Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dickson Nathan Lutevele

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Primary Question

MHE. DICKSON N. LUTEVELE aliuliza:- Je, lini Serikali itaanzisha utaratibu wa kupima ardhi kwa bei nafuu kwa wananchi wa Kata za Isalavanu, Bumilayinga, Rungemba na Sao Hill?

Supplementary Question 1

MHE. DICKSON N. LUTEVELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa ninaipongeza Serikali kwa mpango huu ambao jimboni kwangu Mafinga umeanza. Kusema ukweli, umewavutia sana wananchi wengi kwa sababu, kabla ya Serikali kuachia upimaji huu kwa gharama ndogo wananchi walikuwa wanapata shida sana kupata gharama za upimaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu. Kwa kuwa, mpango huu umeivutia sana jamii na wananchi wengi wamehamasika, hasa wananchi wa maeneo ambayo upimaji haujafika, kwenye Kata zangu za Isalavanu, Bumilayinga, Rungemba, Sao Hill na Changalawe. Je, Serikali haioni kuwa, ipo haja ya kuongeza kasi ya upimaji kwa sababu, sasahivi kasi ni ndogo sana, ili wananchi wa kata hizi nilizozitaja waweze kufikiwa kupata huduma hii na upimaji ufanyike? Ahsante sana.

Name

Kaspar Kaspar Mmuya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Dickson Lutevele, Mbunge wa Mafinga Mjini. Ninaomba kwanza kukiri kuwa, vijiji ambavyo wamevitaja vya Salavanu, Bumilayinga, Rungemba na Sao Hill mimi ninavifahamu na nimeshawahi kuvitembelea katika nafasi mbalimbali. Ni vijiji ambavyo viko pembezoni mwa Mji wa Mafinga na hili hitaji la kupimwa kweli, bado lipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, ninaomba nimhakikishie tutaendelea kuongea na Mkurugenzi wa Mafinga, ili tuweze kupanga muda na jinsi ya kwenda kutekeleza upimaji wa vijiji hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi, mahitaji haya ya upimaji mara nyingi yanatolewa na Mkurugenzi katika eneo husika na sisi tunashirikiana naye, ili kuweza kufikia maeneo ambayo yana uhitaji wa haraka. Ninaomba kuwasilisha.

Name

Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Primary Question

MHE. DICKSON N. LUTEVELE aliuliza:- Je, lini Serikali itaanzisha utaratibu wa kupima ardhi kwa bei nafuu kwa wananchi wa Kata za Isalavanu, Bumilayinga, Rungemba na Sao Hill?

Supplementary Question 2

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Hivi karibuni tumekuwa na mgogoro mkubwa kati ya wafugaji na wakulima katika Jimbo la Bunda, Kijiji cha Sarakwa, ambacho kina wafugaji karibu 90%; wameamua kutengeneza blocks zao kwenye maeneo yao ya kuchungia. Sasa ni lini Serikali itaenda kwenye eneo hilo kuwapimia wale wafugaji maeneo yao, ili kupunguza mgogoro wa wafugaji na wakulima?

Name

Kaspar Kaspar Mmuya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakiri kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Boniphace kuhusu maeneo aliyoyataja katika eneo lake la Bunda. Ni ukweli ambao haupingiki kuwa, Bunge hili limefanya kazi kubwa ya kuiwezesha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutenga fedha zaidi ya shilingi bilioni 35, ambayo kimsingi, fedha hizi zitaenda kumalizia maeneo yote ya vijijini, ambayo hayajapangwa na kupimwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika upimaji huu tunashirikisha sana wananchi wa maeneo husika, ili waweze kutambua shughuli za kiuchumi ambazo zinafanyika katika maeneo yao, ili waweze kutenga maeneo. Hivyo, ninamwomba Mheshimiwa Boniphace kwa ushirikiano na Mkurugenzi na wenyeviti wa vijiji wawe tayari kuonesha maeneo ya mifugo, ili tukienda kupanga iwe rahisi kujua ni kiwango gani cha ardhi kitatengwa katika maeneo yao kulingana na idadi ya mifugo, ambayo ipo katika eneo hilo. Ninaomba kuwasilisha.