Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Bakari Bakari Shingo
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Ukonga
Primary Question
MHE. BAKARI B. SHINGO aliuliza:- Je, lini ujenzi wa Barabara ya Pugu – Mnadani – Bangulo hadi Ulongoni B utaanza?
Supplementary Question 1
MHE. BAKARI B. SHINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninapenda nimjulishe tu kwamba, hii 0.3% kipande cha Mwembe Subu kuelekea Mwembe Kiboko, mkandarasi aliyekuwepo pale kwa awamu ya kwanza hadi tunavyozungumza leo bado miferiji haijajengwa, lakini pia hiyo 10% unayoizungumza kutoka Mwembe Subu kwenda Mwembe Kiboko, Mheshimiwa Waziri nimjulishe tu kwamba mkandarasi alifika kama ku-survey na alivyoondoka hajarudi tena. Kwa hiyo sijui hata 10% iko imepimwa kwa kiwango gani ama kwa kuanzia wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tu, nilitaka nijue tu, Mheshimiwa Waziri anatuambia nini kuhusu barabara ambazo nyingi zimeharibika kipindi hiki cha mvua na hazipitiki, ikiwa ni pamoja na Barabara za Zingiziwa, Barabara za Buyuni, na Chanika. Nyingi sana, imekuwa ni aibu sana, sehemu zingine tumeshuhudia akina mama ili wapite inabidi iwe kama wanavua nguo, kitu ambacho ni kinyume na ustaarabu wetu. Ahsante sana.
Name
Dr. Jafar Rajab Seif
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busanda
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Bakari Shingo, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema awali, tayari tathmini tumeshafanya katika majimbo yote na wilaya zote nchini na kuandaa bajeti ambayo itakwenda kujenga barabara hizi ambazo Mheshimiwa Mbunge ameziainisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge na kupitia Bunge lako Tukufu, nimwelekeze Meneja wa TARURA Kanda ya Dar es salaam aweze kuwasilisha tathmini na afike katika maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyaainisha hapa ili kuona namna gani ya kuweza kuanza na kuendelea kuratibu na ufuatiliaji wa karibu wa barabara hizi ambazo Mheshimiwa Mbunge ameziainisha, ninaomba kuwasilisha.
Name
Exaud Silaoneka Kigahe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Primary Question
MHE. BAKARI B. SHINGO aliuliza:- Je, lini ujenzi wa Barabara ya Pugu – Mnadani – Bangulo hadi Ulongoni B utaanza?
Supplementary Question 2
MHE. EXAUD S. KIGAHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Mufindi Kaskazini na hasa kata tatu; Kata ya Ifwagi, Mdabulo na Ihanu ni kata ambazo ziko ukanda wa juu kwenye mvua nyingi sana. Barabara kutoka Mkuta kwenda Ludilo - Irasa mpaka Ihanu imeharibika sana zaidi ya miaka mitatu sasa haijakarabatiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja kwenye jimbo langu pale Ifwagi, wananchi walileta malalamiko kuna wananchi hasa akina mama wanaojifungua, wanapoenda hospitali wanajifungulia njiani na wengine wanakufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa Serikali itakarabati barabara hii kutoka Mkuta – Ludilo – Ihanu - Mdabulo mpaka Irasa ili wananchi hawa waweze kusafiri kwenda kupata huduma za afya na mambo mengine?
Name
Dr. Jafar Rajab Seif
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busanda
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama alivyoliuliza kuhusiana na Jimbo la Mufindi Kaskazini kwa changamoto ya barabara ambazo ni mvua nyingi ambazo nchi yetu ilipokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa bajeti ambayo tumeitenga, TARURA itaendelea kwenda kurekebisha barabara zile ambazo Mheshimiwa Mbunge ameziainisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo la faraja ni lile ambalo kamati zetu zilishauri, lakini pia Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa maelekezo kwamba zile fedha za tozo ziende moja kwa moja kwenye Mfuko wa TARURA ili waweze kuzirekebisha barabara hizi kwa wakati.
Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wabunge wengine, tutaendelea kuelekeza fedha katika maeneo hayo ili kwenda kukamilisha miundombinu hiyo, ninaomba kuwasilisha.
Name
Hemed Sumry Haidary
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Mjini
Primary Question
MHE. BAKARI B. SHINGO aliuliza:- Je, lini ujenzi wa Barabara ya Pugu – Mnadani – Bangulo hadi Ulongoni B utaanza?
Supplementary Question 3
MHE. HAIDARY H. SUMRY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, Jimbo la Mpanda Mjini, Barabara ya Mlimani City kutoka Kata ya Nsemulwa kwenda Kata ya Uwanja wa Ndege, barabara hii ilitangazwa na akapatikana mkandarasi, lakini mpaka sasa hivi huyo mkandarasi hajaruhusiwa kufanya ile kazi na kuna daraja pale ambalo linaunganisha hizi kata mbili, wazazi ambao wanatakiwa kutoka kwenye Kata ya Uwanja wa Ndege kuja Kata ya Nsemulwa wanashindwa kupita kutokana na daraja hilo kutokamilika.
Ni nini kauli ya Serikali kuhusu mkandarasi kumruhusu ili aweze kuanza kazi ya ujenzi wa barabara hii?
Name
Dr. Jafar Rajab Seif
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busanda
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Mpanda Mjini kama alivyoliuliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tutambue, mpango wa Serikali ulikuwa ni kulipa madeni ya nyuma ya wakandarasi wote ili tunapoenda kuanza kutekeleza bajeti hii tusiwe na madeni mengi ya nyuma.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali imekwishalipa madeni mengi ya wakandarasi wa nyuma na fedha hizi ambazo tunakwenda kutekeleza bajeti ya mwaka 2026/2027 itakwenda moja kwa moja kwenye maeneo ambayo Serikali imeelekeza na hatutakuwa na madeni makubwa ya nyuma. Hivyo Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie na wananchi wa Mpanda Mjini kuwa tutaelekeza fedha katika daraja hilo na kumlipa mkandarasi ili aanze kazi. Kwa hiyo, ninaomba kuwasilisha.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved