Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mohamed Mussa Utaly
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lindi Mjini
Primary Question
MHE. MOHAMED M. UTALY aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi?
Supplementary Question 1
MHE. MOHAMED M. UTALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza ninaipongeza Serikali kwa namna ambavyo inashughulikia suala hili la Hospitali ya Rufaa ya Lindi. Hata hivyo, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa hospitali hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Disemba mwaka 2026, tuliokuwa nao, je, Serikali imejipangaje kuhakikisha kuwa mambo muhimu kama vifaatiba, mashine za kisasa, wataalamu bobezi wa afya wanapatikana mara tu ujenzi utakapokamilika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa Mkoa wa Lindi ni miongoni mwa mikoa inayokua kwa kasi kutokana na Uchumi wa Bluu na mradi wa Mkakati wa Gesi, je, Serikali imezingatia ukubwa wa hospitali hiyo kuendana na ongezeko la watu na mahitaji ya huduma za afya za baadaye? (Makofi)
Name
Dr. Florence George Samizi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mbunge Mohamed Utaly kwa kazi nzuri anayofanya kuwapigania wananchi wa Lindi. Kama nilivyosema, kwenye swali langu la msingi, Hospitali ya Lindi ni hospitali mpya ambayo imeanza kufanya kazi mwezi wa 12 kwa kuhama kwenye majengo ya zamani kwenda kwenye majengo mapya. Sisi kama Serikali tumejipanga kuhakikisha kwamba hospitali hii itakapoisha inakuwa na vifaa kamili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hospitali hii inavyo vifaa muhimu vya kufanya uchunguzi wa radiolojia kwa maana ya ultra sound machine, X-Ray machine, na CT-Scan na vyote hivyo vinafanya kazi. Hospitali hii inayo maabara ya kisasa yenye uwezo wa kupima vipimo vyote vikubwa kwa maana ya kibingwa. Inayo bio-chemistry machine, Cell Dyn pamoja na Haematology Analyzer.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali hii ya Lindi inatoa huduma za kibingwa katika fani tatu, lakini inayo wataalamu watano. Serikali imejipanga kupeleka watumishi sita kwenda kusoma ili tuweze kupata wataalamu wa kibingwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tumejipanga Hospitali ya Lindi kutoa fani za kutosha. Lengo letu ni kwamba ifikiapo 2030, Hospitali hii ya Lindi iweze kutoa fani za kibingwa 17 kama ambavyo Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alielekeza alipohutubia Bunge mwezi wa 11 mwaka 2025 kwamba tunatakiwa kufika katika huduma hizo za kibingwa 17. Kwa hatua za haraka, tutafanya msawazo wa wataalamu wa kibingwa ili waweze kufika Lindi kuendelea kutoa huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili linataka kujua tumejipanga vipi? Lindi inakua, Lindi ni mkoa wa kimkakati, na Serikali imejipanga kuendana na ukubwa wa mkoa huo. Ndiyo maana tumeihamisha kutoka hospitaki kongwe ambayo ilikuwa na eneo dogo na majengo chakavu, na tumeipeleka kwenye eneo jipya ambalo lina ekari 100. Hivyo, ninakuthibitishia Hospitali ile ya Lindi tunaweza kuipanua kwa kadiri tunavyotaka kwa sababu tayari eneo linatosha kuweza kutoa huduma hizo tarajiwa. Ninaomba kuwasilisha.
Name
Rashid Abdallah Shangazi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Primary Question
MHE. MOHAMED M. UTALY aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi?
Supplementary Question 2
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo, ni miongoni mwa hospitali za kwanza kabisa hapa nchini ikiwa imejengwa mwaka 1901, na sasa ina takribani miaka 125. Hospitali hii ni chakavu sana, wodi zake za Galanosi pamoja na Mwapachu na Sokoine zina hali mbaya sana. Hii Galanosi ni wodi ya mama na mtoto na iko katika hali mbaya sana ambayo zinahitaji kujengwa upya. Ni upi mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba wodi zake zinajengwa kwa haraka ili kuweza kuipa hadhi ya kuwa ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa? (Makofi)
Name
Dr. Florence George Samizi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Shangazi kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuwapigania wananchi wake wa Mkoa wa Tanga. Ni kweli kabisa Hospitali ya Bombo ni moja ya hospitali chakavu, lakini ninakuthibitishia, pamoja na uchakavu wake, inafanya kazi vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Bombo ni moja ya hospitali ambazo zinatoa huduma za kibingwa 10. Kwa hivyo inafanya vizuri sana. Sisi kama Serikali tumejipanga kuendelea kuboresha miundombinu ya Hospitali ya Bombo kwa kujenga wodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bajeti hii, tumetenga shilingi 1,000,000,000 ambayo itaenda kuanza ujenzi wa wodi za wagonjwa katika Hospitali ya Bombo. Siyo hivyo tu, tumetenga pia shilingi bilioni 1.6 ili kuweza kumalizia ujenzi wa Jengo la Damu Salama. Hivyo ninakuhakikishia, Serikali imejipanga kuendelea kukarabati hospitali kongwe zote ili ziweze kutoa huduma kulingana na wakati wa sasa.
Name
Alan Thomas Mvano
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kakonko
Primary Question
MHE. MOHAMED M. UTALY aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi?
Supplementary Question 3
MHE. ALAN T. MVANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada nzuri za Serikali yetu, kutoka Kigoma kwenda Bugando ama kuja Dodoma kufuata huduma za rufaa, imekuwa ni mbali sana. Dodoma zaidi ya kilometa 700, Mwanza Bugando zaidi ya Kilometa 600. Kwa kuwa Setikali imekuwa na mpango wa kujenga Hospitali ya Rufaa katika Mkoa wa Kigoma, ni lini sasa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa katika Mkoa wa Kigoma utaanza?
Name
Dr. Florence George Samizi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Ninampongeza Mheshimiwa Alan Mvano, Mbunge wa Kakonko kwa kazi nzuri anayofanya. Mkoa wa Kigoma unayo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa maana ya Maweni Hospitali ambayo inafanya vizuri na inatoa zaidi ya huduma 10 za kibingwa. Hata hivyo, Serikali kwa kuelewa mkakati wa Mkoa wa Kigoma, imetenga fedha shilingi 8,000,000,000 kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Kanda katika Mkoa wa Kigoma ili kuendelea kudumisha huduma bora katika kanda hiyo ya Mkoa wa Kigoma. Ninaomba kuwasilisha.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved