Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
George Natany Malima
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpwapwa
Primary Question
MHE. GEORGE N. MALIMA aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Daraja la Godegode kwa kuwa mkandarasi ameshapatikana?
Supplementary Question 1
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini, nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa mkandarasi alipatikana muda mrefu sasa, lakini ujenzi haujaanza, wananchi wa Godegode na maeneo yanayozunguka wanaomba kujua nini tamko la Serikali na lini malipo ya awali yatatolewa kwa mkandarasi ili ujenzi uanze ili wananchi waendelee kufanya shughuli zao za kiuchumi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, daraja hili linaunganisha majimbo mawili; Jimbo la Kibakwe na Jimbo la Mpwapwa na wananchi wa maeneo yote mawili shughuli zao za kiuchumi zimesimama kwa sababu ya kukatika kwa mawasiliano ya barabara.
Je, kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kujenga daraja la muda ili wananchi hawa wakati wanasubiri taratibu za Serikali zikiendelea waendelee kufanya shughuli zao za kiuchumi?
Name
Abdallah Hamis Ulega
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkuranga
Answer
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa George Natany Malima, Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza kuhusu ni lini? Ni kweli mradi huu umesisitizwa sana na ni maelekezo ya viongozi wetu, Mheshimiwa Waziri Mkuu hapa karibuni alipofanya ziara alitoa maelekezo haya na nimshukuru sana Mheshimiwa George Natany Malima kwa msisitizo wa kutukumbusha katika kuhakikisha kwamba wananchi wa hapa Mpwapwa na Kibakwe na uzuri daraja hili pia siyo tu Mpwapwa na Kibakwe, linaunganisha na Mkoa wa Morogoro, Wilaya ya Kilosa. Kwa hiyo, ni daraja muhimu sana na ni kiungo cha wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe hofu, tumeliweka katika priority kwamba zile mita 154 zote zimeshapata mkandarasi, fedha ya advance itakayokuja wakati wowote sasa tutamlipa mkandarasi yule katika kumtia msisitizo wa maelekezo ya viongozi wetu, Mheshimiwa Waziri Mkuu juzi alipofanya ziara katika Mkoa huu wa Dodoma.
Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa George Natany Malima na Wana-Mpwapwa, Kibakwe na hata Wilaya ya Kilosa kwamba mradi huu tunakwenda kuufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hapa mkoani Dodoma imeondosha hizi bottleneck nyingi ikiwa ni pamoja na kujenga madaraja tisa ya namna hii. Katika barabara kuu ya Morogoro kuja Dodoma tumejenga madaraja manne na barabara ya kutoka Dodoma kwenda Iringa tumejenga madaraja matatu na pale Chamwino Daraja la Nzali tumelikamilisha pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya shilingi bilioni 33.3 zimetumika. Kwa hiyo, ninataka niwahakikishie Wana-Dodoma, Wana-Kibakwe, Wana-Mpwapwa na Wana-Kilosa na Watanzania kwa ujumla, tutalipa jambo hili kipaumbele na nimpongeze sana Mheshimiwa George Natany Malima kwa kulipigania jambo hili kwa uzalendo mkubwa sana. Ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved