Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Jacquline Andrew Kainja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JACQUELINE K. ANDREW aliuliza:- Je, lini Serikali itaangalia upya gharama za uzalishaji wa Tumbaku ili Mkulima apate faida?

Supplementary Question 1

MHE. JACQUELINE K. ANDREW: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kupata nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Ninaipongeza Serikali kwa majibu mazuri, lakini kwa kuwa sasa masoko tayari yameshaanza, na bei iliyoko sokoni inaendelea kuwa chini, tofauti na hata bei elekezi iliyowekwa na Serikali ambayo ni dola 1.95, na sasa mkulima anapata dola 1.4, je, Serikali haioni kama mwananchi huyu anazidi kupata hasara zaidi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Kwa kuwa bei ya uzalishaji haiko sawa na bei halisi ya uzalishaji ya sasa. Je, Serikali haioni kuna haja ya kuweka ruzuku ya haraka kama ilivyowekwa kwenye mafuta ili kumnusuru mwananchi huyu?

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza dada yangu Mheshimiwa Jacqueline Kainja kwa maswali madogo mawili ya msingi kabisa yenye tija na faida kwa wakulima wa zao la tumbaku. Ni kweli anachokieleza ni kwamba kumekuwa na changamoto ya bei kama ambavyo nimeainisha katika jibu la msingi. Ni kweli kwamba bei ya tumbaku imekuwa ikibadilika kila nyakati, na sisi kama Serikali tumekuwa ni watu ambao tunaliangalia hilo ili kuhakikisha kwamba tunaongeza tija kwa mkulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunatambua kuna nyakati mkulima anaweza akapata bei pungufu ambayo inaweza kumpelekea hasara kidogo kulingana na mabadiliko ya kibei, lakini wajibu wetu sisi kama Serikali, ni kuhakikisha tunatengeneza mazingira bora na sahihi ambayo yatamsaidia mkulima kupata tija ikiwemo kupunguza bei kwenye pembejeo za zao la tumbaku ili kuhakikisha walau ana-cover ile gharama ambayo amekuwa ameingia. Kwa hiyo, kwa mfano, hili suala la bei; dola 1.9 na dola 1.4 maana yake sisi kama Serikali tutakaa na tutafanya tathmini upya ili kuangalia ni namna gani tunaweza kumsaidia yule mkulima?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuweka ruzuku, ni jambo ambalo Serikali imekuwa ikifanya. Tumefanya kwenye mazao mengi na kwenye tumbaku kuna wakati tulishajaribu. Bado tunaendelea kufanya tathmini na tukishamaliza hiyo tathmini tutakuja kuainisha kwa wadau wa zao la tumbaku ili kuona namna gani tunaweza kusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kwa kifupi ni kwamba, tumeanzisha Mfuko wa Agriculture Development Fund, mfuko wa pembejeo kwa ajili ya kilimo. Lengo la mfuko ule ni kusaidia changamoto hizi ambazo zinakuwa zinajitokeza hasa katika nyakati ambazo mkulima anakuwa hajatarajia kupata anguko la kibei.