilani ya uchaguzi kujengwa kwa kiwango cha lami. Nini kauli ya Serikali kuhusu barabara hii kwa wananchi wa maeneo hayo ya muhimu sana? Ahsante.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Mnkondya, Mbunge wa Jimbo la Mbozi, lakini nikuhakikishie tu kwamba tunafahamu katika kipaumbele cha Serikali kupeleka barabara, moja ya maeneo ambayo ni kipaumbele cha hali ya juu ni maeneo ya huduma za jamii kama vituo vya afya.

Kwa hiyo, barabara hiyo ambayo inakwenda Kituo cha Afya
cha Isansa ni lazima ijengwe iweze kupitika ili wananchi wapate huduma za afya kwa urahisi, tunafahamu kuna wakina mama wajawazito, kuna masuala ya dharura lazima barabara ipitike vizuri ili ikitokea dharura wananchi waweze kupata huduma kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nikuhakikishie tu
kwamba msimamo wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunatenga fedha kwa ajili ya kuboresha na kukarabati barabara hizo na kwa sababu tunaendelea na utangazaji wa zabuni kuwapata makandarasi kwa bajeti ya 60%. Nitoe maelekezo kwa Meneja wa TARURA wa Wilaya ya Mbozi na Mkoa wa Songwe, waipe kipaumbele barabara hiyo inayokwenda kituo cha afya ili iweze kuboresha huduma za afya kwa wananchi katika maeneo hayo.