Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Sikudhani Yasini Chikambo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuliza:- Je, lini Serikali itamlipa mkandarasi ili kukamilisha Mradi wa Maji Tunduru ambao umesimama?
Supplementary Question 1
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ni kweli kama alivyosema Naibu Waziri kwamba mradi ule unatekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru na kwa hakika wananchi karibia 75,000 watanufaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kwanza kuishukuru Serikali kwamba kwa pesa hizi ambazo wamepeleka shilingi milioni 500 ninashukuru sana zitamwezesha mkandarasi kurudi site, lakini nilitamani kujua, kwa kuwa mradi huu ulitakiwa ukamilike mwezi wa tano mwaka huu, ni lini sasa kiasi cha pesa kilichobaki kitapelekwa ili kukamilisha huu mradi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, pamoja na mradi huu ambao unatekelezwa katika viunga vya Tunduru Mjini, lakini uko mradi mwingine upo katika Kata ya Namwinyu, mradi ule ulitakiwa ukamilike mwaka jana mwezi wa saba. Wanufaika wa mradi ule ni vijiji viwili vya vya Namwinyu na Namakungwa. Kiasi cha pesa kilichobaki ni shilingi milioni 120. Nilitamani kujua na ule mradi utakamilika lini ili wananchi wetu waendelee kunufaika? Ahsante.
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sikudhani Yassini Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuendelea kufuatilia kwa ukaribu miradi inayotekelezwa ndani ya Halmashauri ya Tunduru, lakini pia niendelee kumuomba Mheshimiwa Mbunge kuendelea kufuatilia ili na sisi tunapopata jicho la pili katika utekelezaji wa miradi inatusaidia sana kujua mienendo ya wakandarasi ambao tunawapatia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe hofu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika huu Mji wa Tunduru ambao una majimbo mawili, tunafahamu pale kuna Mheshimiwa Ado Shaibu, lakini pia kuna Mheshimiwa Engineer Fadhili, ambapo ndani ya kipindi cha Bunge hili linaloendelea Mheshimiwa Rais ameshapeleka fedha, kwanza kabisa tulipeleka shilingi milioni 200, lakini sasa tumepeleka shilingi milioni 500, maana yake kwamba inaonesha dhahiri kabisa kwamba Mheshimiwa Rais amedhamiria kuhakikisha kwamba miradi hii inakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe hofu, mradi huu utakamilika, lakini pia tunatambua inawezekana ikawa nje ya muda ambao tulikuwa tumekusudia hapo mwanzoni, lakini nikutoe hofu, tutaongeza nguvu na tutamsimamia mkandarasi kwa ukaribu zaidi ili ahakikisha kwamba anakamilisha na maji yanatoka ili Watanzania wapate huduma hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili eneo la pili, nikutoe hofu pia kwamba huo mkakati wetu wa kuendelea kutatua changamoto za miradi inayoendelea si kwamba itawezekana miradi yote tukaikamilisha kwa pamoja, tutaenda awamu kwa awamu, lakini kama ambavyo nimesema katika majibu yangu ya msingi fedha hizi zimeshapelekwa. Pia tutaweka utaratibu mwingine wa kwenda kupeleka fedha katika eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge ameliomba. Ninakushukuru sana.
Name
Emmanuel John Khambay
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Babati Mjini
Primary Question
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuliza:- Je, lini Serikali itamlipa mkandarasi ili kukamilisha Mradi wa Maji Tunduru ambao umesimama?
Supplementary Question 2
MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri ya Mji wa Babati kuna mradi wa mabwawa manne ya majitaka. Tunaishukuru Serikali kwa kulipa fedha kwa certificate ya kwanza; certificate ya pili inahitaji shilingi bilioni 2.6 na tunaishukuru Serikali juzi kwa kutuwekea shilingi milioni 700.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itamalizia shilingi bilioni 1.9 ili mkandarasi aliyeondoka site aweze kurudi na kuweza kutatua changamoto au ukamilishaji wa mabwawa hayo ili wananchi waendelee kunufaika na huduma hiyo?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa, kwanza nimpongeze kwa kuendelea kuwapigania wananchi wake na kwa kufuatilia malipo ya wakandarasi. Pia tunatambua kwamba wakandarasi tunapowalipa hata ile fedha ndogo ukiwalipa wanashindwa kurudi site kwa sababu unakuta kwamba wame-engage na miradi mingi sana. Siyo miradi pekee yake ya maji, wanakuwa wame-engage na miradi mingine; TARURA, umeme, na kadhalika, kiasi kwamba ukimlipa ile fedha mara nyingine inaenda kulipwa benki na matokeo yake anashindwa kurudi site.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumeanzisha utaratibu mwingine tofauti wa kuhakikisha kwamba kabla hatujamlipa mkandarasi tunawaita na kukubaliana ili kuhakikisha kwamba ile security yake iweze kuwa specific kwa ajili ya mradi husika na pesa inapolipwa basi iende kutekeleza mradi husika.
Kwa hiyo, nimtoe hofu hii shilingi bilioni 1.9 ambayo imebaki pamoja na kumlipa shilingi milioni 700 hajarudi, tutamlipa hii shilingi bilioni 1.9 kuunganisha na ile ili ifikie ile certificate ya shilingi bilioni 2.6 aweze kurudi site na kuendelea na mradi ili Watanzania wapate huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana.
Name
Amina Mussa Mkumba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kibiti
Primary Question
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuliza:- Je, lini Serikali itamlipa mkandarasi ili kukamilisha Mradi wa Maji Tunduru ambao umesimama?
Supplementary Question 3
MHE. AMINA M. MKUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa uchimbaji wa visima 10 katika Kata ya Kibiti, Jimbo la Kibiti ili wananchi waweze kupata maji safi na salama? Ahsante. (Makofi)
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, uchimbaji wa visima 10 katika Jimbo la Kibiti ulikuwa ni mkakati wa Serikali kuchukua hatua za dharura ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama, na ninamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuendelea kukumbushia hili, na sisi lipo ndani ya vipaumbele vyetu ili kuhakikisha kwamba tunapeleka fedha zaidi na wakandarasi waweze kuhakikisha kwamba mradi huu unakamilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu miradi ambayo tunayo inayoendelea nchi nzima zaidi ya 1,206 ni mingi, lakini tutaendelea kuhakikisha kwamba tunatoa vipaumbele kwenye miradi ambayo ni ya kimkakati na ambayo ikitoa matokeo basi inaweza kuwa imetatua changamoto kubwa kwa wananchi. Nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge eneo lake tutalipata kipaumbele kwa ajili ya utekelezaji. Ahsante sana.
Name
Isack Joseph Copriano
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Monduli
Primary Question
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuliza:- Je, lini Serikali itamlipa mkandarasi ili kukamilisha Mradi wa Maji Tunduru ambao umesimama?
Supplementary Question 4
MHE. ISACK J. COPRIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri anajua fika kwamba kuna miradi Monduli ambayo inaendelea na kimsingi hali ya Monduli ya maji siyo nzuri.
Je, huoni sasa ni wakati muafaka mitambo ile ambayo Mheshimiwa Rais alinunua kwenye Kanda yetu ya Kaskazini ikaenda kuchimba baadhi ya maeneo kama Esilalei, Moita na Nagharami kuchimba mabwawa ili angalau basi iweze kuwasaidia wananchi pale wakisubiri maji yale ya vijiji 13 na vijiji saba yafike?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Isack Copriano, Mbunge wa Monduli kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuendelea kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ndani ya jimbo lake na pia kwa kuendelea kutupatia ushirikiano pale ambapo tunatoa taarifa za wakandarasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe hofu, mitambo hii Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliinunua kwa ajili ya Watanzania na sauti ya Mbunge ni sauti ya Watanzania. Sisi tunapokea na tutahakikisha kwamba mitambo hii itaenda kutumika kwa maslahi ya Watanzania hasa katika maeneo ya Monduli ambayo Mheshimiwa Mbunge ameomba, lengo kuu ni kuhakikisha kwamba upatikanaji wa maji yenye uhakika uweze kutokea katika Jimbo la Munduli. Nakushukuru sana.
Name
Charles Mhando Njama
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Korogwe Mjini
Primary Question
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuliza:- Je, lini Serikali itamlipa mkandarasi ili kukamilisha Mradi wa Maji Tunduru ambao umesimama?
Supplementary Question 5
MHE. CHARLES M. NJAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Korogwe Mjini wameahidiwa kupata maji kutoka katika Mradi wa Maji wa Miji 28, karibia ahadi tatu tofauti tofauti. Tuliahidiwa kupata maji mwezi wa tatu, baadaye tukaambiwa mwezi wa tano na mpaka sasa bado maji hayajaanza kutoka katika mradi ule wa miji 28.
Je, ni lini wananchi wa Mji wa Korogwe Mjini wataanza kupata maji kutoka katika Mradi wa Miji 28 wa Mwanga – Same - Korogwe? (Makofi)
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile package kwanza kabisa hatuna changamoto ya kifedha na pili mradi huu unaendelea vizuri kabisa na usimamizi wake uko vizuri kabisa. Tunatambua kwamba tulikuwa na matumaini ya kuukamilisha mapema, lakini miradi hii ni design and building. Sasa unapo-design na ku-build mara nyingine kunakuwa na kubadilika badilika kwa utaratibu wa namna ya kuutekeleza mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunafahamu kwamba tulikuwa tumeahidi mwezi wa tatu, lakini, haijatokea hivyo ni kwa sababu ya model ambayo tulichagua katika utekelezaji wa mradi huo. Nimtoe hofu mradi huu unaendelea vizuri kabisa na tunaamini kwamba bado tuko ndani ya muda wa mkataba ambao mkandarasi alikuwa amepatiwa.
Kwa hiyo, nimtoe hofu mradi huo tutaendelea kuusimamia kwa ukaribu ili uweze kutoa matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi wa Korogwe. Ahsante sana.