Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Primary Question

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: - Je, lini eneo la NDC njia panda ya Machame litaachwa kwa wafanyabiashara ili waweze kulitumia na kuanzisha mji mdogo wa kibiashara?

Supplementary Question 1

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Serikali kwa majibu mazuri sana, lakini na mpango mzuri sana.

Swali langu la kwanza, kwa kuwa wananchi wa Hai wako tayari na wamejiratibu kushiriki kwenye kuendeleza mji huu, na wako tayari kuwekeza kwenye mji huu, je, Serikali iko tayari sasa kupokea majina ya wananchi wa Wilaya ya Hai ambao wako tayari kujenga mji huo na kuendeleza kwa kujenga miundombinu mbalimbali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa sasa
mkandarasi mwelekezi ameshapewa kazi hii, je, Serikali iko tayari sasa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Hai ili mpango huo uweze kuingizwa kwenye mpango wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai na mpango huo uendane na matakwa na mpango kazi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Hai?

Name

Judith Salvio Kapinga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Saashisha, amekuwa akifuatilia jambo hili kwa kipindi kirefu sana na sisi ndani ya sekta yetu ya viwanda na biashara, nimhakikishie kwamba dhamira ambayo wananchi wa Hai wanayo, ndiyo dhamira ambayo sisi ndani ya sekta yetu tunayo. Eneo lile ni eneo la kimkakati na sisi tumekubaliana katika Dira hii ya 2050, pamoja na kufanya biashara na uchuuzi mwingine, lengo letu ni kuhakikisha tunajenga namna ya kuongeza thamani na mojawapo ni kuwa na kongani za viwanda na ndiyo mpango mzuri ambao tunao katika jimbo lake la Hai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, mshauri mwelekezi huyu ana kazi tatu za msingi; la kwanza kuandaa master plan kwa ajili ya mpango wa matumizi, lakini la pili usanifu wa miundombinu, na la tatu tathmini ya mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukikamilisha haya yote,
ninamhakikishia kwamba tutakaa vizuri na halmashauri ili tukubaliane, kwa sababu kongani yoyote inayojengwa hapo lazima iwe na mchango kwa shughuli za uzalishaji za wananchi
katika eneo husika.

Kwa hiyo nimhakikishie itakuwa kipaumbele, na wawekezaji wa ndani sisi tunawapenda na tunawakaribisha sana na kama watakuwa wanatokea katika eneo la Hai, na wenyewe watakuwa considered kwa ajili ya kuendeleza eneo hili muhimu ambalo limekaa kwa muda mrefu. Nikuhakikishie tunalipa
kipaumbele na kongani itaenda kujengwa hapo katika eneo la Hai. Ahsante. (Makofi)

Name

Ibrahim Mohamed Shayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Mjini

Primary Question

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: - Je, lini eneo la NDC njia panda ya Machame litaachwa kwa wafanyabiashara ili waweze kulitumia na kuanzisha mji mdogo wa kibiashara?

Supplementary Question 2

MHE. IBRAHIM M. SHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali kidogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Moshi Mjini ni mji ambao ulikuwa na viwanda vingi sana, lakini sasa hivi Moshi Mjini viwanda vyote vimekufa na kusababisha wananchi wale kukosa ajira. Je, nini kauli ya Serikali kuhusu kufufua viwanda hivyo?

Name

Judith Salvio Kapinga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante na namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake na ninakubaliana naye kwamba mojawapo ya maeneo ambayo yalikuwa na viwanda vingi sana ni pamoja na eneo la Moshi Mjini na kwa kuliona hilo, mwaka na nusu uliopita Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati anafanya ziara
katika Mkoa wa Tanga, alielekeza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wizara ya Uwekezaji, kufanya tathmini ya viwanda vyote ambavyo vimekufa na kuja na mkakati wa kufufua viwanda hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya sekta yetu ya viwanda na biashara tumeanza kuifanya kazi hiyo. Pale Tanga tayari tuna viwanda viwili vimeshafufuliwa na tumekutana na wawekezaji kwenye viwanda karibu 14. Kazi hii pia nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge itafanyika na Moshi Mjini. Moshi Mjini kulikuwa kuna
viwanda vingi, vingi vimekufa; Kiwanda cha KNCU, Kiwanda cha Kibo Match, Viwanda vya Kahawa, Kili Wood na kwa kuonesha dhamira ya Serikali, tumeshaanza kufanyia kazi. Kuna kiwanda
pale cha Timber (mbao), kuna Kiwanda cha Viuatilifu, kuna Kiwanda cha Kukoboa Kahawa, vyote hivi tumeshaanza kuviwekea mkakati na vimeanza kufufuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tunatekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Moshi pia tumeiweka katika mpango wetu wa miaka sita wa kuhamasisha viwanda na kufufua viwanda na tutaenda kuona matokeo hayo kwa kipindi kinachokuja kifupi. Ahsante.