Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Abdallah Dadi Chikota
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyamba
Primary Question
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza: - Je, lini usambazaji wa gesi asilia majumbani katika Jimbo la Nanyamba utaanza?
Supplementary Question 1
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa mahitaji ya matumizi ya gesi ya majumbani ni makubwa kuliko Serikali inavyotenga fedha, je, haioni sasa ni muda mwafaka Serikali kushirikiana na sekta binafsi kwa ajili ya usambazaji wa gesi majumbani? Hilo moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kilometa 25 kutoka Mkuza gesi ilipo ambayo inatoka Madimba kwenda Dar es Salaam kuna kongani ya viwanda vya korosho pale Maranje Halmashauri ya Mji wa Nanyamba, na sasa hivi kuna wawekezaji wakubwa wawili wanajenga viwanda vya ubanguaji wa korosho takribani tani 200,000. Je, Serikali haioni umuhimu sasa kupeleka gesi asilia katika eneo hilo ikiwa kama motisha kwa wawekezaji? (Makofi)
Name
Salome Wycliffe Makamba
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Abdallah Chikota, yeye ni mbobevu katika sekta hii ya nishati ya gesi asilia na tunasambaza gesi majumbani kwa namna tofauti tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali kupitia TPDC inatandaza mtandao wa bomba la gesi kwa ajili ya kuhudumia majumbani na Serikali kwa kuona umuhimu na gharama kubwa sasa hivi Serikali imeshafikisha kwenye nyumba zaidi ya 2,000 na nyumba zaidi ya 1,000 zitasambaziwa katika mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumradhi. Ili kuweza kuongeza kasi, Serikali kupitia ushirikiano na sekta binafsi, tumeshaingia mkataba na kampuni zaidi ya tano ambazo zinasambaza gesi kupitia magari madogo (mini-LNG) na hii itaongeza kasi kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameshauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili, ni kweli kabisa Serikali imetoa maelekezo maeneo yote ambayo yana kongani za viwanda ambazo zina vichocheo vikubwa vya kiuchumi, tuhakikishe gharama za uzalishaji wa bidhaa zinazozalishwa kwenye viwanda zinakuwa ndogo na zinaweza kuwa ndogo kama tu kutakuwa kuna gharama ndogo za nishati ya uzalishaji wa bidhaa hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali, tunavyo vipaumbele vya kuhakikisha kwamba kwenye maeneo ambayo tunaweza tukapeleka mtandao wa bomba la gesi, tutapeleka ili gharama za uzalishaji ziwe chini. Ninakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge, mara baada ya kumaliza Bunge hili tutakuja kukagua na kuona uwezekano wa kupeleka bomba la gesi katika kongani hii ya viwanda ili kuweza kuchechemua uchumi wa maeneo ya Nanyamba na mikoa yote ya Kusini mwa Tanzania.
Name
Issaay Zacharia Paulo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Mjini
Primary Question
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza: - Je, lini usambazaji wa gesi asilia majumbani katika Jimbo la Nanyamba utaanza?
Supplementary Question 2
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Tunaipongeza Serikali kwa hatua kubwa inayochukua ya uunganishaji wa gesi katika taasisi ambazo zina watumiaji wengi na makundi makubwa. Katika Jimbo la Mbulu Mjini tuna shule nne ambazo kila shule ina wanafunzi zaidi ya 1,500. Shule za kidato cha tano na sita; Kainam, Chief, Tlawi, na Gehandu. Shule hizi ni lini Serikali itazifikia ili kuwaunganisha na mitungi ya gesi kwa ajili ya mapishi?
Name
Salome Wycliffe Makamba
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba taasisi zote zinazohudumia wananchi zaidi ya 100, zinaachana na kutumia kuni na mkaa na kwenda kutumia nishati ambayo ni safi. Suala hili limeanza kutekelezwa na Serikali mpaka sasa tumeshafikia zaidi ya taasisi 52. Tumetenga fedha katika mwaka huu wa fedha 2026/2027 kuweza kwenda kwenye taasisi nyingi zaidi. Nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, pole pole ndiyo mwendo, lakini naamini tutafika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii na jukwaa hili kuwaalika watu wa sekta binafsi, tunazo taasisi nyingi sana kama minada, masoko, bado wanatumia nishati ambayo siyo safi, jambo ambalo linawadhuru wale watumiaji, kuchafua mazingira na linawachelewesha kiuchumi. Milango yetu ipo wazi, wale wanaotaka kuwekeza waje ili tuweze kuhakikisha kwamba taasisi hizi zote ifikapo 2030 zinatumia nishati iliyo safi. Ninaomba kuwasilisha.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved