Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Suleiman Mohamed Rashid

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwera

Primary Question

MHE. SULEIMAN MOHAMED RASHID aliuliza: - Je, kero ngapi za Muungano zimetatuliwa mpaka sasa?

Supplementary Question 1

MHE. SULEIMAN MOHAMED RASHID: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze Serikali kwa hatua ambayo imefikia. Pia ninampongeza pia Naibu Waziri kwa majibu ambayo ameweza kutupatia. Nina maswali mawili ya nyongeza.

(a) Je, ni faida gani ambayo imepatikana baada ya utatuzi wa hoja 15 kati ya hoja 18?

(b) Je, ni mikakati gani ya Wizara ambayo imejipangia kuhakikisha hoja tatu ambazo zimebakia tunazitatua kabla 2030?

Name

Kwagilwa Reuben Nhamanilo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Suleiman Mohamed Rashid, amekuwa ni mfuatiliaji mzuri sana wa masuala haya ya Muungano, yeye pamoja na Wabunge kutoka Zanzibar pamoja na Wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2006 aliyekuwa Rais wetu, Mzee wetu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alitoa maelekezo ya kubadilisha namna ya kufanya majadiliano kuhusu hoja za Muungano. Hivyo, ilipelekea kuundwa kwa Kamati ya pamoja ambapo Kamati hii imeleta ufanisi mkubwa sana katika kushughulikia hoja za Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2006 hadi leo Kamati hii imepokea hoja 25, na katika hizo imeshashughulikia hoja 23 na kuzibakiza hoja mbili. Kwa hiyo, huo ulikuwa ni mkakakati mkubwa ndani ya Serikali wa kuhakikisha tunaweka mazingira mazuri ya kuondoa hoja hizi kwenye hoja za Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ndani ya Serikali tumeendelea kupitia timu mbalimbali za wataalamu kufanya mapitio ya sheria, mapitio ya kisera pamoja na kuandaa nyaraka mbalimbali kwa ajili ya kuiwezesha Kamati hii ya pamoja kufanya maamuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kamati hii ya pamoja kiutaratibu ambao tumeuweka inaongozwa na Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ametaka pia kufahamu faida ambazo zimepatikana kwa kuondosha hoja hizi za muungano ambazo zimekwisha fanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazitaja chache kwa sababu ni nyingi. Kwanza, ushiriki wa Zanzibar kwenye masuala ya Kimataifa na kikanda umekuwa bayana. Nafasi ya Zanzibar inaonekana kwa dhahiri katika ushiriki huo, katika kuandaa hoja na kuandaa msimamo wa pamoja kama nchi kwenye makubaliano ya Kimataifa tunapokuwa tumewasilisha hoja au kuhudhuria mikutano hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumeweka utaratibu mzuri wa shughuli za uvuvi kwenye ukanda wa uchumi wa bahari kuu. Tumeweka miongozo ambayo inaondoa migongano isiyokuwa ya lazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wafanyabiashara kutoka Zanzibar wameondolewa mzigo wa kulipa kodi mara mbili. Kodi ya mapato (Pay as You Earn) pamoja na Kodi ya Zuio (Withholding Tax).

Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo, kupitia kamati hii ya pamoja tumepelekea kuondoa hoja iliyokuwa ikitupa mkanganyiko katika mikopo ya Kimataifa inayohitaji dhamana na ile isiyohitaji dhamana ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninaomba kuwasilisha.