Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Regina Christopher Malima
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. REGINA C. MALIMA aliuliza: - Je, lini Serikali itatunga sheria ya kuwalinda wazawa katika miradi ya uvuvi na vizimba?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. REGINA C. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa majibu ya Serikali na namna ambavyo Serikali imejipanga kuwalinda wazawa katika miradi ya uvuvi wa vizimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza; swali la kwanza, ikiwa sheria hizi zilizopo zinawalinda wazawa, kwa nini katika baadhi ya maeneo ikiwemo Kisiwa cha Ukerewe ambacho kinategemea zaidi ya 95% katika masuala ya uvuvi,
wazawa ni wachache katika miradi hii ya uvuvi wa vizimba ilhali wageni ni wengi katika miradi hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali ipo tayari kufanya tathmini ya kila katika Kisiwa cha Ukerewe katika masuala ya uvuvi wa vizimba ili na wao wawe wanufaika wa miradi hii badala ya kuwa watazamaji? Ahsante.
Name
Amb. Dr. Bashiru Ally Kakurwa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Answer
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Dkt, Regina Christopher Malima kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipende kulieleza Bunge lako kwamba mnyororo wa thamani wa ufugaji wa vizimba ni mrefu ukijumuisha uzalishaji wa vifaranga, uzalishaji wa vyakula vya samaki na kwa hiyo kuwezesha ushiriki wa wananchi kuweza kushiriki katika shughuli hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama kunaonekana kwamba wanapatikana watu wengi wageni ndio wanafanya shughuli hizo, sina uhakika sana na suala hilo kwa sababu ufugaji wa samaki kwa vizimba ni eneo jipya na kwa kiwango kikubwa Serikali ndio
imeweka nguvu kidogo ya fedha kuweza kuanzisha ufugaji huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo hamasa hiyo
inatakiwa iendelee ili upanuzi wa shughuli hizo uonekane dhahiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu tathmini kuhusu hali ya Ukerewe tupo tayari kufanya hivyo, lakini ninadhani ushiriki wa Wanaukerewe katika shuguli hizi tagemeana na upatiakanaji wa mitaji na hapa nihamasishe halmashauri za wilaya nchi nzima zianze kutenga fedha hasa zile za 10% kwa maeneo ambayo ya uvuvi kuelekeza huko badala ya kuwapa pesa wananchi kupika vitumbua na kuuza vitumbua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tupeleke maeneo ambayo hapa ni mapya ili wananchi waanze kunufaika na hapa nipende kutambua baadhi ya halmashauri kwa mfano kama Ilemela na Nyamagana wameanza kufanya hivyo na ushiriki wa wananchi unaongezeka na sisi kwa upande wa Serikali tutaendelea kutoa mikopo isiyokuwa na riba kubwa na muda sio mrefu tutaanza pia kutoa fedha ambazo Mheshimiwa Rais amezitoa na ninadhani na hakika Ukerewe pia watanufaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nihamasishe mabenki nayo yaanze kusaidia na baadhi yameanza kusaidia NMB wameanza, CRDB wameanza, Benki ya Ushirika nao wameingia nao pia waweze kuwawezesha wananchi wa maeneo ambayo yanaweza kufanya shughuzi za ufugaji wa vizimba wakiwemo Ukerewe waweze kupata mikopo na kushiriki katika shughuli hizo, ahsante sana.
Name
Tinnar Andrew Chenge
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. REGINA C. MALIMA aliuliza: - Je, lini Serikali itatunga sheria ya kuwalinda wazawa katika miradi ya uvuvi na vizimba?
Supplementary Question 2
MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti,
ninakushukuru kwa kuniona.
Kwa kuwa sasa hivi kuna upungufu mkubwa sana wa samaki kwenye Ziwa Victoria, je, Serikali haioni umuhimu wa kuja na sheria au mwongozo utakaoruhusu vifaranga vya samaki kuzalishwa
kwenye vizimba na baadaye vikarudishwa ziwani ili viendelee kukua na kuzaliana, lakini sambamba na kutenga maeneo maalum ambayo yatakuwa ni kwa ajili ya breeding na ambapo hakutaruhusiwa kuwa na uvuvi wa aina yoyote ile?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
Name
Amb. Dr. Bashiru Ally Kakurwa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Answer
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana Mheshimiwa Chenge kwa swali lako zuri lilo na ushauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio mwelekeo ambao tunakuwa nao, kama nilivyosema hili ni eneo jipya na linatusaidia kusema ukweli kuongeza uzalishaji wa samaki kwa sababu uvuvi wa asili samaki wameanza kupungua na kwa kiwango kikubwa ni kutokana na uvuvi usiozingatia sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo itabidi tufanye kazi
mchanganyiko, mbinu uchanganyiko, kwanza ufugaji wa samaki wa vizimba si mbadala wa uvuvi wa asili, lazima tuwekeze nguvu kubwa sana kulinda uvuvi wa asili kwa sababu ndiyo chanzo kikubwa cha mazao ya samaki kuliko huu uvuvi ambao ni mbadala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo Serikali
imejipanga kuleta sheria hapa Bungeni ili kuunda chombo Madhubuti/mamlaka ya uvuvi kuweza kusimamia raslimali za uvuvi ili tuongeze rasilimali na tuzilinde.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni hilo unalolipendekeza ambalo ni kuanza kufanya kitu kinaitwa restocking, kutengeneza vifaranga, halafu na kuvipandikiza, halafu na kutenga maeneo ambayo utapandikiza yawe yamehifadhiwa viweze kukua na
kuongeza uzalishaji wa samaki. Ahsante sana Mheshimiwa Chenge. (Makofi)
Name
Haji Kombo Mdowe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nungwi
Primary Question
MHE. DKT. REGINA C. MALIMA aliuliza: - Je, lini Serikali itatunga sheria ya kuwalinda wazawa katika miradi ya uvuvi na vizimba?
Supplementary Question 3
MHE. MDOWE HAJI KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri anayoendelea kutupatia hapa, lakini mimi nina swali
moja tu dogo la nyongeza ambalo ninapenda kujua ni mpango gani wa Serikali katika suala zima la kuongeza thamani mazao ya uvuvi ili kuongeza kipato kwa wavuvi wetu?
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, majibu.
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana ni kweli kuna haja ya kuongeza thamani ya mazao ya samaki ikiwa ni pamoja na kuwezesha viwanda vya samaki ambavyo vina..., samahani. Ili kuongeza thamani ya samaki itategemea kuongeza thamani ya...
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba arudie swali lake. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Haji, tafadhali ongeza sauti na Waheshimiwa Wabunge tunaomba utulivu ili muuliza swali na mjibu swali waweze kusikilizana.
MHE. MDOWE HAJI KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mimi swali langu ni dogo tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeomba kujua mpango wa
Serikali katika suala zima la kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi ili tuweze kuwasaidia wavuvi wetu kupata kipato zaidi. (Makofi)
Name
Amb. Dr. Bashiru Ally Kakurwa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Answer
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo tatizo kubwa la upotevu wa mavuno ya samaki baada ya kuvunwa na inafikia asilimia kama 30 ya upotevu (post-harvest loses). Ili kuongeza thamani itabidi kuwa na mifumo na teknolojia za kutunza samaki hao wasipotee na hasa mfumo wa vipozeo na Serikali iko inafanya mazungumzo na baadhi ya makampuni ambayo yana teknolojia za kutunza samaki ama kwa njia ya magari au kwa njia ya fridge na vifaa vingine vidogo vidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kwa mfano kwa upande wa dagaa, dagaa wengi hupotea uoza kwa hiyo tuna teknolojia pia ya ukaushaji wa hao samaki ili waweze pia kufika masokoni.
Kwa hiyo, Serikali ina mkakati kwa kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha kwamba wavuvi wanapata vifaa vya teknolojia vya kuhifadhi samaki baada ya kuvuna ili kupunguza kiwango hicho cha upotevu wa samaki kwa 30% ambayo ni kiwango kikubwa sana na kwa maana hiyo, hiyo itasaidia kuongeza thamani ya samaki nakushukuru sana. (Makofi)